To Chat with me click here
Showing posts with label Katiba. Show all posts
Showing posts with label Katiba. Show all posts

Thursday, April 10, 2014

KAMA VITA IMEFIKIA HAPA, WAJUMBE WA TUME YA KATIBA WAJIHADHARI!

Tovuti ya tume ya katiba ionekanavyo baada ya kufungiwa na serikali

Serikali isiyo na soni. Imefunga tovuti ya tume ya mabadiliko ya katiba, eti lengo kuu ni kuhakikisha wananchi hawapati rejea na nyaraka mbalimbali ambazo zinaweza kusaidia uelewa na ufahamu wao. Sababu ya serikali ni kuwa, kazi ya tume imekwisha hivyo na tovuto yake haina kazi!!!!!!!!!

Serikali inayoogopa wananchi wake wasiendelee kuelimika, kujielimisha na kufahamu mambo muhimu ya nchi ni serikali ya ajabu sana.

Tovuti ni maktaba za kielektroniki, tume ya katiba ya Kenya hadi leo tovuti yao ipo hewani, tume ya katiba ya Ghana hadi leo inafanya kazi, ya Afrika ya kusini hadi sasa iko hewani baada ya miaka mingi ya kutunga katiba ya taifa hilo mara baada ya Madiba kuingia madarakani.

Hapa Tanzania, serikali iloituma tume kukusanya maoni ya wananchi sasa imekasirika, kwa hiyo inayapiga vita maoni ya wananchi, inaipiga vita tume ya mabadiliko ya katiba.

Serikali nyingi za kiafrika zina rekodi mbaya mno kila inapotokea matakwa yake fulani yamezuiwa na na watu fulani kwa njia halali.

Kwa chuki hizi za waziwazi dhidi ya tume na Wajumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba, natoa wito kwa wajumbe hao kuwa makini na nyendo zao na kutojiamini sana.

Ikumbukwe nchi hii watu wamewahi kung'olewa macho na wengine meno na vyombo vya dola viliishia kukamata wendawazimu na kuwapa mashtaka huku wahusika halisi waliotumwa kufanya kazi hizo za kinyama kwa maslahi tusiyoyajua wakitamba mitaani hadi leo.

Nasisitiza kuwa, ikiwa serikali ya kiafrika inafunga hadi tovuti yenye taarifa za maoni ya wananchi iliyokuwa wazi kwa umma, ni muhimu wajumbe wa tume wakajichunga sana. Mimi siiamini sana serikali hii ambayo leo inaweza kukutuma kazi na kesho asubuhi ikakugeuka na kukupiga vita wewe na kazi uliyoifanya.

Haya ni maoni na mtizamo wangu binafsi. Inatosha tu kuheshimu mawazo ya kila mtu.

By Julius Mtatiro, 
Mjumbe wa Bunge la Katiba,
Dodoma
09/04/2014

Friday, April 4, 2014

JAJI WARIOBA AVUNJA UKIMYA!


Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya katiba Jaji Warioba.

SIKU moja baada ya Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete kutoa taarifa ya kejeli na kumsuta Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, mwenyekiti huyo naye ameibuka kujibu mapigo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Jaji Warioba alisema ameiona taarifa ya serikali kuhusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lakini ameshangazwa na maudhui na lugha iliyotumiwa na Ikulu dhidi yake.

Majibu ya Jaji Warioba kwa Ikulu ya Rais Kikwete, yalitokana na taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ambayo ilimwita Jaji Warioba  mnafiki kwa kujifanya hajui ukomo wa tume yake.

Ikulu ilitoa taarifa hiyo baada ya gazeti moja juzi kumkariri Jaji Warioba akidai kuwa tume yake ilifukuzwa kazi na kwamba haikupewa muda wa kuandaa na kuwasilisha nyaraka za kukabidhi ofisi na madaraka na kwamba wajumbe wa tume hiyo waliporwa magari ambayo yamewekwa Ikulu.

Akitoa ufafanuzi wa taarifa ya Ikulu ya juzi, katika taarifa hiyo, Warioba alifafanua hivi:

“Kwanza, tume iliwaheshimu sana waheshimiwa marais wetu. Mafanikio ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yametokana na jinsi Mheshimiwa Rais wa Jamhuri na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar  walivyoiunga mkono na kuisaidia tume. Milango yao ilikuwa wazi wakati wote. Wakati wowote mimi kama mwenyekiti nilipoomba kuonana nao nilipata nafasi haraka na tume ilipoomba chochote, pamoja na kuongezewa muda hawakusita. Na wakati wote hawakutoa shinikizo la aina yoyote.  Makatibu wakuu viongozi nao waliisaidia tume kwa kiwango hicho. Heshima yangu na wenzangu kwa waheshimiwa marais na makatibu wakuu viongozi ni kubwa.

