To Chat with me click here

Saturday, August 25, 2012

BBC KATIKA HISTORIA MPYA YA KIHABARI


 Mhariri Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Ali Saleh

SHIRIKA la Utangazaji la Uingereza (BBC), limepiga hatua katika historia ya utangazaji wa kimataifa kwa kuanzisha matangazo ya Kiswahili (Dira ya Dunia) kupitia televisheni.

Kipindi hicho kitaanza kurushwa nchini Tanzania na katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kuanzia keshokutwa Jumatatu, Agosti 27, 2012 kupitia kituo cha televisheni cha Star (Star TV) kuanzia saa tatu usiku.

Hii ni mara ya kwanza kwa Shirika la Utangazaji la Kimataifa kurusha matangazo ya televisheni katika lugha ya Kiswahili. Kwa miaka mingi, zaidi ya hamsini, matangazo ya Kiswahili yamekuwa yakirushwa kupitia vituo vya radio.

Mhariri Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Ali Saleh anasema:“Hatua hii ni dhihirisho kwamba BBC inakwenda na mabadiliko ya teknolojia, kwa kuzingatia matakwa ya hadhira”.

Aliongeza: “Dira ya Dunia kupitia televisheni ni jukwaa mwafaka la kuonyesha sura ya Afrika ambayo haijapata kuonekana kabla. Afrika ni bara ambalo linashuhudia mabadiliko makubwa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Kama ilivyo desturi ya BBC, tuzingatia maadili ya kuwa huru, kutangaza kwa njia halisi na isiyopendelea upande wowote.” 



Kwa takriban miaka 60 Idhaa ya Kiswahili ya BBC imejenga sifa na kupitia matangazo yake ya radio kama vile, Dira ya Dunia,  Amka na BBC na Michezo. Idhaa ya Kiswahili ya BBC inajivunia kuwa na wasikilizaji takriban milioni 20.

Kipindi cha televisheni kitafungua ukurasa mpya katika uhusiano kati ya BBC na wasikilizaji ambao sasa wanageuka kuwa watazamaji.

Kipindi hicho kitakuwa kikirushwa kila siku, Jumatatu hadi Ijumaa, kupitia vituo washirika. Nchini Tanzania kitaonyeshwa kupitia Star TV. Nchini Kenya kitakuwa kwenye kituo cha QTV huku mipango zaidi ikifanywa kukisambaza katika kanda nzima ya Afrika Mashariki na Kati.

Mtangazaji kinara wa kipindi hicho ni Salim Kikeke ambaye anasema: “Naona fahari kubwa kushiriki katika hatua hii kubwa na ya kihistoria ya kuanzisha matangazo ya televisheni”.

Tumekuwa tukifanya kila tuwezalo kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri kabla ya kuzindua kipindi hiki ambacho tunatumia kitawavutia wengi,”anasema Kikeke na kuongeza:

“Hiki ni kipindi ambacho kinatumia lugha inayounganisha wana Afrika Mashariki na Kati. Huenda wakati mmoja Kiswahili kikasambaa katika Bara zaima la Afrika.”

Kwa jumla wasikilizaji wengi wa matangazo ya BBC kupitia kwenye redio wapo barani Afrika. Zaidi ya watu milioni 80 wanasikiliza BBC kupitia lugha za Kiingereza, Kiswahili, Kihausa, Kisomali, Kinyarwanda/Kirundi, Kiarabu na Kifaransa.

Barani Afrika kwenyewe mengi yameripotiwa na BBC kama vile harakati za ukombozi, mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, kuachiliwa kwa shujaa Nelson Mandela na maandalizi ya kombe la dunia la mwaka 2010 nchini Afrika Kusini ikiwa ndiyo mara ya kwanza na ya kihistoria kwa bara Afrika kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya kimataifa.
 
Utazamaji wa televisheni unaongezeka kwa kasi hasa katika sehemu za mijini.

Kutokana na teknolojia mpya aina ya digitali, idadi ya stesheni za Televisheni itaongezeka, hivyo ushindani ni jambo linalotarajiwa.

Mhariri wa Idhaa ya Afrika ya  BBC, Solomon Mugera kwa upande wake anasema: “Mkakati wa BBC ni kuhakikisha matangazo yetu yanapatikana kwenye redio, televisheni, tovuti, facebook na simu ya mkononi.”

“BBC pia imezindua kipindi kama hiki kwa lugha ya Kiingereza kuangalia masuala makubwa katika bara Afrika na kujenga daraja kati ya bara hili na Ulimwengu mzima.”

Nathan Lwehabura ambaye ni , Meneja mipango na utafiti wa Sahara Media Group Ltd, ambao ni wamiliki wa Star Tv anasema: “ Ni heshima kubwa kwa Star TV kujumuisha Dira ya Dunia katika vipindi vyake vya kila siku, tunaamini kipindi hiki kitavutia watu wengi”.

Anaongeza: “Kipindi cha BBC cha Kiingereza (Focus on Africa) kilichozinduliwa hivi karibuni kupitia Star TV tayari kimepata watazamaji wengi kutokana na jinsi kinavyozingatia weledi na utangazaji wenye ubora wa hali ya juu.

No comments:

Post a Comment