BAADHI YA WAISLAMU WAGOMEA, WAKAMATWA
SENSA
ya watu na makazi iliyoanza jana nchini kote, imegubikwa na kasoro kadhaa
katika maeneo mbalimbali, huku suala la uhaba wa vifaa kwa makarani likionekana
kuwa kubwa.
Hata
hivyo, mbali ya uhaba wa vifaa kwa makarani, pia tishio la baadhi ya viongozi
wa Kiislamu kuwashawishi waumini wao kususia, nalo lilileta mkanganyiko kwa baadhi
ya maeneo.
Katika
maeneo kadhaa, vilionekana vipeperushi kwenye baadhi ya nyumba vyenye ujumbe wa
kuwakataza Waislamu wasishiriki shughuli hiyo, jambo lililowalazimu polisi
kusambaa mitaani na kuwatia mbaroni baadhi ya watu waliodaiwa kuvisambaza.
Pia,
uelewa mdogo wa baadhi ya makarani nao ulilalamikiwa na wananchi wengi, kwani
walitumia muda mrefu kuandikisha taarifa zao na huku wakidai kuwa maswali
mengine yanayoulizwa kwenye dodoso hizo hayana maana yoyote.
Waislamu
wasusia Dar
Jijini
Dar es Salaam, makarani katika baadhi ya maeneo walikwama kupata takwimu za
baadhi ya wakazi kutokana na kushikilia msimamo wa viongozi wao wa kiroho wa
kususia sensa hiyo.
Tanzania
Daima ilifika kwenye maeneo tofauti ukiwemo Mtaa wa Kibondemaji wilayani Temeke
na kubaini changamoto hizo za baadhi ya waumini wa Kiislamu kupinga kuhesabiwa.
Akizungumza
na Tanzania Daima Mwenyekiti wa Mtaa huo, Rashidi Mrisho, alisema hadi sasa
kumekuwa na upinzani kutoka dhehebu hilo ambapo katika mtaa huo, nyumba zaidi
ya 13 zimepinga kuhesabiwa.
Alisema
waumini hao, wamedai kuwa shughuli hiyo imekiuka kipengele namba 2.109 hadi
2.111 cha Umoja wa Mataifa, kinachosema takwimu ni lazima ioneshe kila dhehebu
kama sehemu inayounda jamii nzima kwa ujumla wake, maelezo mafupi ya waumini wa
dini au dhehebu.
Aliongeza
kuwa, kitendo cha kutowalipa wajumbe wa mitaa, pia ni moja ya changamoto ambayo
imeifanya kazi hiyo kukosa msisimko wa kutosha.
Hata
hivyo, alisema kwa wajumbe waliopinga kutoa ushirikiano, majina yao
yatafikishwa ngazi za mbele zaidi kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
Naye
Mwenyekiti wa Mtaa wa Miembeni wilayani Ilala, Saburi Sabur, alisema pamoja na
watu wengi kutoa ushirikiano, bado baadhi ya Waislamu wameendeleza msimamo wao
wa kupinga kwa madai kuwa wanatii maelekezo ya viongozi wao.
Alisema
kuwa, katika mtaa huo inaonesha nyumba zipatazo 30 wakazi wake walipinga mpango
huo wa sensa, kwa kutotoa ushirikiano kwa makarani.
Akizungumzia
kuhusu malipo ya wajumbe wa mtaa, Saburi alisema tatizo hilo kwake halikuwapo
kwa kuwa kila mjumbe alilipwa sh 20,000 ambapo mwenyekiti alilipwa sh 100,000.
Katika
hatua nyingine, Saburi alisema iwapo upizani kama huo ukiendelea, kuna hatari
kazi hiyo ikashindwa kukamilika katika muda uliopangwa wa siku saba. Alifafanua
kuwa, katika mtaa huo shughuli hiyo ilichelewa kuanza kutokana na vifaa
kuchelewa kufika ambapo makarani ilibidi wakae kwa muda mrefu bila kazi hadi
vilipoletwa.
Wakati
gazeti hili linakwenda mitamboni, kulikuwa na taarifa kuwa kituo cha polisi
wilayani Temeke kimevamiwa na baadhi ya wananchi waliokuwa wakidai kupinga
kitendo cha wenzao kukamatwa baada ya kugomea sensa.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Temeke, Davis Misime licha ya kukanusha taarifa hizo, lakini
alikiri kuwa watu 17 walikamatwa kwa ajili ya mahojiano kwa kugoma kuhesabiwa
kabla ya kufikishwa mahakamani.
Alisema
watu hao ni kutoka maeneo ya Kindungulile kata ya Mianzini, Yombo
Kilakala-Barabara ya Mwinyi, Kiburugwa, Kigamboni na Kibada.
Kagera wakosa vifaa
Kutoka
mkoani Kagera katika Wilaya ya Biharamulo, makarani 1,999 wameilalamikia kamati
ya sensa kwa kuchelewa kuwagawia vifaa vya kazi katika vituo vyao.
Wakizungumza
na gazeti hili, baadhi ya makarani hao walisema hadi kufikia saa tatu asubuhi,
walikuwa hawajagawiwa vifaa hivyo.
Walisema,
kamati ya sensa wilayani humo, ilishindwa kutoa ushirikiano kwao hali inayoweza
kuchangia kutofanikiwa kwa shughuli hiyo licha ya kukaa kwenye vituo vyao kwa
muda wa siku tatu kama walivyoagizwa na wasimamizi wao wakisubiri vifaa.
Mmoja
wa makarani hao, Paulo Kamihanda kutoka Kata ya Nyarubungo, alisema kuwa vifaa
vya kazi zikiwemo sare, kofia pamoja na malipo ya siku ya kwanza na nauli bado
hawajapewa.
“Kulingana
na jiografia ya Biharamulo ilivyo, mpaka kufikia muda huu hatujakabidhiwa
vifaa, unategemea nini? Kama si kukwamisha sensa ni nini?” alihoji.
Aidha,
aliyataja baadhi ya maeneo ambayo yamecheleweshewa vifaa hivyo ni pamoja na
kata za Nyarubungo, Nemba, Nyantakala na Kalenge.
Mratibu
wa sensa wilayani humo, Richard Kalulu alikiri kuwepo kwa ucheleweshaji wa
vifaa, akisema vilipokelewa saa 6 usiku wa kuamkia jana kutoka Bukoba, hivyo
kusababisha uchelewaji huo.
Wakesha msikitini Arusha
Mkoani
Arusha, baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu juzi waliamua kukesha msikitini
kutimiza azima yao ya kutokuhesabiwa kama walivyohamasishwa na viongozi wao.
Wanaodaiwa
kukesha msikitini, ni baadhi ya waumini wa Msikiti Mkuu wa Bondeni, ambao
waliondoka hapo jana baada ya swala ya alfajiri.
Hata
hivyo, mwenyekiti wa msikiti huo, Abdulazizi Mkindi, alikanusha madai hayo kwa
kile alichowaeleza waandishi wa habari kuwa, awali walipanga kufanya mkesha
msikitini hapo kwa ajili ya kuiombea nchi amani, lakini waliahirisha baada ya
vifaa vya maandalizi kutotimia.
“Ni
kweli ilikuwa tufanye mkesha wa kuiombea nchi amani, kwani inapita kwenye
kipindi kigumu, kuna mambo ya sensa na mambo mengine, lakini ilibidi
tuahirishe kwani vifaa havikutimia… tulikuwa tumepata mbuzi saba na ng’ombe
mmoja, lakini swala hiyo ya mkesha itafanyika leo,” alisema.
Alisema
kuwa hao wanaodaiwa kulala msikitini hapo inaweza kuwa ni wageni ambao ni
utaratibu wa kawaida endapo Muislamu atafika mahali na kukosa pa kulala, basi
huenda msikitini.
Mkindi
alisema kuwa, msimamo wa kugomea sensa uliisha baada ya viongozi wa dini hiyo
kukutana na Rais Jakaya Kikwete Ikulu na kuahidi kufanyia kazi malalamiko yao.
Hata
hivyo, Katibu wa Baraza la Waislamu (BAKWATA) mkoani hapa, Abudulkareem Jonjo,
alikiri kupata taarifa za baadhi ya waumini kulala msikitini hapo, hivyo
kuwahimiza kuacha msimamo wa kutohesabiwa.
Mratibu
wa sensa mkoani hapa, Magreth Martin, alisema kuwa mpaka jana saa kumi
jioni, shughuli hiyo ilikuwa ikiendelea vizuri licha ya kuwepo kwa kasoro za
upungufu wa vifaa kama vizibao vinavyopaswa kuvaliwa na makarani wa sensa.
Baadhi
ya wananchi wilayani hapa nao waligoma kuhesabiwa, hivyo kuwafanya makarani wa
sensa kuwa katika wakati mgumu kupata takwimu zao.
Hali
hiyo ililazimu mratibu wa sensa kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa sensa, Mkuu wa
Wilaya, John Mongela na kuitisha kikao cha dharura kushughulikia tatizo hilo
haraka.
Akizungumza
na gazeti hili, mratibu wa sensa, Palangyo, alisema maeneo yaliyokutwa na
changamoto hiyo ya mgomo ni kata za Elerai, Ngarenaro, Oysterbay, Engutoto,
Sombetini na Unga Limited ambapo wahusika walikataa kuandikishwa bila kutoa
sababu zozote.
Iringa shwari
Mkoani
Iringa, shughuli ya sensa ya watu na makazi ilianza katika hali ya utulivu
katika maeneo mbalimbali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Iringa, Michael Kamuhanda, alisema kuwa tangu kuanza shughuli hiyo
saa 6 usiku wa kuamkia jana, hakuna tukio lolote la
uvunjifu wa amani ambalo limetokea.
Alisema kuwa,
jeshi hilo linaendelea kujipanga kuona kila Mtanzania anatumia
haki yake ya msingi katika kuhesabiwa bila kuzuiwa na mtu ama
kikundi chochote.
Vifaa adimu Dodoma
Uhaba
wa vifaa kwa makarani umeukumba pia Mkoa wa Dodoma jana wakati shughuli ya
sensa ya watu na makazi ikianza rasmi nchini nzima, hivyo kuleta usumbufu.
Mkuu
wa mkoa huo, Dk. Rehema Nchimbi, alithibitisha uwepo wa kasoro hiyo akisema
ilitokana na upungufu wa vifaa kama majaketi kwa ajili ya makarani.
Alisema
kuwa majaketi hayo ambayo hutumika kuwatambulisha makarani hayakuweza kufika
kwa wakati na kusababisha baadhi yao kutumia vitambulisho kwa kuvaa shingoni
badala ya makusudio ya awali.
Alipoulizwa
ni kwanini vifaa hivyo vimechelewa kufika wakati maandalizi ni ya muda mrefu,
alisema kuwa jambo hilo lipo nje ya uwezo wake kwani vifaa vyote vilikuwa
vinapakiwa kutoka jijini Dar es Salaam kupelekwa katika mikoa mbalimbali.
Hata
hivyo, alisema kutokana na kukosekana kwa vifaa hivyo, bado hakuzuii shughuli
ya sensa kuendelea.
Baadhi
ya wananchi waliozungumza na gazeti hili, walisema pamoja na siku hiyo kuwa ya
Jumapili, lakini wamepoteza muda wao mwingi kuwasubiria makarani bila
mafanikio.
Geita utata mtupu
Mkoani
Geita, sensa ya watu na makazi imekuwa na utata mkubwa baada ya vifaa kuchelewa
kukabidhiwa kwa makarani, baadhi ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji kususia
kushiriki na kucheleweshwa kwa malipo ya makarani.
Baadhi
ya wananchi waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, walisema shughuli
hiyo haiwezi kufanikiwa kwa asilimia 100 kutokana na maandalizi kuwabagua
viongozi hao wa vijiji na vitongoji licha ya serikali kutambua wazi kuwa ndio
wapo karibu zaidi na wananchi.
Mwenyekiti
wa Kitongoji cha Elimu, Khasan Mwibara na Khamisi Jagi ambaye ni mwenyekiti wa
Kitongoji cha Nyantorontoro, Kata ya Kalangalala, walisema wameshindwa kutoa
ushirikiano wa kutosha kwa makarani hao kutokana na wao kutoshirikishwa katika
mchakato mzima tangu awali.
Walidai
kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakiwapigia simu tangu kuanza kwa sensa jana
asubuhi baada ya kuwafananisha makarani na vibaka kutokana na kutokuwa na sare,
vitambulisho wala kutembezwa na kiongozi yeyote wa kijiji au kitongoji.
Mratibu
wa Sensa Mkoa wa Geita, Ersmus Lugarabamu, alikiri shughuli hiyo kukumbwa na
changamoto mbalimbali na kudai kuwa hali hiyo ilitokana na serikali
kuchelewesha vifaa vilivyohitajika kutoka jijini Dar es Salaam.
Mbali
ya changamoto hizo, alisema tayari baadhi ya vifaa vimewasili japo kwa
kuchelewa, na kwamba vimegawiwa na kazi inatarajiwa kuendelea vizuri kuanzia
leo.
No comments:
Post a Comment