To Chat with me click here

Monday, October 1, 2012

UCHAGUZI CCM BALAA

NAGU AFANYA KWELI, MFUTAKAMBA CHALI

HATIMAYE kinyang'anyilo cha kumpata Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Wilaya ya Hanang’, mkoani Manyara, kimemalizika juzi baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dkt. Mary Nagu, kuibuka mshindi.

Katika uchaguzi huo, Dkt. Nagu alipata kura 648 wakati mpinzani wake Waziri Mkuu mstaafu Bw. Frederick Sumaye alipata kura 481 kati ya kura 1129, zilizopigwa ambapo kura 41 ziliharibika.

Uchaguzi huo ambao ulikuwa na mchuano mkali, ulisimamiwa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa mkaoni hapa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa Bw. Elaston Mbwilo.

Nafasi nyingine iliyogombewa ni Mwenyekiti wa (CCM) wilayani hapa ambayo ilikuwa na wagombea watatu, Bw. Michael Bayo aliibuka mshindi na kuwashinda wenzake watatu.

Wagombea wengine walikuwa Bw. Hassan Hilbagroy na Bw. Goma Gwaltu, ambaye alikuwa akitetea nafasi yake ambapo Bw. Bayo alipata kura 647 na Bw. Hilbagroy (291).

Bw. Mbwilo pia alimtangaza Bi. Christina Mndeme (Mkuu wa Wilaya ya Hanang'), Bw. Anju Mang’ola, Mateo Darema na Bi. Hawa Hussen, kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Halmashauri Kuu.

Awali mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Mkutano Mkuu, Leonsi Marmo, alimwomba Bw. Mbwilo aondoe jina lake kwa sababu wagombea wenzake ni vigogo hivyo asingeweza kushinda.

Nchimbi aibuka kidedea
Katika Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma, Mbunge wa Songea Mjini ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, aliibuka mshindi katika nafasi ya ujumbe wa NEC baada ya kupata kura 722 kati ya 889 zilizopigwa.

Nafasi ya Mwenyekiti wa CCM wilayani Songea mjini ilichukuliwa na Bw. Gerad Muhenga kwa kura 540 kati ya 838 zilizopigwa. Wagombea wengine walikuwa Bw. Gorden Sanga (251) na Bi. Elizabethi Ngongi (37).

Wilaya ya Songea vijijini, Bw. Nelly Duwe alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM kwa 550 ambapo Bw. Ditram Tindwa (273), Bw. Nasri Nyoni (69).

Nafasi ya mjumbe wa NEC ilichukuliwa na Mwanasheria wa CCM Kutoka Makao Makuu mjini Dodoma, Glorius Luoga (649), ambapo Bw. Athanas Nyimbi alipata kura 205 na Bw. Peter Lwena (102).

Wagombea 16 waliwania ujumbe wa Mkutano Mkuu Taifa ambapo wajumbe watano walioshinda ni Bw. Joseph Muhagama (542), Vastus Mfikwa (423), Athon Kantala (383), Bi. Celina Kayombo (339) na Bw. Rajab Mtiula (320).

Ujumbe wa NEC Kihaba
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Wilaya ya Kibaha Mjini, mkoani Pwani, Bw. Rugemalira Rutatina, aliibuka mshindi wa nafasi ya ujumbe wa NEC baada ya kupata kura 547 kati ya 681, zilizopigwa na kuwashinda Bw. Rashid Bagdela (23) na Fratern Kiwango (11).

Wajumbe watano ambao walichaguliwa kuwakilisha Mkutano Mkuu Taifa ni Bi. Catherine Katele, Bw. Joseph Chale, Bw. Jumanne Mangala, Bw. Mohammed Mpaki na Fratern Kiwango.

Nafasi mbili za ujumbe Mkutano Mkuu CCM Mkoa  ni Bi. Hawa Kadibo na Bw. Said Mkuti. Nafasi ya Halmashauri Kuu Wilaya kupitia UVCCM, waliochaguliwa bila kupingwa ni Bi. Mwamvua Mwinyi, Bw. Joseph Chale, Bw. Simba Mohammed na Bi. Sophia Mlao ambapo Bw. David Mramba na Bw. Yusuph Mbonde, walichaguliwa kupitia wazazi.

Wajumbe wa Halmashauri Kuu kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Bi. Fatuma Silingo, Bi. Gertruda Mtiga, Bi. Hawa Kadibo na Bi. Joyce Shauri ambapo nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Kibaha Vijijini ilikwenda kwa Bw. Hamis Kanesa.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Bw. Mwinshehe Mlao, alisema viongozi na wanachama wanapaswa kuacha tabia ya ushabiki na makundi yasiyo na tija.

Wilaya ya Uyui
Katika Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora, aliyekuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Bw. Athuman Mfutakamba, ameshindwa kufurukuta mbele ya Ofisa Mtendaji Kata. Bw. Beatus Mlolua.

Bw. Mlolua alishinda ujumbe wa NEC baada ya kupata kura 706 dhidi ya 231 za Bw. Mfutakamba.

Dalili za kushindwa Bw. Mfutakamba zilianza kujionesha mapema wakati akijieleza na kuomba kura ambapo swali aliloulizwa na mmoja wa wajumbe lilimfanya ahamaki.

Muulizwa swali alimtaka Bw. Mfutakamba aeleze kwanini anawania nafasi ujumbe wa NEC, wakati Rais Jakaya Kikwete, alimtosa katika nafasi yake ya Unaibu Waziri.

Akijibu swali hilo, Bw. Mfutakamba alisema, “Aliyeniponza ni waziri wangu (Dkt. Omary Nundu) Rais Kikwete alinionea, kwani mimi ni mchapakazi hodari”.

Nafasi ya Mwenyekiti wa CCM wilayani hapa, aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Bw. Abdallah Kazwika, ameangushwa baada ya kupata kura 544, wakati Bw. Mussa Ntimizi alipata kura 769.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wilayani humo ni Bw. Joseph Kidaha, Bi. Anifa Kitwana Kondo, Bw. James January, Bw. David Malecela na Msafiri Abdurahaman.

Katika Wilaya Mpya Kaliua, Profesa Juma Kampuya alishinda nafasi ya ujumbe wa NEC wakati katika Wilaya ya Tabora, Bi. Margareth Sitta, akipita bila kupigwa.

Kivumbi Dodoma
Nafasi ya ujumbe wa NEC Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma ilichukuliwa na Bw. Malecela Samwel John, kwa kupata kura 727.

Bw. John aliwashinda Kusaja Jeremia (33), Mlugu Nassoro (209), Shamsi Hosea (333) wakati Habel Ngoli aliamua kujitoa.

Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa CCM mkoani hapa, Bw. Albert Mgumba, alisema katika Wilaya ya Kongwa, Bw. Mussa Abdi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti CCM kwa kura 836 na kuwashinda Mbijima Tagwe (44) na Simango Filemond (327).

Ujumbe wa NEC Wilaya ya Kongwa, mshindi ni Bw. Godwin Mkanwa (738), ambaye aliwashinda Bw. Mathias Kanyata (117), na Amon Anderson (334).

Katika Wilaya ya Chamwino, nafasi ya Mwenyekiti wa Wilaya alichukuliwa na Ulanga Benjamini (776), aliyewashinda Kusaja Jeremia (54) na Mtweli Malile (58)

Wilaya ya Mpwapwa Bw. John Chigwile alipata kura 794 na kuwashinda Honorati Pima (285) Bw. Said Mguto (255).

Nafasi ya NEC Mpwapwa, mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Bw. George Lubeleje alipata kura (911) na kuwashinda Bi. Rehema Halala (155) na Clavery Peter (279).

Katika Wilaya ya Chemba, kulikuwa na mgombea moja wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM, Alhaji Issa Mlalo, ambaye alipata kura 867 za ndio na 11 zilimkataa.

NEC Wilaya ya Chemba, Bw.  Juma Nkamia alipata kura 602  na kuwashinda Bw. Saidi Sambara (110) na Bw. Fredrick Duma (121). ambapo katika Wilaya ya Kondoa, kura zilipigwa mara mbili.

1 comment:

  1. This comment has been removed by a blog administrator.

    ReplyDelete