To Chat with me click here

Wednesday, January 9, 2013

TENDWA AZUNGUMZIA UCHAGUZI MKUU 2015


Msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa

Msajili wa Vyama Vya Siasa Nchini, John Tendwa amekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kusimamisha mgombea wa Urais mwaka 2015 anayekubalika na Watanzania ili kukabiliana na changamoto za kisiasa zinazozidi kuongezeka hapa nchini.

Kadhalika, Tendwa amesema kuanzia sasa ofisi yake itaanza kuvifanyia uchunguzi vyama vyote vya siasa ili kubaini vile ambavyo havifanyi kazi za kisiasa na kuviweka katika madaraja.

Aliyasema hayo jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa kwa sasa changamoto za kisiasa hapa nchini zimezidi kuwa kubwa.
Alisema CCM ili kiweze kuvuka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ni lazima kisimamishe mgombea ambaye anakubalika na wananchi wengi.

Alitoa mfano kuwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimezidi kuwa na nguvu Bara na Visiwani na kwamba hiyo ni changamoto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Alisema mwaka 2012 vyama vya siasa vilikabiliwa na changamoto nyingi na kwamba sasa ni wakati wa kujiangalia na kujiandaa kwa ajili ya kushiriki uchaguzi mkuu ujao.

Alipendekeza kwamba vyama vinavyokuwa kisiasa na kufanikiwa kupata wabunge vinapaswa kupewa ruzuku ili kuviwezesha kufanya vizuri zaidi.

Akizungumzia siasa za Zanzibar, Tendwa alisema kwa sasa zimebadilika kutokana na muafaka uliofikiwa kati ya vyama vya CUF na CCM na hatimaye kuunda serikali ya umoja  wa kitaifa.

Kuhusu vyama vinavyoibuka katika uchaguzi na kufa baada ya uchaguzi kumalizika, Tendwa alisema mwisho wao umefika na kwamba vitajifuta vyenyewe. Aliongeza kuwa ofisi yake itaviweka vyama katika daraja la 1-3 na vile vitakavyoangukia daraja la nne na sifuri havitakuwa vinaalikwa na kutambulika kama vyama vya siasa.

Aidha, Tendwa aliwaambia wanadishi wa habari kuwa kuanzia sasa mfumo wa chama kupata wadhamini ili kisajiliwe utabadilika na badala ya kupata wanachama 200 kila mkoa katika mikoa 10 sasa watatakiwa watu 1,000 kila mkoa.

No comments:

Post a Comment