KATIKA
kile kinachoonekana kama hofu ya kuuawa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk.
Steven Ulimboka, amefichwa kusikojulikana ikiwa ni siku moja baada ya kurejea
kutoka nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa matibabu.
Kufichwa
kwa Dk. Ulimboka kunadaiwa ni sababu za kiusalama ili kuwakwepa wabaya wake
waliodaiwa kumteka na kumpiga, ambao inaelezwa kuwa wamekuwa wakihaha kutaka
kukatisha uhai wake akiwa hospitali nchini Afrika Kusini bila mafanikio.
Dk.
Ulimboka aliyefikia nyumbani kwa baba yake, mzee Steven Mwaitenda eneo la
Ubungo Kibangu jijini Dar es Salaam baada ya kurejea nchini juzi alasiri,
amefichwa kusikojulikana huku baba yake mzazi akieleza kuwa wanajiandaa kutoa
tamko la familia.
“Kwa
sasa Dk. hayupo hapa nyumbani… siwezi kusema alipo wala kutoa tamko langu ila
muda ukifika tunamwandaa msemaji wa familia, vyombo vya habari mtajulishwa.
Ninawapenda sana wanangu, lakini katika hili naomba tusubiri,” alisema baba wa
Dk. Ulimboka aliyekutwa chini ya mti nje ya nyumba yake pembeni ya banda la
kuku wachache wa kienyeji jana.
Kabla
ya Tanzania Daima kuanza mazungumzo na baba huyo, ambaye awali alikuwa tayari
kuzungumza, dada wawili wa Dk. Ulimboka waliingilia kati wakidai mzee huyo si
msemaji wa familia.
Mmoja
wa dada zake Dk. Ulimboka, aliyejitambulisha kwa jina moja la Hidaya, aliwataka
waandishi wa gazeti hili kuondoka kwa sababu familia haijamteua msemaji wa
suala hilo, hivyo muda ukifika, litawekwa wazi kwa vyombo vya habari.
“Kwanza,
tutambuane nyie ni kina nani? Eee baba si msemaji wa familia… kwanza familia
haijamteua msemaji wake kila mtu akisema tunaweza kupishana maneno, muda
ukifika mtaambiwa tu.
“Hatuwezi
kusema alipo, hayo yote subirini mtaambiwa tukiwa tayari na hata yeye Dk.
mwenyewe anaweza kuzungumza, lakini si sasa,” alisisitiza Hidaya huku akionesha
hofu na kuwataka waandishi hao kuondoka.
Hata
gazeti hili lilipojaribu kutumia mbinu za kiuandishi ili kupata taarifa zaidi
juu ya Dk. huyo, baba huyo alisisitiza kuwa hana taarifa zozote zaidi ya
kuwasisitizia waandishi kuwa na subira.
Mzee
Mwaitenda, alisema kuwa hata hatua ya kuruhusu waandishi hao kuingia ndani ya
eneo la nyumba yake ilikuwa ni busara zaidi, la sivyo angeweza kuwarudishia nje
ya geti la nyumba hiyo.
“Niwe
mkweli, nimetumia busara tu kuwaacha muingie hadi ndani ya geti hilo …kwanza
siwafahamu na wala sijawahi kuwaona, ningeweza kuwarudisha pale,” alisema huku
akinyoosha kidole.
Mazingira
ya nyumbani
Nyumba
ya baba yake Dk. Ulimboka inatazamana na nyumba ya kulala wageni iitwayo
Samaria, eneo hilo la Kibangu ambayo imezungukwa na ukuta wa matofali ya
saruji.
Hata
hivyo, Tanzania Daima ilikuta mafundi wawili wakiendelea na kazi ya kuchomelea
geti jekundu la kuingilia ndani ya nyumba hiyo ambayo ndani yake kuna nyingine
mbili.
Juzi
Dk. Ulimboka alirejea kwa kishindo nchini kutoka Afrika Kusini alikokuwa
anatibiwa, na kusema yupo tayari kendeleza mapambano na kazi baada ya kupona
kabisa.
Dk.
Ulimboka alikwenda Afrika Kusini Juni 30 mwaka huu kwa ajili ya matibabu bora
zaidi baada ya kutekwa, kupigwa na kutelekezwa kwenye msitu wa Pande, nje
kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na watu wasiojulikana.
TUCTA
watoa neno
Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Nicholaus Mgaya, ameeleza
kufurahishwa na hatua ya kurejea salama kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari
nchini, Dk. Steven Ulimboka, akisema anaamini hataogopa kuendeleza
ujasiri wake katika kupigania haki za madaktari. Akizungumza na Tanzania Daima
kwa njia ya simu jana, Mgaya alisema akiwa kama kiongozi wa wafanyakazi,
anatambua ujasiri wa Dk. Ulimboka katika kutetea masilai hayo.
“Kama
Mtanzania, nimefurahi kwa sababu Ulimboka ni mtu msomi, ni daktari na sisi tuna
shida ya madaktari katika nchi hii, kwa hiyo namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjalia
afya njema akarejea salama. “Nikiwa kama kiongozi wa wafanyakazi na nikitambua
ujasiri wake katika kupigania haki za madaktari wenzie, nimeguswa sana na
kurudi kwake salama na katika afya nzuri, naamini hatakuwa mwoga bali
ataendelea na ujasiri aliokuwa nao tangu mwanzo kwa sababu haki siku zote haiji
kwenye sahani,” alisema Mgaya.
Mgaya
alisisitiza kwamba, anaamini Dk. Ulimboka ataendelea kushirikiana na madaktari
wenzie kudai haki zao za msingi ambazo hadi leo hazijalipwa.
Alisema,
ni wazi kwamba madai ya madaktari hasa kutaka wapewe vitendea kazi ni halali
kwa sababu wanataka iwe hivyo ili waweze kuwatumikia vizuri Watanzania.
No comments:
Post a Comment