To Chat with me click here

Tuesday, August 14, 2012

TUDAI HAKI BILA KUMWAGA DAMU : CHADEMA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka Serikali kuacha kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuangalia upepo wa kisiasa, ili kuepuka kuwapa wananchi mateso na umaskini.

Pia kimewataka wanachama wake, kudai haki zao kwa amani badala ya kutumia nguvu zinazoweza kusababisha umwagaji wa damu.

Rai hizo zilitolewa juzi  kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Makamu wake wa Zanzibar, Said Issa walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari.

Mbowe kwa upande wake, alitoa rai hiyo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, Zitto Kabwe, katika  mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Mnadani Mjini Katesh.

Zitto na wabunge wengine wa Chadema, walipita katika kijiji hicho wakitokea wilayani Rombo.

Katika hotuba hiyo, Mbowe alisema Chadema imedhamiria kufa ikiwa katika harakati za kupigania haki za wananchi ikiwemo ya kumiliki ardhi na kupinga uonevu wa aina mbalimbali, unaofanywa na baadhi ya watawala wasiokuwa waaminifu.

“Chadema imejipanga ili kuhakikisha kuwa haki za wananchi zinapatikana na wanatumia rasilimali zao kujinufaisha kiuchumi  kuliko ilivyo sasa wanapoambulia kula makopa,” alisema Mbowe kupitia hotuba yake.

Huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu katika uwanja huo, Zitto alisema, “Mara nyingi tumekuwa tukiambiwa kuwa Chadema ni wachokozi, nasema angalieni amani yetu msikubali damu imwagike na daini haki zenu kwa mapambanao ya amani bila ya kuchoka, Chadema tuko pamoja nanyi hadi kieleweke.”

Akizungumzia migogoro ya ardhi, Zitto alisema machafuko nchini Tanzania hayataletwa na udini wala ukabila na kwamba yatatokana na pengo kubwa la walionacho na wasiokuwa nacho.

“Kingine, ambacho kitaleta machafuko hapa Tanzania ni suala la ardhi, watu watachoka na utafika wakati wataamua kuwa liwalo na liwe, Chadema hatutaki kufika huko, naomba mtuamini ili mwaka 2015 tukamate dola na kurudisha ardhi yote ambayo mmenyang’anywa,”alisisitiza.

Katika mkutano huo, Chadema ilivuna wanachama wengi  waliokuwa wakigombania kupata kadi kutoka kwa Zitto, ambaye baadaye aliwakatalia kwa madai kuwa  muda umekwisha.

Kwa upande wake akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mbutu, wilayani Ulanga, katika operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, alisema uamuzi wa kufuata upepo wa kisiasa unawaumiza wananchi.

Alisema mwaka 1995 Serikali kupitia halmashauri ya wilaya hiyo, ilijenga zaidi ya visima 10 katika kijiji hicho ili kukinusuru Chama Cha Mapinduzi kilichokuwa kikikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa Chama cha Wananchi (CUF).

No comments:

Post a Comment