To Chat with me click here

Monday, October 1, 2012

MWASISI WA NCCR-MAGEUZI AFARIKI DUNIA

Mwasisi wa NCCR, Ndg. Emmanuel Ole Sirikwa
MWASISI wa Chama cha NCCR- Mageuzi, Emmanuel Ole Sirikwa (70) amefariki dunia katika Hospitali ya AICC, iliyopo mkoani Arusha. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Mussa Kombo Mussa, alisema Ole Sirikwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kupooza (stroke), hadi alipofariki Septemba 28, mwaka huu hospitalini hapo.

Alisema hadi mauti yanamkuta, marehemu Ole Sirikwa alikuwa kamishna wa NCCR Mageuzi Mkoa wa Arusha, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na mmoja wa wajumbe wa Baraza la Wadhamini wa chama hicho.

“Marehemu Ole Sirikwa alikuwa mwasisi wa chama aliyekuwa na kadi namba 3 ya NCCR-Mageuzi, akitanguliwa na wenye kadi namba 1 na 2 ambao wamekisaliti chama na kuhamia kwingine kutokana na misukosuko ya kijamii.

“Chama kimempoteza mtu muhimu ambaye hakuyumba na aliendelea kubaki ndani ya chama chake, hali iliyotufanya baadhi yetu kumuona kama mzee wa boma la chama,” alisema Musa na kuongeza:

“Marehemu Ole Sirikwa alibaki ndani ya chama kwa sababu ya kuheshimu na kuthamini kile alichokianzisha, huku akiamini lengo na madhumuni yake bado hayajafikiwa, sisi tuliobaki tutaendeleza na kuyasimamia mazuri yote ili kufikia lengo alilokusudia,” alisema.

Mussa alisema kutokana na umuhimu wa marehemu Ole Sirikwa, chama kimeamua kuenzi uvumilivu na misimamo yake kwa kuuita ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu jina la Ukumbi wa Sirikwa.

Alisema mazishi yanatarajiwa kufanyika Oktoba 3, 2012 kijijini kwake Olijilah, Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, yakiongozwa na Mwenyekiti chama hicho taifa, James Mbatia.

Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi, Faustine Sungura, alisema kitendo cha vyama vingine kuzindua kaulimbiu na kuzifanyia kampeni nchi nzima ni dalili za kuanza kupata hofu ya uchaguzi ujao.

Sungura alisema NCCR Mageuzi imejipanga kujibu kwa vitendo kwa kuibuka na ushindi wa wabunge mwaka 2015, licha ya kutofanya operesheni wakati huu.

“Sisi NCCR Mageuzi tumejipanga na mipango yetu ipo ndani ya chama, tunafanya kampeni zetu kisiri, hatuhitaji maandamano na mziki mkubwa kwenye gari, tunataraji kuwa na mavuno mazuri kuanzia 2014 hadi 2015,” alisema.

No comments:

Post a Comment