To Chat with me click here

Monday, October 1, 2012

MANISPAA YA ILALA YASHINDWA KUFIKIA LENGO

KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Dk. Severine Assenga, amesema manispaa yake imeshindwa kufikia lengo la kukusanya Sh bilioni 26 kutoka katika vyanzo vyake vya mapato kwa mwaka wa fedha wa 2011/12.

Assenga alitoa taarifa hiyo juzi jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kikao cha kupitisha bajeti ya matumizi ya mwaka wa fedha uliomalizika Juni 30, mwaka huu kwa ajili ya ukaguzi utakaofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.

Alisema manispaa yake imeshindwa kufikia kiwango hicho kutokana na sababu mbalimbali na kusema kuwa hata hivyo imefanikiwa kukusanya Sh bilioni 17 pekee, ambazo ni sawa na asilimia 70 ya mapato yote.

“Tumeshindwa kufikia malengo kutokana na kuwepo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ukusanyaji mbaya wa mapatao ya leseni za biashara ambao Serikali kuu haijaruhusu kukusanya,” alisema.

Aliongeza kuwa sababu nyingine ya kushindwa kufikia malengo ni kuwapo kwa matumizi makubwa ambapo fedha nyingi hutumika katika maendeleo kama ujenzi wa vituo vya afya, shule na ulipaji wa mishahara ya watumishi.

Assenga alibainisha kuwa uwezo wa manispaa hiyo wa kulipa madeni yake si wa kuridhisha na pia uzalishaji wa madeni mapya umekuwa ukikua kwa kasi kubwa na kusema kuwa manispaa inahitaji kuchukua hatua za makusudi ili kukabiliana na hali hiyo.

"Mapendekezo yetu ni kupunguza matumizi na kutenga kiasi cha kutosha kwenye bajeti kila mwaka ili kulipa madeni yanayotukabili. Halmashauri yetu inatakiwa kuweka mikakati endelevu ya kudumu ili kuweza kuinua mapato ya ndani kwa kiwango kikubwa,” alisema.

No comments:

Post a Comment