WAKATAA
KULIPA HASARA YA MGOMO
CHAMA
cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema hakipo tayari kulipa gharama ya hasara za
uharibifu wa mali zilizotokana na mgomo wa walimu, kwa vile hakuna ushahidi wa
moja kwa moja kuwa wao ndio waliohusika na uhalifu huo.
Tamko
hilo linakuja ikiwa ni siku chache tangu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi, Dk. Shukuru Kawambwa, kulieleza Bunge kuwa CWT kama waratibu wa mgomo
huo, wanapaswa kulipa fidia za uharibifu wa jengo na ofisi ya Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Mji wa Tunduma na mali nyingine.
Akizungumza
na waandishi wa habari juzi mjini Tunduma baada ya kujionea uharibifu wa ofisi
hiyo iliyovamiwa na wanafunzi Julai 30 wakidai haki ya kufundishwa, Kaimu
Katibu wa CWT, Ezekiah Oluoch, alisema kama kuna walimu walihusika moja kwa
moja, serikali iwachukulie hatua.
“Ninachoweza
kusema kwa niaba ya CWT ni kutoa pole kwa uongozi wa mamlaka kwa kuvunjiwa
ofisi na kuibiwa samani na kikundi cha wahuni, na tunalaani tukio lililotokea,
lakini kwa sababu ofisi za CWT na mamlaka ni majirani wema, tutakapopata
tathmini ya uharibifu huo tutatoa kifuta machozi ila si fidia ya ujumla,
vinginevyo serikali itupeleke mahakamani,” alisema Oluoch.
Aliongeza
kuwa, serikali haikitendei haki chama chao kwa kuwahusisha viongozi wake kuwa
wanafadhiliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa ajili ya
kuvuruga amani ya nchi, na kwamba ikithibitisha suala hilo, yeye atakuwa wa
kwanza kujiuzulu wadhifa wake na kurudi kufundisha.
Kuhusu
sensa ya watu na makazi itakayofanyika hivi karibuni na kuwashirikisha walimu,
Oluoch alisema kuwa hawapo tayari kuwatetea walimu walioenguliwa majina yao
katika mchakato huo wa kusimamia sensa, na hivyo akawaonya kujiepusha na vurugu
zinazoweza kukwamisha.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mji wa Tunduma, Aidan Mwasiga, alisema kuwa
uharibifu uliotokea siku ya mgomo wa walimu, CWT hawawezi kukwepa lawama kuwa
chanzo, na kwamba suala hilo halihusiani na siasa.
Alizitaja
baadhi ya athari zilizopatikana bada ya ofisi yake kuvunjwa kuwa ni pamoja na
mji huo kukosa ushuru kutokana na nyaraka zote za kiserikali kuibwa, vikiwemo
vitabu vya kukusanyia mapato.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment