To Chat with me click here

Tuesday, May 14, 2013

LWAKATARE AENDELEA KUSOTA RUMANDE



WAKILI wa Serikali Mkuu, Prudence Rweyongeza ameendelea kumbana Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph akidai hawawezi kupata dhamana hadi Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), atakapowasilisha taarifa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Rweyongeza alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo wakati kesi dhidi ya akina Lwakatare ilipoahirishwa kwa sababu hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Aloyce Katemana yuko likizo.

Hoja ya kupinga dhamana ilibuuka baada ya Wakili wa utetezi, Peter Kibatala kuwasilisha maombi ya dhamana, akidai kosa linalomkabili mteja wake lina dhamana hivyo akaomba adhaminiwe.

Kibatala alidai washtakiwa hao wamebakiwa na shtaka moja lililochini ya sheria ya kanuni ya adhabu ambalo linadhaminika.

Shtaka hilo, ni la kula njama ya kutaka kumdhuru kwa sumu Dennis Msacky ambaye ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi ambako Jaji Laurence Kaduri,alisema linaweza kusikilizwa na Mahakama ya Kisutu.

“Mheshimiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,iliwafutia mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakiwakabili washtakiwa hao na kubakiwa na shtaka moja tu ambalo linadhaminika.

"Ingawa hakimu anayesikiliza shauri hili hayupo,tunaomba dhamana chini ya kifungu namba 148 (1,2)cha kanuni ya adhabu,ambacho kinasema mahakama inaweza kutoa dhamana na hasa ukizingatia ni haki yake kwa kosa linalodhaminika,” alidai Kibatala.

Kibatala alisema kuwa afya ya Lwakatare si nzuri, hivyo anaomba apewe dhamana kwa masharti atakayoona yanafaa.

Wakili Rweyongeza akijibu hoja hizo, alidai mahakama hiyo haiwezi kutoa dhamana kwa sababu DPP hajawasilisha taarifa yoyote Mahakama Kuu.

Hoja hiyo, ilipingwa vikali na Wakili Kibatala na kudai kuwa msimamo wa sheria upo wazi na umesisitiza kuwa mahakama za chini zina uwezo wa kutoa dhamana na kutoa mifano ya kesi mbalimbali za aina hiyo ambazo washtakiwa walipewa dhamana.

"Hakimu nayesikiliza kesi hii, nadhani atakuwapo baada ya siku 14, kama mnaona hamjaridhika mlango wa mfawidhi uko wazi, huna haja ya kuniomba mimi kwenda kumuona. Kesi itatajwa tena Mei 27, mwaka huu,"alisema hakimu Fimbo.

No comments:

Post a Comment