To Chat with me click here

Friday, February 1, 2013

MUHOGO UNAFAIDA NYINGI ZAIDI TUNAVYOFIKIRI


Zao la Muhogo mkombozi wa Mwananchi Tanzania
Zao la muhogo linalimwa karibu katika mikoa yote nchini. Karibu asilimia 48.8 ya zao hilo linalimwa ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi.  Asilimia 23.7 inalimwa katika mikoa inayozunguka ukanda wa Ziwa Victoria, asilimia 13.7 inalimwa katika ukanda wa Ziwa Nyasa, na asilimia 7.9 inalimwa ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Uwiano huo wa kuzalisha muhogo umekuwa ukipanda na kushuka kulingana na sababu mbalimbali. Katika maeneo hayo yote, zao la muhogo ni chakula muhimu kikifuatiwa na mahindi, mtama, uwele, mchele au ndizi, na viazi vitamu katika baadhi ya maeneo nchini.

Zao la muhogo lina uwezo wa kulifanya baa la njaa nchini kuwa historia. Zao hilo muhimu pia lina uwezo mkubwa wa kutokomeza umaskini uliokithiri vijijini ambako wakulima wadogo wanaishi kwa pato dogo yaani chini ya dola moja kwa siku (dola ya Marekani).

Muhogo ni zao ambalo lina soko kubwa la nje, tofauti na wengi wanavyofikiria.
Endapo muhogo utafanywa kuwa zao rasmi la biashara, kutaongeza hamasa kwa wakulima wa zao hilo, na hatimaye kunufaika.

Kuna mambokaribu kumi ambayo ambayo lazima yazingatiwe ili kufanikisha azma ya kusababisha muhogo kuwa zao la biashara kama mazao mengine.

Kwanza, lipo suala la kuzalisha mbegu za kisasa za muhogo, ambazo zitatoa mavuno mengi zaidi kuliko mbegu za jadi na kujenga mtandao imara wa kusambaza mbegu kwa wakulima kote nchini bila ukiritimba na mizengwe isiyokuwa na lazima.

Katika mpango huo  uzalishaji wa mbegu au vishina bora unapaswa  ufanyike katika vituo mbalimbali vya utafiti wa zao hilo katika maeneo mbalimbali nchini na kusambazwa kwa wakulima.

Pia wakulima wanapaswa kupewa mafunzo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuzalisha vishina hivyo.

Baadhi ya vituo hivyo ni Naliendele (ARI) mkoani Mtwara, Kibaha (ARI) Mkoa wa Pwani, Ukiliguru (ARI) Mkoa wa Mwanza, Maruku (ARI) Mkoa wa Kagera, Uyole (ARI) Mkoa wa Mbeya, Hombolo (ARI) Mkoa wa Dodoma, Tumbi (ARI) Mkoa wa Tabora, Tengeru (ARI) Mkoa wa Arusha,  na Kizimbani (ARI) Unguja visiwani.

Wakulima wanapaswa kupewa mafunzo ya kutosha katika kukabiliana na waadudu wanaoshambulia zao la muhogo pamoja na pembejeo nyingine.

Jitihada za kuimarisha kilimo cha muhogo ziende sanjari na utengenezaji wa mashine maalum za kusindika muhogo kwa njia za kisasa na kuzalisha unga wa muhogo wenye ubora wa hali ya juu (HQCF) ambao una soko kubwa hapa nchini na nje ya nchi.

Hivi sasa, kuna kiwanda au karakana moja tu nchini, mjini Morogoro yenye uwezo wa kufanya kazi hiyo. Hili ni jambo la aibu.

Karakana za aina hiyo ni muhimu ziwepo katika kila mkoa, na ikibidi katika kila wilaya. Ni teknolojia rahisi ya kisasa na yenye gharama nafuu .

Jaribio la kwanza la matumizi ya mashine hizo za teknolojia ya kisasa ya kusindika muhogo ili kupata unga bora (HQCF) , lilifanyika miaka 17 iliyopita (1997/98) katika Kituo cha Utafiti cha Naliendele Mtwara , katika vijiji vinne vya majaribio vya Makukwe, Nakahako, Mumbaka, na Mkarango, mkoani Mtwara.

Uthibitishaji wa Ubora wa Teknolojia hiyo ya kusindika mihogo kwa njia za kisasa na kuzalisha Unga Bora wa Muhogo  (HQCF) ambao ulifanywa na Taasisi Moja ya Utafiti ya NRI ya Chuo Kikuu kimoja cha Uingereza, pia kilihusisha baadhi ya taasisi muhimu nchini kama,  TBS/TFNC/SUA/SRI/TFDA, na taasisi nyingine kama Plan International, Naliendele ARI, RIPS Mtwara, TADENA (NGO).

Kutokana na kuanzishwa kwa mpango huo kuna vikundi visivyo pungua 8 vya wakulima wasindikaji (farmer groups/processors), katika Mkoa wa Pwani kuna vikundi visivyopungua 18 ,  na Zanzibar kikundi kimoja cha wasindikaji wa muhogo.

Plan Internationalni taasisi pekee iliyowahi kusambaza mashine 25 za aina hiyo katika Wilaya Kisarawe.

Teknolojia hiyo imeanza kusambaa polepole katika mikoa ya Mwanza na Kigoma. Lakini, bado ipo kazi kubwa.

Hivi karibuni wakulima wa Kijiji cha Tongwe, wilayani Muheza wamenufaika na matumizi ya teknolojia hiyo kwa msaada mkubwa wa watafiti za zao hilo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA) kwa Ufadhili wa Serikali ya Norway.

Mbali na hayo Serikali inapaswa  kutenga fungu maalum kwa ajili ya pembejeo na pia kuandaa utaratibu wa kutoa mikopo yenye masharti nafuu  kwa wakulima wa muhogo ili wanunue mashine za teknolojia ya kisasa ya kusindika zao la muhogo na kupata unga bora wa muhogo (HQCF).

Thamani ya zao la muhogo inatokana na matumizi yake. Mbali na unga bora wa muhogo, pia zipo bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao hilo (cassava byproducts), kama wanga ambao ni malighafi muhimu katika viwanda vya nguo, malighafi katika baadhi ya vifaa vya ujenzi (gypsum, ceramics),  na malighafi kwa ajili ya kutengeneza karatasi.

Pia malighafi ya muhogo inatumika kutengeneza baadhi ya vileo, chakula/kirutubisho cha mifugo, gundi ya viwandani (industrial glue), madawa mbalimbali (pharmaceuticals), na nishati ya Ethanol.

Kwa upande wa vyakula, muhogo una matumizi mengi sana ya kibiashara ambayo yanaweza kumwongezea mkulima kipato. Muhogo una wanga sana pamoja na madini ya Calcium, Phosphorous  na Vitamin C . Lakini una upungufu mkubwa wa Protini na virutubisho vingine.

Kisamvu kwa upande mwingine, ambako Kongo DRC, kinajulikana kwa jina la sombe’ au ‘mpondu’ kwa Kilingala au ‘sakasaka’ kwa lugha ya Kikongo, kina utajiri wa protini (Lysine), lakini pungufu katika Amino Acid.

Majani ya kisamvu pia yamekuwa yakitumika kama dawa (Herbal Remedies) katika madhara mbalimbali ya ngozi ya mwili kama majipu, madonda, na mambo mengine mengi.

Pia mmea wa muhogo umekuwa ukitumika kama tiba ya sumu ya nyoka (snakebites), Flu, kuhara ngiri, kuvimba macho, na mambo mengine mengi. Pia kutibu kansa.

Bado utafiti zaidi na wa kina utahitajika katika kuyatumia majani ya kisamvu na mmea mzima wa muhogo katika tiba kamilifu ya maradhi hayo yote na mengine ya ziada.

No comments:

Post a Comment