TAKUKURU YASEMA
IMEANZA KUWACHUNGUZA
SIKU
moja baada ya Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto,
kutishia kuwataja vigogo wa serikali walioficha mabilioni ya fedha kwenye
akaunti za nje ya nchi, ikiwa serikali haitawataja, Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imeibuka na kudai kuwa inazifanyia kazi tuhuma
hizo.
Zitto
alisema kuwa wamepata taarifa kuwa mmoja wa viongozi wa juu nchini
na baadhi ya mawaziri wa serikali za awamu zilizopita ni miongoni mwa
wamiliki wa fedha hizo zipatazo sh bilioni 314.5.
Alisema
sehemu kubwa ya fedha hizo zililipwa na kampuni za utafutaji wa mafuta na
gesi katika pwani ya Mkoa wa Mtwara, zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na
2006, hivyo akaitaka serikali iwataje wahusika na kuwachukulia hatua,
vinginevyo atawataja kwa majina.
Hata
hivyo, Mkurugenzi wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah, jana alijitokeza katika
Kipindi cha Baragumu kinachorushwa na kituo cha runinga cha Channel Ten na
kusema kuwa tayari wameanza kazi ya kuchunguza tuhuma hizo.
“Jambo
lolote likituhumiwa lazima lifuate taratibu, TAKUKURU imeshawasiliana na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sababu ndiyo mamlaka ya kuwasiliana na Uswisi,
tufahamu ni kiasi gani benki za Uswisi zinacho na ni kina nani wamehusika,
tumfuatilie nani amehusika na ufisadi huo na kupeleka hizo fedha huko,”
alisema.
Alisema
kwa sasa Uswisi wanayafanyia kazi madai hayo na wakikamilisha kazi hiyo
watapeleka majibu kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kisha TAKUKURU watajua
maeneo gani ya kuyafanyia kazi.
“Kumekuwapo
na dhana kwamba hatuwafikishi mahakamani na kwamba kuna watu wametuhonga ili
tusifanye hivyo; kama kuna ushahidi tutaachaje kumfikisha mtu mahakamani? Ni
aibu kumfikisha mtu mahakamani halafu ionekane huna ushahidi, lakini
tukubaliane kwamba kazi inafanyika,” alisema Dk. Hoseah.
Tuhuma kwa wabunge
Kuhusu
tuhuma za baadhi ya wabunge wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kudaiwa
kujihusisha na rushwa, Dk. Hoseah alisema wanasubiri Bunge limalize kazi yake
ndipo nao wafanye kazi yao.
“Itakumbukwa
kwamba Mheshimiwa Spika aliunda kamati ya kushughulikia yaliyojitokeza kwa
baadhi ya wabunge, tutakachofanya ni kusubiri Bunge lifanye kazi yake,”
alisema.
Alisema
hatua zitachukuliwa lakini lazima wapishe kamati ya Bunge ifanye kazi yake
kwanza. Alisisitiza kuwa wanasubiri ripoti ya kamati hiyo ambayo ilipewa wiki
mbili imalize kazi yake ili iwasaidie kuona maeneo gani ya kuyafanyia kazi.
“Sisi
tunajikita zaidi kuona sheria ya kupambana na rushwa inavyokwenda, ikiwamo
kuona kama kuna mtu alihongwa,” alisema Dk. Hoseah.
Alisema
si kila tuhuma TAKUKURU inaweza kuibaini, lakini kuna zile ambazo wamekuwa
wakizifanyia kazi ambapo tayari wameshaanza kuwahoji baadhi ya wabunge.
Alisema
taasisi yake haiwezi kutangaza kwa umma kila kitu, kwani sheria inawabana,
kwamba wanapokuwa wanamchunguza mtu yeyote au taasisi hawaruhusiwi kwenda
kutangaza.
Gharama za uchaguzi
Alisema
taasisi hiyo inafanya kazi na hadi sasa kuna kesi 24 mahakamani zinazowahusu
wanasiasa mbalimbali kudaiwa kuhusika na vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi.
Alisema
sheria hiyo ilianza kutumika mwaka 2010, dhana yake kubwa ni kuzuia vitendo vya
rushwa wakati wa uchaguzi kwa kumzuia mgombea kutowarubuni wananchi kwa fedha
ili washawishike kumchagua.
“Mwanasiasa
yeyote anapotaka kuingia kwenye ulingo wowote wa siasa lazima awe na fedha ili
aweze kufanya hivyo, vitu vyote vinakubalika, lakini asichoruhusiwa kufanya ni
kuwarubuni wananchi kwa zawadi, usafiri, chakula na mengine ili wamchague,”
alisema Dk. Hoseah.
Pamoja
na mambo mengine, alisema kuna haja ya kuangalia mfumo mzima kwa vyama vya
siasa ili kumudu gharama za uchaguzi wakati wa uchaguzi.
Aliweka
wazi kwamba ni vigumu kushughulikia vitendo vya rushwa, kwa sababu ofisi za
TAKUKURU hazijafika kwenye maeneo ya kata, bali wako kwenye wilaya.
Alisema
ili kuvidhibiti ni jukumu la wanasiasa wenyewe kuheshimu suala hilo kwa kuepuka
kutoa rushwa.
No comments:
Post a Comment