ATISHIA KUJIUZULU,
SERIKALI YAFUNGA MJADALA, CHENGE SAFI
WAKATI
Rais Jakaya Kikwete akisema hakuna rushwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada
kutoka nchini Uingereza, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
wamemkalia kooni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard
Membe, wakimtaka awataje watuhumiwa na kashfa hiyo.
Wabunge
hao walitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa wakichangia hoja ya bajeti ya
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa na kwamba mbali na kutajwa kwa
watuhumiwa hao pia serikali iwachukulie hatua na si kufurahia tu chenji yake
ambayo imerejeshwa nchini hivi karibuni.
Mbunge
wa Viti Maalum, Rachel Mashishanga (Chadema), alisema kuwa Waziri Membe alipata
kueleza anawafahamu watuhumiwa na kashfa hiyo ni vema akawataja, ili jamii
iwatambue.
Naye
mbunge wa Gando, Khalifa Khalifa (CUF), mbali ya kumtaka Waziri Membe kuyataja
majina ya watu waliohusika katika kashfa hiyo, kwani kitendo cha kutoyataja
kinaashiria kuwa naye anahusika.
“Mheshimiwa
Waziri utakapokuwa unahitimisha hoja yako wataje hao waliohusika katika kashfa
ya rada…usifurahie chenji ya rada, kwani huo ni udhalilishaji mkubwa kwa
serikali yetu.”
Awali,
msemaji wa kambi ya upinzani wa wizara hiyo, Ezekia Wenje, alisema kambi hiyo
inaendelea kuhoji ni kwa nini mpaka sasa watuhumiwa wa kashfa hiyo wanaendelea
kutembea vifua mbele bila kuchukuliwa hatua zozote.
“Mpaka
sasa haieleweki ni kwa sababu gani nchi hii pamoja na kudai kuwa ina uhuru wa
kujiamulia mambo yake yenyewe iliamua kuliachia suala hili kufanyiwa kazi na
serikali ya Uingereza, kuanzia uchunguzi hadi mashtaka ya kurudishwa fedha
zilizotokana na rushwa ya rada ambayo sasa imebatizwa jina tamu ya chenji ya
rada,” alisema.
Wenje
ambaye pia ni waziri kivuli wa wizara hiyo, alisema pamoja na serikali
kushindwa kufanya uchunguzi na hatimaye kuwashtaki watuhumiwa wa rada,
ilipobainika kuwa inatakiwa kurudishwa chenji ya rada serikali ilikuwa mstari
wa mbele kufuatilia chenji hiyo na kuipangia matumizi.
“Tunashindwa
kuelewa umakini wa serikali uko wapi, kwamba inaweza kuweka msisitizo katika
kuhakikisha fedha za rushwa ya rada zinarudishwa nchini, lakini haiwezi
kuthubutu kushughulikia wale waliosababisha upotevu wa fedha hizo kwa njia ya
mkataba,” alisema.
Alibainisha
kuwa taarifa mbalimbali zinazotokana na utafiti wa suala hilo, zinaeleza namna
wizi huo ulivyofanyika ukiwahusisha Watanzania wengine wakiwa ni viongozi
mbalimbali waandamizi wa serikali ya CCM na kwamba Watanzania wanashangaa
watuhumiwa hao sasa wanachaguliwa kuongoza mhimili muhimu wa Bunge.
Serikali
yalazimisha kufunga mjadala
Akijibu
hoja za wabunge kuhusu kashfa hiyo ya rada, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias
Chikawe, alisema serikali imefunga mjadala kwani hakuna rushwa katika suala
hilo.
Alisema,
hata Uingereza iliyochunguza suala hilo imeeleza bayana kwamba hakuna rushwa na
katika hatua hiyo serikali haiwezi kumfikisha mahakamani mtu yeyote.
“Katika
hali kama hii tukimpeleka mtu mahakamani na ushahidi tunaoutegemea, ni upande
ule wa BAE na SFO maana huku hakuna mashahidi… sasa kule hata kumtaja mtu
hauruhusuwi na serikali hii iliingia mkataba na hawa, tukisema tunataka kumwita
mtu aje kutoa ushahidi huku hawatakubali,” alisema.
“Kwa
hiyo naomba jambo hili lifike mwisho hakuna rushwa katika rada ambayo inawahusu
Watanzania tunaowajua,” alisema.
Alieleza
kuwa kabla ya kuzungumza hayo aliwasiliana na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na
kumuuliza kama kuna kitu kipya na alimwambia hakuna anayehusika.
Alisema
kuwa alilieleza suala hilo Julai 5 mwaka jana na kudhani kuwa limekwisha, lakini
anaona bado linajirudia na kusema inaonekana jambo hilo halijaeleweka kwa
wananachi.
“…Jamani
hakuna kesi ya rada dhidi ya mtu yeyote hapa Tanzania kuhusu sakata la
rada…Niliomba kama kuna mtu ndani au nje mwenye ushaidi aulete, maneno maneno
mahakamani hakuna unatakiwa ushahidi unaojitegemea.
“Sasa
nikaambiwa kuna kitabu kimeandikwa na mimi nimekisoma na wale waliotajwa kama
ningekuwa mshauri wao ningewashauri wamfungulie mashtaka mwandishi wa kitabu
hicho maana msingi wa kitabu chake ni magazeti. Anasema fulani mwizi ananukuu
This Day, fulani mwizi ananukuu The Guardian.”
Wiki
iliyopita Rais Kikwete wakati akizungumza na waandishi wa habari, alisema
hakuna rushwa kwenye ununuzi wa rada na badala yake kulikuwa na makosa ya
uchapaji.
Ingawa
Rais Kikwete hakutaja jina, lakini kwa kauli hiyo ni dhahiri kwamba alimsafisha
Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM), ambaye kwa muda mrefu amekuwa
akitajwa ndani na nje ya chama chake kuhusika na kashfa hiyo kutoka Kampuni ya
BAE- System ya nchini Uingereza.
Chenge,
ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi,
anatajwa kuhusika kutoa ushauri wa kisheria wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, ushauri ambao unatajwa kuzingatiwa katika hatua za uamuzi.
Mwingine
anayehusishwa na kashfa hiyo, ni aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT) Dk. Idriss
Rashid.
Pamoja
na hao, wanatajwa wafanyabiashara wenye asili ya India, lakini ambao
wanaishi/walipata kuishi Tanzania, Tanil Somaiya, ambaye alikuwa akimiliki
kampuni ya uwakala wa simu ya Shivacom na Sailesh (Shailesh) Vithlani kuwa watu
wa kati wa biashara hiyo.
Mchakato
wa ununuzi wa rada, uliwahusisha watu wa madaraka na kada mbalimbali ambao ni
pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.
Blair
anatajwa kuwa ndiye aliyemshawishi aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo,
Benjamin Mkapa, kununua rada hiyo kutoka kampuni ya kutengeneza silaha ya
Uingereza BAE-Systems. Wakati huo aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa,
Clare Short, alikataa katakata Tanzania, moja kati ya nchi maskini kabisa
duniani, kutumia sh bilioni 40 kununua rada katikati ya umaskini unaonuka.
Waziri
Membe atishia kujiuzulu
Katika
hatua nyingine, Membe ametishia kujiuzulu iwapo atajitokeza mtu atakayeweza
kuendesha wizara hiyo kwa bajeti ya asilimia 42.
Akijibu
hoja mbalimbali za wabunge waliochangia hoja yake, Waziri Membe alisema wizara
hiyo inapata mgao kidogo wa bajeti isiyokidhi mahitaji na katika mwaka wa fedha
ulioisha wizara hiyo ilipata asilimia 44 ya bajeti iliyoombwa.
“Kama
atajitokeza mtu anayeweza kuendesha wizara hii kwa bajeti ya asilimia 42
nitakuwa tayari kujiuzulu, kwani wizara hii imekuwa ikipata mgao kidogo wa
bajeti, hivyo tuna changamoto nyingi,” alisema.
Alisema
pamoja na mapungufu hayo, wizara hiyo ambayo ni kiungo muhimu cha nchi yetu na
nchi za nje imeendelea kushirikiana kwa karibu na wizara, idara na taasisi
mbalimbali za serikali na sekta binafsi kuhakikisha nchi inafaidika kwa kadri
iwezekanavyo na fursa mbalimbali zenye manufaa kwa nchi.
Alitoa
mfano kuwa wizara hiyo imeshirikiana na ubalozi wa China na Wizara ya Nishati
na Madini pamoja na Wizara ya Fedha kuhakikisha nchi inapata dola bilioni 1.2
kwa ajili ya ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar
es Salaam.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment