To Chat with me click here

Tuesday, August 21, 2012

SITTA: MSIISUBIRI SERIKALI KUTAJA WALIOFICHA MABILIONI

AWASHANGAA WANAOIPA MUDA HUKU WAKIWAFAHAMU WAHUSIKA, ASEMA HAIWEZEKANI MWANASIASA KATIKA NCHI MASKINI AWE BILIONEA, ATAKA WAKAMATWE WAFIKISHWE MAHAKAMANI

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amewataka wanaotangaza kuwafahamu vigogo walioficha mabilioni ya fedha nje ya nchi kuwataja mara moja ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao badala ya kuisubiri Serikali kufanya hivyo.Kauli hiyo ya Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), imekuja wakati baadhi ya wanasiasa, wakiwamo wabunge kutishia kuwataja watu hao, lakini wakisisitiza kuwa ni pale tu Serikali itakaposhindwa kufanya hivyo.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Fedha la Global Financial Integrity, unaonyesha kuwa tatizo la utoroshaji wa fedha nchini limekuwapo katika awamu zote za Serikali zilizoiongoza Tanzania, lakini Awamu hii ya Nne imetia fora.

Utafiti huo uliofanywa kuanzia mwaka 1970 hadi 2009, unaonyesha kuwa katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, fedha zilizofichwa nje ya nchi ni Dola za Marekani 7,967.4 milioni (sawa Sh12.7 trilioni).

Akizungumza katika mahojiano maalumu, kuhusu nini kifanyike ili kuiokoa Tanzania isiendelee kufilisiwa na watu wachache, Sitta alisema anasikitishwa na watu hao kuogopa na kuwaficha watu wanaofisadi mali za nchi na hasa pale inapokuwa wahusika ni vigogo wa Serikali.

Alisema vigogo hao ni sababu ya watu kupata kigugumizi katika hili akihoji : “Kwa nini linapokuwa ni suala linalowahusu hawa wanaoitwa vigogo hawatajwi?”

Sitta ambaye ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini katika awamu tofauti, alisema haoni kama kuna kosa kumtaja hadharani mtu aliyeficha fedha nje ya nchi huku akisababisha Watanzania kuendelea kukabiliwa na maisha magumu.

“Watajwe! Kama ni Samuel Sitta ameficha fedha nje atajwe. Kwa kweli mimi sioni kama kuna dhambi yoyote kumtaja,” alisema Sitta huku akisisitiza kwamba huo ni msimamo wake binafsi unaotokana na uzoefu wake kwenye uongozi wa nchi na siyo kwa mamlaka aliyonayo ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Alisema njia nzuri ya kukomesha tabia hiyo ni kuwataja na vyombo husika kuwafikisha mahakamani kwa kuzingatia kuwa sheria ni msumeno, haipaswi kubagua aliye mdogo au mkubwa kwa maana ya wadhifa katika nchi.Sitta ambaye pia aliwahi kuwa Spika wa Bunge alisema: “Swali la kwa nini hawatajwi, ni jambo la kushangaza.”

Alisema amesikia na kuwasoma baadhi ya wanasiasa wakitishia kuwa watawataja wahusika iwapo Serikali haitafanya hivyo, lakini akasema haoni sababu yoyote ya mtu kusita katika kuokoa taifa dhidi ya wizi wa fedha za umma.

“Haiwezekani kwa mwanasiasa yeyote katika nchi maskini kama Tanzania au kiongozi wa Serikali kuwa na utajiri wa mabilioni ya fedha.”

Alisema hata kama anafanya biashara, siyo rahisi kuwa na utajiri wa kiwango hicho hasa ikizingatiwa kuwa hutumia muda mrefu kulitumikia taifa.
“Sisi tunaofanya kazi serikalini, tunatoka saa moja usiku. Sasa muda huo wa kufanya biashara ni saa ngapi?”

Tuhuma hizo ziliibuka bungeni Jumatano iliyopita baada ya Kambi ya Upinzani kudai kwamba nawafahamu wahusika wa ufisadi huo na kutishia kuwataja ikiwa Serikali haitafanya hivyo.

Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe alipokuwa akiwasilisha hotuba ya kambi yake kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Fedha alisema miongoni mwa wanaomiliki fedha hizo ni kiongozi wa juu nchini pamoja na aliyepata kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Benjamin Mkapa.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kwamba kuna Watanzania 27, wakiwamo wanasiasa na wafanyabiashara walioficha mabilioni ya fedha huko Uswisi, huku mmoja wao akiwa anamiliki Dola za Marekani milioni 56 (sawa na Sh89.6 bilioni).

Katika uchunguzi huo ilibainika pia kuwa kiasi cha fedha kilichothibitishwa kumilikiwa na Watanzania hao ni jumla ya Dola za Marekani 186 milioni (takriban Sh300 bilioni) kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1,600 kwa Dola ya Marekani.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa mbali na kigogo anayemiliki Sh90 bilioni, wapo wengine wanne huku anayefuatia akiwa anamiliki Dola 30 milioni (Sh48 bilioni), mwingine dola 20 milioni (Sh32 bilioni) na wengine wawili kila mmoja anamiliki dola milioni 10 (Sh16 bilioni).  

Hiyo inamaanisha kwamba vigogo watano tu katika kundi hilo, wanamiliki Dola milioni 126 (Sh201.6 bilioni) sawa na asilimia 67.74 ya fedha hizo, wakati wengine 22 waliobaki wanamiliki Dola milioni 60 (Sh96 bilioni) sawa na asilimia 32.25.

Kwa hesabu za kawaida, kiasi cha Sh300 bilioni, kinaweza kugharimia ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya 33,300, ikiwa chumba kimoja kinagharimu kiasi cha Sh9 milioni.

Katika orodha ya walioweka fedha nchini humo, pia wamo wafanyabiashara wanaomiliki kiasi cha dola kati ya milioni mbili na milioni saba. Kadhalika, wamo wawili waliowahi kuwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere ambao akaunti zao zina kiasi kisichozidi Dola 500,000 kwa kila mmoja.

No comments:

Post a Comment