Nimefuatilia
Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) na kujulishwa kuwa hatua zimeanza
kuchukuliwa kuhusu matatizo ya maji yanayoendelea katika maeneo mengi ya kata
za Mbezi Luis na Msigani kwa takribani wiki tatu kufuatia ratiba ya mgawo wa
maji kuathiriwa na kuhamishwa kwa huduma ya maji kutoka katika bomba la maji la
inch 24 mpaka la inch 30. Hali hiyo imeathiri zaidi maeneo ya Magari Saba,
Kibanda cha Mkaa, Kwa Msuguri, Temboni na maeneo mengineyo.
Aidha,
kuhusu maghati ya umma na maeneo ya pembezoni ambayo yalikuwa na matatizo
makubwa ya maji kabla hata ya kipindi husika ikiwemo maeneo ya Bwaloni na
Msingwa, nimeiandikia barua Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA)
kuwaalika kufanya nao ziara ya kikazi mapema iwezekanavyo katika maeneo husika
kwa ajili ya kutoa maelezo ya kiutendaji kuhusu hali iliyopo na kueleza mipango
inayopaswa kutekelezwa ya kupata ufumbuzi wa haraka.
Natoa
taarifa hii kwa kuzingatia kuwa tarehe 25 Agosti 2012 nilipokutana na wananchi
katika eneo la Mbezi kwa Msuguri wakati nikiwa katika kazi ya kuhamasisha
wananchi kushiriki katika sensa, kujiandaa kutoa maoni ya katiba mpya na kupata
mapendekezo yao kuhusu masuala ya kuyapa kipaumbele baada ya kurejea kutoka
katika mkutano wa nane wa Bunge nilielezwa kuhusu matatizo ya maji katika
maeneo tajwa.
Kufuatia
maswali yaliyoulizwa na masuala yaliyoelezwa nilitoa majibu ya ujumla kwamba:
Mosi, kuhusu matatizo yaliyojitokeza nilieleza kuwa chanzo chake ni marekebisho
yaliyokuwa yakiendelea ya kuondoa baadhi ya watu waliokuwa wamejiunganisha maji
kinyemela katika mabomba makuu pia kuhamisha huduma kwa wananchi wa maeneo
tajwa kutoka bomba la inch 24 mpaka la inch 30, hata hivyo kwa kuwa matatizo
hayo yameendelea niliahidi kuwasiliana na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka
(DAWASCO) na kutoa majibu ya hatua za kuharakisha huduma ya maji kurejea katika
hali ya kawaida.
Pili,
kuhusu maeneo ambayo yalikuwa hayatoki maji hata kabla ya wiki tatu ikiwemo
baadhi ya maghati ya umma na maeneo ya pembezoni nilieleza chanzo cha hali hiyo
kwa kadiri ya majibu niliyoelezwa na DAWASCO nilipofanya nao ziara katika kata
ya Msigani tarehe 1 Machi 2012 na kwa kuwa matatizo katika maeneo hayo
yanahitaji hatua kubwa zaidi niliahidi kwamba nitawaalika Watendaji wa Mamlaka
ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) ili kufanya nao ziara ya kikazi karibuni
kuweza kutafuta ufumbuzi.
Izingatiwe
kwamba kazi ya mbunge ni kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali na vyombo
vyake kuwezesha maendeleo, na katika muktadha huo Machi Mosi 2012 niliungana
pamoja na DAWASCO kwenye kata za Sinza, Makurumla, Mburahati, Msigani,
Mabibo, Saranga, Kwembe na Makuburi kufuatilia kazi za kuboresha upatikanaji wa
maji katika Jimbo la Ubungo.
Kupitia
ushirikiano huo tuliona bayana kwamba mtandao wa biashara haramu ya maji
unaohusisha kujiunganisha mabomba ya maji kinyemela nao unachangia katika
matatizo ya maji katika baadhi ya maeneo, mathalani tuliona mota za biashara
hizo katika maeneo ya kata ya Makurumla hususani mtaa wa Kagera, Makuburi
kwenye nyumba yenye matanki yaliyounganishwa chini chini kwa ajili ya biashara
ya maji na Kata ya Saranga eneo la Kimara B ambapo mtandao wa maji ulitolewa
toka kwenye maeneo ya wananchi na kupelekwa nje ya makazi ya watu kwenye
mtandao wa wafanyabiashara wakubwa wa maji. Mitandao hiyo ilianza kukatwa na
majalada yalifunguliwa polisi kwa ajili ya wahusika kuchukuliwa hatua za
kijinai.
Hali
hiyo ilishamiri kutokana pia na vishoka na tulikubaliana kwamba kuanzia wakati
huo yoyote anayekwenda kugusa bomba la DAWASA lazima kwamba aripoti kwenye
serikali za mitaa na pia popote anapofanya kazi hizo lazima awe na kitambulisho
cha DAWASCO na pia kadi ya kazi (job card) yenye saini ya meneja wa eneo ya
kueleza aina ya kazi na ruhusa iliyotolewa kuifanya. Nachukua fursa hii
kuwakumbusha wananchi kuchukua hatua dhidi ya yoyote anayekwenda kinyume na
makubaliano hayo kama ilivyo kwa wahalifu wengine wanaokiuka sheria.
Katika
kazi tulizofanya Machi Mosi 2012, ilionekana bayana kwamba bado yapo maeneo
ambayo mtandao wa mabomba ya wachina hautoi maji kutokana na msukumo mdogo na
matatizo ya mfumo mzima, kama ilivyo katika majimbo yote ya Dar es salaam, Kwa
upande wa Jimbo la Ubungo hali hii imeathiri maeneo ya Malambamawili, kwa
Msuguri, Makoka na mengine. Aidha, yapo maeneo ambayo hayakufikiwa kabisa
kwenye awamu ya kwanza ya utandazaji wa mabomba husika mathalani ya Msingwa,
Mbezi Msumi na mengineyo katika jiji la Dar es salaam.
Haya
ni masuala yanayohusu mwenye mali na miundombinu ambaye ni Serikali kupitia Wizara
ya Maji na DAWASA, zaidi ya DAWASCO ambayo pamoja na kuwa nalo ni shirika la
umma ni mwendeshaji tu. (Maji DSM ni kama duka, kuna mwenye bidhaa ambaye
anawajibika kujaza duka lake ili wateja wasikose-DAWASA na muuza duka ambaye
ana kazi ya kuuza duka lenye bidhaa chache-DAWASCO malalamiko mengi ya wateja
yanamuangikia yeye).
Kufuatia
hali hiyo niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge hoja Binafsi kwenye mkutano wa nane
wa Bunge uliomalizika kutaka bunge lipitishe maazimio ya hatua za haraka zaidi za
kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo
la Ubungo na Jiji la Dar es salaam; hata hivyo hoja hiyo haikupangiwa
kujadiliwa bungeni kutokana na ufinyu wa muda baada ya ratiba ya bunge
kufanyiwa marekebisho na kipengele cha hoja za wabunge kuondolewa. Kutokana na
hali hiyo, wakati nikisubiri mkutano tisa wa bunge unaofuata niendelee na kazi
zingine ikiwemo kuwaandikia DAWASA ili wafike jimboni Ubungo na kuchukua hatua
kwa masuala ya maendeleo yaliyo ndani ya uwezo wao.
Wenu
katika uwakilishi wa umma,
John
Mnyika (Mb)
27
Agosti 2012
No comments:
Post a Comment