KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa,
ameibua tuhuma nzito dhidi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), akidai kimeingiza
silaha nchini bila ya vibali ili zitumiwe na vijana wao kukabiliana na
wapinzani.
Dk.
Slaa alisema kuwa wanazo nyaraka zinazoonesha namna CCM walivyoingiza silaha
hizo nchini kwa ajili ya kuwapatia vijana wao waliowekwa kwenye makambi maalumu
wakipatiwa mafunzo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana mjini Morogoro, kuelezea tathmini ya Operesheni
Sangara, maarufu kama Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) inayoendelea mkoani humo,
Dk. Slaa alisema mbinu hizo zimekuwa zikitumiwa muda mrefu na viongozi wa CCM.
Alitolea
mfano kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, aliyoitoa wakati wa uchaguzi
mdogo jimboni Igunga akidai kuwa CHADEMA imeingiza askari wenye mafunzo maalumu
nchini.
“Nilikuwa
ninajiuliza hawa CCM wana ujasiri gani wa kusema uongo kwa vyama vingine juu ya
kuingiza silaha, sasa nimejua dhamira yao baada ya kupata nyaraka zinazoonesha
mpango mkakati wao wenye lengo la kuwatumia vijana walio katika makambi yao kwa
ajili ya kufanya vurugu kwa kutumia silaha wanazowapatia,” alisema.
Aliongeza
kuwa kudhihirisha CCM hawatanii katika kutaka kufanya vurugu, msafara wa
CHADEMA mkoani humo umekuwa ukiandamwa na watu tofauti kwa kutumia magari
tofauti.
Dk.
Slaa alibainisha kuwa juzi wakiwa wanatoka katika Jimbo la Gairo, gari lenye
namba za usajili T 886 AVS aina ya Prado lilikuwa likiwafuatilia hadi wilayani
Mvomero na taarifa hizo walizitoa kwa askari waliokuwa wakilinda mikutano yao
katika Wilaya ya Mvomero.
“Juzi
walifanya hivyo tukiwa Mvomero, tukatoa tarifa polisi na leo asubuhi tumepata
taarifa ambazo hatuwezi kuzipuuza kuwa kuna vijana kati ya 10-20 wakiwa na
sumu, sindano na visu wanawawinda watu walio katika operesheni kwa ajili ya
kuwadhuru na nimewaagiza vijana wangu wa idara ya usalama wakatoe taarifa
polisi,” alisema Dk. Slaa.
Hata
hivyo, wakati Dk. Slaa akisema taarifa za msafara wao kufuatiliwa wakiwa wanatoka
Gairo kuelekea Mvomero, waliziwasilisha polisi ili zifanyiwe kazi, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alisema hana taarifa hizo.
Nape akanusha
Katibu
wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa wa CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alikanusha
tuhuma za Dk. Slaa, akidai kuwa mwanasiasa huyo anazeeka vibaya na kwamba ni
bora akawaachia vijana siasa.
“Maneno
haya hayapaswi kusemwa na mtu kama Dk. Slaa lakini nikwambie kuwa CCM haina
makambi hayo anayoyasema, naomba Watanzania wampuuze,” alisema.
Nape
aliongeza kuwa CCM haijawahi kuwaza kuwa na mawazo ya kutumia silaha na
haitakuwa nayo kama alivyodai Dk. Slaa, akibainisha kuwa hata wakati wa kudai
uhuru silaha hizo hazikutumika.
Alisema
kuwa anachokiona ni kwamba CHADEMA inasambaratika na hivyo inaanza kutafuta
sababu za uongo, huku akikumbushia madai aliyoyatoa Dk. Slaa mwaka juzi wakati
wa Uchaguzi Mkuu kuhusu wizi wa kura.
“Utakumbuka
mwaka 2010 wakati wa Uchaguzi Mkuu, Dk. Slaa alisema kuna kontena lina kura
mkoani Mbeya, lakini hadi leo hajawahi kuthibitisha uongo wake,” alisema Nape.
Pinda abanwa
Katika
hatua nyingine, Dk. Slaa amemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuweka hadharani
michango iliyokusanywa kwa ajili ya waathirika wa matukio ya mabomu ya Gongo la
Mboto na Mbagala; na mafuriko ya Kilosa na Dar es Salaam.
Dk.
Slaa alisema waziri mkuu anapaswa kutoa maelezo ya kina ndani ya siku 30 ili
Watanzania wajue michango waliyochanga kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zao ni
kiasi gani na imetumikaje.
Alisema
baada ya waziri mkuu kutoa hesabu ya vitu vilivyokusanywa pia anapaswa
kumuagiza Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuvifanyia ukaguzi ili kujua
namna vilivyotumika na kwamba kama hilo litashindikana, wabunge wa CHADEMA
watakuwa na wajibu wa kuandaa hoja binafsi na kuiwasilisha bungeni.
“Tumeshuhudia
namna waathirika wa mafuriko ya Kilosa walivyochangiwa na Watanzania kutoka
sehemu tofauti ya nchi, sasa leo wamefikia kulazwa chini chumba kimoja kwa
familia nzima pasipo kujali umri wala jinsia na mbaya zaidi, vyoo
wanavyotumia havina milango, huku ni kufedhehesha utu wa Mtanzania,” alisema.
Wavuna wanachama 31,337
Wakati
huo huo, Mkuu wa Operesheni Sangara wa CHADEMA katika mikoa mitano ya Morogoro,
Singida, Manyara, Dodoma na Iringa, Benson Kigaila, alisema baada ya
kupita katika majimbo sita ya mkoani Morogoro wamefanikiwa kuvuna wanachama
31,337.
Kigaila
alisema wanachama hao ni baada ya CHADEMA kufika katika kata 137 na vijijji 471
kwenye majimbo sita ya mkoa huo. Kwamba alipokea kadi 7,603 kutoka katika vyama
vingine.
Alisema
katika operesheni hiyo, wananchi walichangia kiasi cha sh 17,895,650, ndizi
mikungu 831, magimbi 73, mayai trei 17 na mchele kilo 148.
Kigaila alifafanua kuwa
kadi zilizouzwa ziliingiza kiasi cha sh 15,768,500.
No comments:
Post a Comment