“Pili, tume ilikuwa haijamaliza kazi yake wakati inakabidhi ripoti kwa Mheshimiwa Rais. Tume iliendelea na kazi ya kuandaa Randama ya Rasimu, Bango Kitita la Rasimu na maelezo niliyotoa kwenye Bunge Maalumu. Serikali ilijua tulikuwa tunafanya kazi hiyo na nyaraka hizo zilikabidhiwa bungeni siku ya kuwasilisha Rasimu.

Tatu, wajumbe wa tume hawajatoa madai ya kulipwa shilingi milioni mia mbili. Hakuna mjumbe yeyote aliyetoa dai kama hilo na serikali inajua,” alisema Jaji Warioba.

Alisema alichozungumza ni muda wa kuandaa makabidhiano na kuandaa safari ya wajumbe kurudi makwao. Alisema aliwasilisha rasimu Machi 18, 2014, tume ilivunjwa Machi 19, 2014 wakati wajumbe wako Dodoma.

Tuesday, October 22, 2013

UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA UFANYIKE 2015


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba  

Jana  gazeti la Mwananchi lilichapisha habari katika ukurasa wa kwanza ikisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeomba kuongezewa muda wa mwezi mmoja kutokana na ugumu wa kazi ya uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na wananchi na asasi mbalimbali. Kama mambo yangekwenda kama ilivyotarajiwa hapo awali, Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 1 mwaka jana, chini ya Jaji Joseph Warioba ingekamilisha kazi yake Novemba 1, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Sura ya 83 ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Tume hiyo ilitakiwa kufanya kazi kwa miezi 18. Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Augustino Ramadhan alisema juzi kwamba wamepeleka serikalini ombi la kuongezewa muda wa kufanya kazi kutokana na kukabiliwa na kazi ya ziada ya kuchambua maoni hayo. Pamoja na Serikali kukiri kupokea ombi hilo, hadi tunakwenda mitamboni jana ilikuwa haijatoa jibu la kulikubali wala kulikataa.

Sisi hatuoni sababu yoyote inayoweza kuisukuma Serikali kulikataa ombi hilo, hasa kutokana na kujitokeza kwa mambo mengi ambayo hayakutarajiwa kabla na wakati wa mchakato wa Katiba Mpya. Mikutano ya Mabaraza ya Katiba iliyofanyika nchi nzima, kwa mfano ilizua tafrani kubwa ambapo wajumbe wa mabaraza hayo waligawanyika kwa misingi ya kisiasa na kiitikadi. Tume hiyo ililazimika kutumia muda mwingi kujielekeza katika kutoa tafsiri na kufafanua vifungu katika Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Pia Tume ilitumia muda mrefu kuratibu mijadala ya Rasimu hiyo, kwani wajumbe wengi wa mabaraza hayo walikuwa wakijadili hoja zilizotokana na misimamo ya vyama vyao badala ya kujadili rasimu yenyewe.

Hivyo, Serikali haina budi kukubali ombi hilo la tume haraka iwezekanavyo, pamoja na ukweli kwamba kuiongezea tume mwezi mmoja kuchambua maoni ya wananchi na asasi mbalimbali ni kuongeza gharama za mchakato huo. Lakini, wahenga waliposema maji ukiyavulia nguo ni sharti uyaoge, walipatia kabisa usemi huo, kwani kama tumeamua kama taifa kupata Katiba Mpya itakayotuvusha miaka 50 mingine ijayo lazima tubebe gharama hizo za kutuletea demokrasia ya kweli.

Ni vyema tukatambua kwamba hatua ya tume ya kuomba kuongezewa mwezi mmoja siyo ya ajabu. Sheria inaipa tume hiyo fursa ya kuongezewa miezi miwili nje ya muda uliowekwa. Kinachotakiwa sasa ni Serikali kujipanga vizuri na kutekeleza mambo mbalimbali kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015. Mambo hayo ni pamoja na kuandaa, kurekebisha na kupitisha sheria mbalimbali kwa lengo la kuondoa sheria kandamizi na kuweka sheria zitakazowezesha kuwapo mazingira linganifu ya ushindani wa kisiasa. Kwa mfano, inahitajika sheria mpya ya Tume Huru ya Uchaguzi.

