To Chat with me click here

Tuesday, August 21, 2012

WAKE WA MARAIS WA SADC WASAINI AZIMIO

MKE WA RAIS WA TANZANIA KUSHOTO MAMA SALMA KIKWETE NA KULIA MKE WA RAIS WA ZAMBIA DR. CHRISTINE KASEBA –SATA WAKIUFURAHIA AZIMIO LA MKATABA WA KUONDOA UKIMWI KATI YA MAMA KWENDA KWA MTOTO MKATABA ULIOFANYIKA MJINI MAPUTO MSUMBIJI JUZI
WAKE WA MARAIS WA KUSINI MWA AFRIKA WAKIWA KWENYE CHUMBA CHA MAJADILIANO ,KUTOKA KUSHOTO NI MKE WA RAIS WA MOZAMBIQUE DR.MARIA da LUIZ Dai GUEBUZA, WA PILI KUSHOTO MKE WA RAIS WA NAMIBIA PENEHUPIFO POHAMBA ,WA TATU KUSHOTO NI MKE WA RAIS WA ZAMBIA DR.CHRISTINE KASEBA –SATA,WA KWANZA KULIA NI MKE WA RAIS WA TANZANIA SALMA KIKWETE WAKISUBIRI KUSAINI AZIMIO LA MKATABA WA KUONDOA UKIMWI KUTOKA KWA MAMA KWENDA KWA MTOTO MJINI MAPUTO JUZI
KAMATI YA WAKE WA VIONGOZI WA WAKUU WA KUSINI MWA AFRIKA (SADC ) WAKIWA KWENYE PICHA YA PAMOJA BAADA YA MAPUMZIKO MJINI MAPUTO KABLA HAWAJASAINI AZIMIO YA MKATABA WA KUONDOA MAAMBUKIZO YA UKIMWI KUTOKA MAMA KWENDA KWA MTOTO

WAKE wa marais wa nchi za Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wamepitisha azimio la  kutokomeza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU)  kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Pamoja na azimio hilo, wamejipanga kuhakikisha wanapunguza vifo vya mama na watoto vinavyotokana na uzazi.

Azimio hilo lilisainiwa jijini Maputo, Msumbiji jana na wenza hao wa marais waliohudhuria mkutano wa  siku mbili wa kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni hitaji la awali kwa maendeleo ya kikanda ulioenda sawia na mkutano wa 32 wa SADC.

Akisoma Azimio hilo mbele ya waandishi wa habari, Katibu wa Kamati iliyoandaa azimio hilo, Daud Nasibu, alisema nia ya SADC ni kuimarisha biashara na uhusiano wa kikanda ambao matokeo yake ni kusafiri kwa watu na bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine.

Alisema jambo linalosababisha kupatikana kwa ajira na kupunguza umaskini huku kukiwa na changamoto ya maambukizi ya magonjwa ukiwemo ukimwi. Nasibu alisema wake hao watafanya kazi na wadau wa maendeleo na serikali zao ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo wakiamini inawezekana kwa kizazi kijacho kwenye nchi za SADC kuwa na watoto wasiokuwa na maambukizi ya ukimwi.

“Tutawahamasisha  wanawake  ili waweze kuhudhuria katika vituo vya afya  na kupata huduma za mama na mtoto ikiwemo kuzuia maambukizi ya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT)  kabla na baada ya kujifungua,” alisema Nasib aliposoma azimio hilo.

Kwa upande wake, mke wa Rais Jakaya Kikwete, Salma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kitu kikubwa ni kuhakikisha kwamba azimio walilolisaini likishapata baraka za wakuu wa nchi lianze kufanyiwa kazi ili kutimiza lengo la kutokomeza ukimwi kwa vizazi vyao.

Naye Rais wa Umoja wa Wake wa  Marais wa  Afrika wa Kupambana na Ukimwi (OAFLA), ambaye pia ni mke wa Rais wa Namibia,  Penehupifo Pohamba, aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo na kusema kazi iliyobaki ni kuhakikisha lengo linatimia.

Takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka 2011 zaidi ya watu milioni 34 wanaishi na maambukizi ya VVU kati ya hao milioni 30.7  ni watu wazima, milioni 16.7 wanawake  na milioni 3.4 ni watoto wenye umri chini ya miaka 15.

No comments:

Post a Comment