To Chat with me click here

Tuesday, January 8, 2013

WASSIRA ATAJWA VURUGU ZA CHADEMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, ametajwa kwamba anaongoza mtandao wa kukivuruga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kupitia Baraza la Vijana la Chama hicho (BAVICHA).

Wassira ametajwa jana na Mwenyekiti wa BAVICHA, John Heche, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya CHADEMA, Kinondoni Dar es Salaam.

Chini ya mkakati huo, Heche alisema Wassira amekuwa akishirikiana na Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA aliyevuliwa uanachama, Juliana Shonza.

Kutokana na hali hiyo, amesema mtandao huo ambao umekuwa ukifadhiliwa na waziri huyo, utavunjwa kwa sababu wameshaufahamu.

Aliwataja wanachama wengine waliokuwa wakishirikiana na Shonza ili kuhakikisha wanaibomoa BAVICHA kuwa, ni wajumbe wa baraza hilo, Habib Mchange, Mtela Mwampamba, Joseph Kasambala na Ben Saanane. 

Heche alisema Shonza kwa kutumia nafasi yake, alikuwa akishirikiana na baadhi ya watu kulisaliti baraza hilo kwa kuwatumia vijana wapenda mabadiliko.

“Katika kikao cha mkutano mkuu wa baraza hivi karibuni, tulijadili masuala mbalimbali ikiwamo tuhuma dhidi ya Shonza na alikutwa na makosa zaidi ya sita, ikiwamo kufanya mikutano na vikao vya siri kwa manufaa ya CCM.

“Shonza anadaiwa kukusanya vijana ambao ni wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali waliosimamishwa masomo au kufukuzwa vyuoni na kuwalaghai ili wakichafue chama na viongozi wa ngazi za juu. 

“Shonza alifanya kazi hiyo kwa ushawishi wa hongo, ili vijana wakubali kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kutoa matamko machafu dhidi ya CHADEMA na viongozi wakuu akiwamo Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa na Mwenyekiti wetu Freeman Mbowe.

“Katika hili tuna mfano hai ambapo katika kikao kilichofanyika katika Baa ya Highland Makumbusho kuanzia saa 9 hadi 11 jioni, aliwaita wanafunzi ambao ni viongozi wa CHASO (Umoja wa Wanavyuo wa Chadema), ambapo aliwashawishi wafanye mkutano na waandishi wa habari na kuisema vibaya Chadema.

“Desemba 6, mwaka jana, alifanya kikao kingine katika Hoteli ya MIC, hapa hapa Dar es Salaam, kuanzia saa 10 hadi saa 12 jioni kwa ajili ya kupanga njama za kukichafua chama na kutukana viongozi kwa manufaa ya CCM.

“Pia amekuwa akikutana na kufanya vikao vya siri na wenzake kupanga njama za kufanya hujuma dhidi ya CHADEMA na pia amekuwa akishiriki vikao vya kuanzisha chama kipya kinachoitwa CHAUMMA, amekuwa akishiriki katika makundi yaitwayo MASALIA na PM7 ambayo yote yalikuwa na lengo la kuvuruga chama na wanachama.

“BAVICHA imejiridhisha bila shaka, kwamba Shonza haendani na Katiba, falsafa, sera na maadili ya chama makini na tumaini la watu, CHADEMA.

Shonza ajibu mapigo

Akizungumzia uhusiano wake na Wassira, alisema hana mawasiliano yoyote na waziri huyo na kwamba hajawahi kukutana naye zaidi ya kumsoma na kupitia vyombo vya habari.

Pamoja na hayo, alisema atawasiliana na mwanasheria wake ili achambue kwa kina hatua alizochukuliwa na BAVICHA kisha atajua cha kufanya.

Wassira awashangaa Chadema

Naye, Wassira kwa simu jana kuhusiana na tuhuma dhidi yake, alikanusha madai hayo na kusema sasa Chadema kimepoteza mwelekeo.

“Hao ni waongo na nimeshawazoea kwa tabia yao ya kunisingizia pale wanapopata misukosuko, kwanza wanapoteza muda kunifikiria wakati wao wenyewe wamepoteza mwelekeo,” alisema Wassira.

No comments:

Post a Comment