Sasa ni sahihi kwamba Zenawi hayupo
tena duniani. Televisheni ya taifa ya Ethiopia imetangaza mapema leo kwamba
kiongozi huyo aliyekuwa na nguvu sana nchini humo, amefariki dunia mjini
Brussels, Ubelgiji, alikokuwa akitibiwa. Televisheni hiyo imesema Zenawi
amefariki dunia wakati akiwa anapata afuweni kutokana na maambukizi ya ghafla.
Tangazo la televisheni hilo limesema na
hapa ninanukuu: "Waziri Mkuu Zenawi amefariki ghafla usiku wa jana. Meles
alikuwa akipata afuweni katika hospitali moja ughaibuni kwa miezi miwili,
lakini alifariki kutokana na maambukizi ya ghafla saa 5 na dakika 40."
Mwisho wa kunukuu.
Uvumi kwamba kiongozi huyo wa zamani wa
vita vya msituni alikuwa akiumwa sana, ulianza kusambaa tangu aliposhindwa
kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa mwezi
uliopita. Tangu hapo wasiwasi ulikuwa umezuka juu ya nani hasa anaiongoza nchi hiyo,
baada ya Zenawi kuchukuwa likizo ya kutokuwapo kazini.
Serikali ilikanusha ugonjwa wa Zenawi
Siku ya Alhamis, msemaji wa serikali,
Bereket Semon, alirejelea kauli yake ya mara kwa mara akikanusha kuwa Zenawi
alikuwa mgonjwa sana. Serikali ilikuwa imesema kuwa Zenawi alilazimika kuchukua
likizo kwa ushauri wa daktari.
Kwa ujumla, ni shida kujuwa hasa
ugonjwa uliomaliza maisha ya kiongozi huyo ambaye amekuwa madarakani tangu
kumpindua Megistu Haile Mariam hapo mwaka 1991, lakini inaaminika kwamba
alikuwa akisumbuliwa na uvimbe kwenye ubongo.
Zenawi atakumbukwa kwa sera yake ya
kiutawala ambayo ilijuilikana kama shirikisho la makabila, akitoa mamlaka
fulani mwa mamlaka za mikoa zenye misingi ya kikabila, lakini akisalia na nguvu
kubwa kwenye serikali chini ya chama tawala. Nafasi ya uraisi inachukuliwa kama
heshima tu, na Zenawi ndiye hasa aliyekuwa na nguvu za kisiasa.
Naibu Waziri Mkuu Hailemariam achukua
madaraka
Kwa mujibu wa katiba ya Ethiopia, naibu
waziri mkuu ndiye anakuwa na wajibu wa kukaimu nafasi ya uwaziri mkuu, ikiwa
waziri mkuu hayupo. Hata hivyo, sheria haisemi wazi na mahsusi ikiwa naibu huya
wa waziri mkuu anachukuwa pia majukumu yote ya waziri mkuu.
Kwa kifo hiki cha Zenawi, kitu cha
mwanzo ambacho kinaweza kushuhudiwa haraka nchini Ethiopia, wanasema
wachambuzi, ni ombwe la kiuongozi, ikihofiwa kwamba hakuna yeyote katika watu
wake wa karibu aliyetayarishwa vyema kujaa kwenye kiti cha uwaziri mkuu.
Baadhi ya wanadiplomasia wamesema
kwamba hawana hakika ni nguvu kiasi ambazo Naibu Waziri Mkuu, Hailemariam
Desalegn, anazo hivi sasa. Hailemariam alikuwa nchini China hadi hivi karibuni
kabisa katika mkutano wa kilele na China. Taarifa za kibalozi na wachambuzi
zinaonesha kuwa bado hakujawa na vita vya kugombea madaraka ndani ya chama
tawala hadi sasa.
Source: DW
No comments:
Post a Comment