To Chat with me click here

Monday, November 5, 2012

SUDAN KUSINI YAMFURUSHA AFISAA WA UN


Sudan Kusini imemfukuza afisaa mmoja wa Umoja wa Mataifa aliyekuwa anachunguza hali ya haki za binadamu. Msemaji wa serikali anasema kuwa afisaa huyo alichapisha ripoti ya uchunguzi wake ambayo haikuwa na ukweli Maafisa wa umoja wa mataifa wamekosoa hatua hiyo wakisema kuwa ilikiuka majukumu ya nchi hiyo ya kisheria.

Kufukuzwa kwa afisaa huyo, walisema kunaweza kuhusishwa na ripoti iliyochapishwa mwezi Agosti na ambayo ilishutumu jeshi kwa kutesa, kufanya ubakaji , mauaji na utekaji nyara. Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wametoa madai sawa na hayo dhidi ya nchi hiyo ambayo ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Sudan mwezi Julai mwaka jana.

Mchunguzi huyo wa umoja wa mataifa, alitajwa na maafisa wa umoja wa mataifa kama Sandra Beidas. Msemaji wa serikali Barnaba Marial Benjamin alisema kuwa afisaa huyo aliripoti madai ambayo hangeweza hata kuthibitisha na amekuwa akizichapisha ripoti zake bila sababu.

"Hili ni jambo linalokiuka maadili’’ alisema bwana Marial bila kufafanua zaidi.
Hilde Johnson, mkuu wa ujumbe wa vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini Sudan, aliitaja hatua hiyo ya kufurushwa kwa mjumbe huyo kama kuhujumu sheria ya serikali chini ya makubaliano ya umoja wa mataifa.

Alisema kuwa alitaka serikali kutoa maelezo kuhusu hatua hiyo.

"Kuchunguza hali ya haki za binadamu na kuripoti na vile vile kuwezesha mashirika ni mojawapo ya majukumu ya jeshi la UNMISS ambalo linapaswa kulindwa ," alisema afisaa huyo.

Mwezi jana shirika la, Amnesty International lilichapisha ripoti iliyotuhumu wanajeshi wa serikali kwa kufanya vitendo vya kushangaza vya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo mauaji na ubakaji. Serikali ilijibu kwa kupuuza visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu akisema vilikuwa visa ambavyo havikutarajiwa.

No comments:

Post a Comment