WAKATI
walimu wakikubali kurejea kazini na kuendelea kutafakari amri ya mahakama,
mkakati mzito unapangwa kuhakikisha hawakiungi mkono Chama cha Mapinduzi (CCM)
kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa tangu kutolewa kwa kauli ya Rais
Jakaya Kikwete kwamba mgomo huo si sahihi na serikali yake haina uwezo kutimiza
madai yao na kufuatiwa na uamuzi wa mahakama, walimu wamekuwa wakiangalia namna
nyingine ya kuibana serikali.
Mwishoni
mwa wiki, walimu katika wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, walikuwa na kikao
kizito ambapo pamoja na mambo mengine, walipendekeza kuiangusha CCM kwenye
uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Katika
mkutano huo ulioitishwa na uongozi wa Chama cha Walimu (CWT) na kufanyika
katika ukumbi wa Afro Berch mjini Nansio Ukerewe, baadhi ya walimu ambao
waliomba majina yao yahifadhiwe, waliwataka wenzao waungane kuing’oa CCM kwa
madai kuwa serikali inayoiongoza imeshindwa kusimamia maslai yao.
“Ndugu
zangu walimu, walimu tusitarajie kupata maslai bora kama CCM itaendelea kushika
dola. Hebu angalieni tangu tulipoanza mvutano na serikali chama hicho kimebaki
kimya huku kikitambua matatizo makubwa yanayotukabili. Tuungane tufanye maamuzi
magumu mwaka 2015,” alisema mwalimu huyo.
Huku
akiungwa mkono na walimu wengi, mwalimu huyo bila kumung’unya maneno, alisema
ingawa maadili ya utumishi wa umma yanazuia watumishi kushiliki siasa, lakini
muda umefika kwa walimu kutumia ushawishi wao kuhakikisha mwaka 2015, CCM
inang’oka madarakani.
Mwalimu
huyo alisema, walimu wakiamua kwa wingi wao wanaweza kwani ndio wanaotumika na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wakati wa uchaguzi.
Mwalimu
mwingine aliungana na mwenzake kuishambulia CCM kwamba inalinda kundi dogo la
wanasiasa wanaoneemeka na rasilimali za taifa huku Watanzania wengi
wakikabiliwa na umaskini.
Mwalimu
huyo pia aliushambulia mfumo wa mahakama kwamba hauko huru kwenye kutoa
maamuzi, akitolea mfano uamuzi wa kesi yao kuwa ulikuwa na mkono wa serikali.
Kwa
upande wake, Katibu wa CWT wilayani humo, John Kafimbi, alimlalamikia Rais
Kikwete kuzungumzia kesi yao huku akijua fika kwamba suala hilo liko
mahakamani.
Aliwataka
walimu wajipongeze kwani katika kipindi cha mgomo, wamedhihirisha kwamba
wakiamu wanaweza kupigania haki zao.
Jijini
Dar es Salaam, Chama cha Wananchi (CUF), kimesema Rais Kikwete ameudanganya
umma kwamba serikali inahitaji asilimia 75 ya bajeti yake kuboresha maslahi ya
walimu tu wakati kiasi hicho ni kwa ajili ya watumishi wote.
Mbali
ya hilo, CUF imeitaka serikali kuacha kutumia mahakama kuzima madai ya msingi
ya walimu bila kutafuta njia sahihi ya kutatua.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba,
alisema katika mazungumzo yake na wahariri wa vyombo vya habari yaliyofanyika
Ikulu jijini Da es Salaam Agosti mosi, Rais Kikwete alichukulia madai ya walimu
na kulinganisha na nyongeza ya wafanyakazi wote serikalini badala ya kuja na
tamko la kushughulikia matataizo ya walimu.
“Rais
anaposema tutatumia asilimia 75 ya bajeti kama tukitekeleza madai ya walimu
hawatendei haki Watanzania waliomsikiliza kwani alitumia takwimu za wafanyakazi
wote serikalini kama wataongezewa mishahara kwa kiwango hicho na kuyafanya
ndiyo madai ya walimu,” alisema Prof. Lipumba.
Alisema,
ingawa CUF haiamini kama migomo ya wafanyakazi ndio suluhu la matatizo,
inaamini walimu wana madai ya msingi na ya haki yanayopaswa kushughulikiwa na
kupewa kipaumbele. Mwenyekiti
huyo wa CUF alimshangaa Rais Kikwete kushindwa kueleza mikakati ya kutekeleza
madai ya walimu ili kuwanusuru na hali ngumu ya maisha.
“Serikali
isiyo na mipango kwa vyovyote vile haina uhalali wa kuwatumikia wakulima na
wafanyakazi, na hali hiyo inaitia aibu serikali inayoamua kuwahadaa walimu kwa
mambo yaliyo wazi,” alisema Prof. Lipumba.
Alisema
kuna fursa nyingi ambazo serikali ya CCM imeshindwa kuzitumia na kama
zingetumiwa ipasavyo, leo kusingekuwa na madai ya walimu wala wafanyakazi wa
kada nyingine.
“Kwa
kweli elimu ya Tanzania itaendelea kuwa duni ikiwa mchezo huu wa kuwapiga
danadana walimu utaendelea….vigogo wa CCM ambao watoto wao wanasoma katika
shule za kimataifa na za kimombo, katu hawawezi kuwafikiria watoto wa maskini
wasio na mbele wala nyuma,” alisema Prof. Lipumba.
Alibainisha
kuwa lazima walimu watambue CCM haiko madarakani kutatua matatizo yao, hivyo ni
vema wakaungana kuhakikisha chama hicho kinaondoka madarakani.
Hivi
karibuni Mahakama Kuu divisheni ya kazi ilisitisha mgomo wa walimu kwa madai
kuwa ni batili.
Mahakama
hiyo iliamuru pande zote zinazotofautiana kurudi katika meza ya majadiliano kwa
ajili ya kusaka suluhu.
Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment