Askofu
Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Kardinali
Polycarp Pengo
|
Alisema kiongozi huyo na kuibua vifijo kutoka
kwa mamia ya waumini walioshiriki misa hiyo.
Dar Es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es
Salaam, Kardinali Polycarp Pengo amesema waumini wa kanisa hilo hawana sababu
ya kuingiwa wasiwasi kuhusu hali yake kiafya kwa kuwa anastaafu miaka mitano
ijayo.
Akihubiri
katika ibada maalumu ya misa iliyoandaliwa na Utume wa Wanaume Katoliki (Uwaka)
jimboni humo juzi, Kardinali Pengo mwenye umri wa miaka 70 alieleza kuwa
anajiandaa kustaafu kisheria, jambo ambalo halina sababu ya kuwaweka roho juu
waumini.
Katika
mahubiri yake ya muda mfupi kwenye misa hiyo iliyofanyika Kituo cha Kiroho
Mbagala, Dar es Salaam juzi Kardinali Pengo alitumia muda huo kuzungumzia afya
yake, akisema kwa muda sasa amekuwa haonekani hadharani kutokana na kuumwa.
Hata
hivyo, bila kutaja aina ya ugonjwa uliokuwa ukimsumbua, Kardinali Pengo ambaye
Machi mwaka huu aliadhimisha miaka 30 ya uaskofu na wakati ule ilielezwa kuwa
alikuwa mgonjwa asiyetakiwa kusafiri umbali mrefu, alitumia muda huo juzi
kuwashukuru waumini wa kanisa hilo na Watanzania kwa jumla kwa maombi yao
wakati wote alipokuwa akiumwa.
“Wapo
watu wengi walikuwa na wasiwasi kuhusu hali yangu, wengine si Wakristo,
walinipigia simu wakinijulia hali. Nawashukuru
wote kwa kuniombea, sasa nimepata nafuu.
“Najua
wengine wanashangaa kuona askofu wao akitembea namna hii, kwa mkongojo, hivi
ndivyo ilivyo, nilikuwa mgonjwa, lakini nawashukuruni nyote kwa kuniombea,
Mwenyezi Mungu awabariki,” alisema kiongozi huyo na kuibua vifijo kutoka kwa
mamia ya waumini walioshiriki misa hiyo.
Tofauti
na kawaida yake ya kuzungumzia mambo mengi katika jamii kwa kujiamini, katika
misa hiyo juzi, kiongozi huyo alitumia mahubiri yake kueleza kuwa kanisa hilo
ni taasisi iliyo imara na ambayo hata akiondoka katika uongozi, atapatikana
mwingine bila kuvuruga misingi iliyopo.
“Hata
kama afya yangu isingetetereka, nimebakisha miaka mitano, nitastaafu, lakini
hakuna sababu ya msingi ya waumini kuanza kuingiwa hofu yoyote kuhusu ni nani
atarithi nafasi yangu. Sisi (kanisa) tunao mfumo imara wa kupata viongozi
wetu.”
Pia,
Kardinali Pengo alikemea migawanyiko ambayo alisema imeanza kujitokeza katika
baadhi ya parokia za jimbo hilo, akisema haikubaliki.
“Nimesikia
minong’ono kuwa baadhi ya parokia, zipo nyingine zinajitangaza kuwa ni za
mashirika ya kitawa, sikubali, sitaki kuona hili likitokea, mwenye mamlaka
kusimamia parokia zote ni askofu, ni mimi,”alisema.
No comments:
Post a Comment