KADA
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika tawi jipya la
Misongeni, mjini hapa (Morogoro), Emmanuel Constantine, amenusurika kifo baada
ya kushambuliwa na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa CCM.
Katika
tukio hilo lililotokea juzi saa 12 jioni, Emmanuel ambaye amefungua
jalada polisi Agosti 28, mwaka huu, aling’olewa meno mawili ya juu na kuumizwa
sehemu mbalimbali za mwili.
Vyanzo
vya habari hizi vilifika katika wodi namba moja ya Hospitali ya Rufaa mjini
hapa ambapo kada huyo amelazwa na kuelezwa na mashuhuda kuwa watu hao wakiwa na
fimbo na makopo ya rangi, waliing'oa bendera ya CHADEMA kwenye jiwe
lililozinduliwa juzi na kisha kulipaka rangi nyingine jiwe hilo.
“Ilipofika
saa 12 jioni wakatokea hao jamaa wa CCM wakiwa na fimbo na makopo ya
rangi, wakaing'oa bendera na kuitupa kisha wakaanza kupaka rangi walizokuwa
nazo, Emmanuel akawasogelea na kuwauliza kwanini wanafanya hivyo, ndipo
wakamgeukia na kuanza kumpiga,” alisema shahidi aliyejitambulisha kwa jina la
Innocent.
Mwenyekiti
wa CHADEMA mkoani hapa, Zuberi Kiloko, aliyefika eneo hilo baada ya kada huyo
kujeruhiwa, alisema kuwa alimkuta Emmanuel akiwa hajitambui na kulazimika
kukodi gari ili kumkimbiza hospitali.
“Ingawa
kulijitokeza usumbufu wa kupata PF3, tunashukuru kuwa hatimae
tuliipata na mgonjwa ametibiwa kwa kuwekwa nyaya mdomoni na kushonwa nyuzi sita
kwenye taya...ameruhusiwa kurudi nyumbani,” alifafanua.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alikana kuwa na taarifa hiyo,
huku akisema matukio kama hayo ni mengi sana hivyo hawezi kufahamu labda ni walevi waligombana
vilabuni.
No comments:
Post a Comment