Moja ya mambo muhimu ambayo Serikali inapata kigugumizi kuyatolea uamuzi ni suala la kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa sambamba na Uchaguzi Mkuu wa 2015. Muda uliobaki kati ya sasa na 2014 (ambao ulipangwa kufanyika) hautoshi kufanya maandalizi na uchaguzi ulio huru na haki. Uchaguzi huo ni vyema usimamiwe na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Hivyo, Tamisemi iliyokuwa ikisimamia chaguzi za Serikali za Mitaa na kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa wananchi itakuwa imeondolewa mzigo huo mzito. Kufanya uchaguzi huo wakati mmoja na Uchaguzi Mkuu kutapunguza gharama kwa kiasi kikubwa kama ilivyo katika nchi nyingi barani Afrika na kwingineko.

Wednesday, August 7, 2013

SERA, ITIKADI ZA VYAMA ZIKAE KANDO, KATIBA MALI YA WATANZANIA WOTE



Zanzibar.  Mabaraza ya Katiba yaliyosimamiwa na Tume ya Katiba kwa sehemu kubwa yametupa picha ya namna watu walivyokuwa wameyafikiria. Ingawa Tume ilitoa muongozo, wengi hawakuusoma au nisema hawakutaka kuelewa.

Tulichokiishuhudia ni baadhi ya wajumbe kutoka katika vyama vya siasa kushiriki katika mabaraza wakiwa na waraka mfukoni wenye maelekezo ya vyama vyao!

Ni jambo la kushangaza, lakini ndio demokrasia yenu ilipofikia kwamba watu wazima wanashindwa kujenga hoja wenyewe aina ya katiba wanaitakayo, wanasubiri kulishwa maneno kutoka kwa wanasiasa.

Ninaipongeza Tume ya Jaji Warioba kwa kuwa haikuruhusu taratibu na miongozo iliyowekwa na Tume hiyo kuvunjwa kwa makusudi, muda wote walisimama kwenye upande wa haki na pale alipozuka mtu akiwa na “waraka” wenye maelekezo alipigwa ‘stop’, ili aeleze ya kwake.

Siku chache baada ya kuanza kwa mabaraza tulimsikia Jaji Warioba akiwakosoa wajumbe wa mabaraza hayo waliokuwa wakienda  na matamko au nyaraka za vyama, badala ya maoni ya wananchi waliowachagua.

Inavyoelekea baadhi ya watu bado wana mawazo kuwa mfumo wa chama dola unaendelea katika nchi yetu na inawezekana mfumo huo umewalemaza baadhi ya watu kiasi cha kuingia woga hata katika yale mambo yenye uhusiano wa maisha ya kila siku.

Bado wanafikiri chama kushika hatamu katika wakati huu wa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Wanasahau kuwa Katiba ni mali ya wananchi, na ni wao wenye haki na mamlaka ya kueleza wanataka namna gani nchi yao iongozwe.

Wananchi ndio wenye uamuzi wa mwisho kuamua Katiba yao iweje na wala sio watawala wala vyama vya siasa vinavyoweza kujigeuza au kupora mamlaka na nguvu za wananchi.

Kwa maana hii sera za vyama vya siasa hazina upenyo wa kwenye suala zima la Katiba Mpya maana wananchi wanaweza hata wakasema kwa mfano hawaoni ulazima wa kuwepo kwa vyama vya siasa na badala yake wakapendekeza aina nyingine ya mifumo ya kidemokrasia ambayo inakubalika.

Sisemi kuwa tuachane na vyama vingi, la hasha, isipokuwa ninachora picha kwamba nguvu ya mwisho ya uamuzi katika nchi yeyote ya kidemokrasia ni kwa wananchi wenyewe.

Tunasimama pamoja na Tume ya Jaji Warioba kwa kitendo chao cha ushupavu katika kuona Taifa letu linapata Katiba ambayo inatokana na matakwa ya wananchi badala ya wanasiasa.

Kamwe tusikubali kufanya mambo kwa ajili ya maslahi ya muda mfupi, lazima tutangulize uzalendo kwa ajili ya kupata Katiba bora inayotokana na matakwa ya watu wenyewe na sio kundi fulani.

Ni wajibu wa wajumbe wa mabaraza ya Katiba kujiepusha na makundi maslahi kwa kuwa mwisho wa siku hata wao watakuja kuona uzuri au ubaya wa Katiba waliyoiandika.

Katika hili pia sina budi kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa nyakati tofauti amekuwa akisisitiza uhuru wa mawazo, kwamba kila mtu atoe mawazo yake mwenyewe bila ya woga wala wasiwasi.

Ni wajibu wake akiwa Rais wa watu wote kusimamia sheria na taratibu za nchi tulizojiwekea. Hapa Zanzibar wamejitokeza baadhi ya wajumbe wa mabaraza ya katiba wakiwa na maelekezo ya vyama vyao vya siasa, lakini tunashukuru Mungu Tume imesimama imara kuwaeleza haja ya wajumbe kuboresha Rasimu ya Katiba kwa mtazamo wao.
 
Sitaki kuamini kuwa mchakato wa Katiba tulioanza tangu mwaka jana ni kiini macho au kupoteza wakati na fedha, siamini hivyo kwa sababu suala la kuwa na Katiba mpya limepigiwa kelele siku nyingi,l akini pia tukiwa watu wazima hatuna sababu ya kudanganyana kwani Serikali ingeweza kujifungia na kuandika Katiba wanayoitaka kisha kuipeleka bungeni.

Kwa kuwa nchi yetu inaongozwa na Katiba na sheria pamoja na viongozi wenye dhamira ya dhati ya uongozi wao, hatuwezi kufanya mchezo wa aina hiyo ambao hauna faida kwao wala kwetu.

Ndio maana Rais Kikwete hakutoa matamshi ya kuwashurutisha wananchi kutoa maoni na mapendekezo yanayotakiwa na chama chake wala Serikali. Na wala serikali zote mbili –Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya  Mapinduzi Zanzibar hazikuwa na na msimamo wake katika suala la kupata Katiba mpya, wametuachia wananchi tuamue.
 
Ingekuwa Serikali ina maoni yake katika suala hili au ingetaka sera ya chama tawala ndio kiwe msingi wa kuandika Katiba mpya ingefanya hivyo na mambo kadhaa yangetokea;

Mosi, utoaji maoni ungekuwa ni wa kiini macho na kwamba Katiba hiyo isingekuwa imebeba matakwa ya wananchi bali maslahi ya watawala na kikundi fulani cha watu.

Suala la pili, hii ingedhihirisha kuwa wananchi bado lepe la usingizi halijawatoka, woga umetawala miongoni mwao na wanadhani Serikali ni mali ya watawala na kwamba mamlaka ya uendeshaji nchi haitoki kwao.

Hata hivyo, ukweli ni kuwa mamlaka ya uendeshaji nchi ni kwa wananchi wenyewe, lakini kwa kutokufahamu namna ya jinsi Serikali inavyopaswa kuendesha mambo yake au kwa sababu ya kutokujiamini kunakoambatana na utashi wa maslahi binafsi, baadhi ya watu wanaweza kuyumbishwa na wanasiasa au makundi maslahi.

Wapo wanasiasa na hata makundi maslahi yalijaribu kutaka kujipenyeza kwenye akili za wananchi, lakini hawakuweza kuwashawashi waliowengi na badala yake tumeona namna watu walivyotoa mawazo yao katika Tume ya Jaji Warioba.

Ni busara ya kawaida kwa wananchi tukaelewa kwamba vyama vyetu vya siasa havina mamlaka ya kuifanyia Katiba ya nchi mabadiliko, zile enzi za mfumo wa chama kimoja zimeshapitwa.

Sunday, May 5, 2013

BAREGU AIVURUGA CHADEMA

MSIMAMO WAKE KATIBA MPYA WAKITIKISA, DK. SLAA ASEMA ATAHUKUMIWA KAMATI KUU

Dr. Willbrod Slaa
Prof. Baregu
MSIMAMO wa mwakilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesigwa Baregu, kugomea agizo la chama chake lililomtaka ajiengue katika Tume hiyo ifikapo Aprili 30, umeonekana kukivuruga chama hicho.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, zinaeleza kugoma huko kwa Profesa Baregu kumeilazimisha Chadema kufanya maamuzi ya kuitisha Mkutano wa dharura wa Kamati Kuu kwa ajili ya kulijadili suala hilo, ikiwa ni pamoja na kufikia maamuzi ya kichama na hatua za kuchukua.

Hivi karibuni Chadema kilisema kuwa hakiridhishwi na mchakato mzima wa kutunga Katiba mpya, baada ya masharti kiliyotoa kwa serikali kikitaka kifanye mabadiliko kutotimizwa, na hivyo kumuagiza mwakilishi wao, Prof. Baregu ajitoe ndani ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba baada ya kujitoa kitaanzisha kampeni ya nchi nzima kuwahamasisha wananchi wasusie mchakato huo.

Hata hivyo, uamuzi huo wa Chadema ulipingwa na Prof. Baregu mwenyewe, ambaye alikataa kujitoa kwa hoja kwamba haoni kama kuna mambo yanapindishwa na serikali ndani ya Tume hiyo kama ambavyo chama chake kinadai.

Zikiwa zimepita siku tano (jana) tangu muda aliopewa Prof. Baregu na Chadema kujitoa katika Tume kuisha na yeye kugoma, kimesema kuwa suala hilo majibu yake yatapatikana kupitia kikao cha dharura cha Kamati Kuu kitakachoketi muda wowote kuanzia sasa.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema: “Suala hili alilitoa Mwenyekiti wangu na sina cha kuongea, nimekuwa najibu swali hili kwa waandishi mbalimbali wa habari, kwa ufupi jambo hili litazungumzwa kwenye kikao cha Kamati Kuu ya Chama. Sijui muda wala siku kwa sababu bado hakijapangwa.”

Wakati Dk. Slaa akiweka msimamo huo wa chama, baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa wanamshutumu Prof. Baregu kuwa amekataa kufuata maagizo ya chama chake kwa sababu ya malipo makubwa wanayopatiwa viongozi na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Taarifa ambazo hazijathibitishwa kutokana na wahusika kugoma kuzungumza zinaeleza kuwa, viongozi na wajumbe wa Tume hiyo kwa siku wanalipwa kiasi cha shilingi laki tano, ambapo kwa mwezi ni karibu na shilingi milioni 12-16.

Pamoja na hilo, juzi wakati Msemaji wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alipokuwa akiwasilisha hotuba yake kuhusu mpango wa makadirio ya mapato ya fedha ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014, alihoji matumizi makubwa ya mabilioni ya fedha za wananchi ndani ya Tume hiyo, akidai kuwa yanaashiria harufu mbaya ya ufisadi.

Alisema matumuzi hayo hayaelezeki wala kukubalika kwa misingi ya kisheria na kwa rekodi ya utendaji kazi wa Tume hiyo.

Lissu alihoji Bunge kuombwa tena kuidhinisha shilingi bilioni 33.944, kiasi kile kile kilichoidhinishwa mwaka jana kwa ajili ya matumizi ya Tume kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/14.

Katika mwaka wa fedha 2012/2013, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 33.944 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya Sheria za Tanzania.

Hata hivyo matumizi yake yamezua mashaka na kwa mujibu wa Lissu, kuna ulaji zaidi kwa wajumbe wa Tume hiyo.


Tuesday, January 8, 2013

MAONI YA CHADEMA JUU YA KATIBA MPYA YA TANZANIA


A.   JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MUUNDO WAKE

1.       Kutakuwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo itakuwa ni shirikisho lililoundwa na nchi ya Tanganyika na nchi ya Zanzibar.

2.    Kutakiwa na haki kamili ya kila nchi inayounda Jamhuri ya Muungano kujitoa katika Muungano lakini haki hiyo itatumiwa kwa masharti kwamba uamuzi wa kujitoa katika Jamhuri ya Muungano lazima upate ridhaa wa upande husika kwa kura ya maoni (referendum/plebiscite) kwa idadi isiyopungua theluthi mbili ya kura zote halali.

3.     Kutakuwa na Serikali ya Muungano ambayo itakuwa na madaraka juu ya mambo ya Muungano pekee. Mambo ya Muungano yatakuwa yafuatayo:
(a) Mambo ya nje yanayohusu masuala ya diplomasia lakini yasiyohusu ushirikiano wa kimataifa;
(b) Ulinzi na usalama isipokuwa kwa masuala ya polisi na magereza;
(c) Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano (Supreme Court of the United Republic);
(d) Uraia na uhamiaji;
(e) Sera za fedha na sarafu;
(f) Sera za biashara ya kimataifa na masuala ya forodha;
(g) Masuala ya ithibati ya elimu ya juu.

4.    Kutakuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa Mkuu wa Serikali ya Muungano, Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi ya Jamhuri ya Muungano.

5.   Rais wa Jamhuri ya Muungano atachaguliwa na Wajumbe wote wa Bunge la Muungano, Bunge la Tanganyika, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wenyeviti, mameya na magavana wote. 

 6. Rais wa Jamhuri ya Muungano atachaguliwa kwa kipindi kimoja cha miaka mitano na anaweza kuchaguliwa kwa kipindi kingine kimoja cha miaka mitano, na atachaguliwa kwa msingi wa kuachiana zamu ya kushikilia madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano Kati ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano.