Mwaka 1975 Mwanafunzi
wa mwaka wa Kwanza wa Chuo Kikuu cha Haile Selasie (sasa Chuo Kikuu cha Addis
Ababa) Legese Zenawi, akiwa na umri wa miaka 19 tu, aliacha masomo yake na
kujiunga na kikundi cha Ukombozi cha watu wa Tigray (Tigray Peoples Liberation
Front). Legese alikuwa anasomea shahada ya kwanza ya udaktari. Hakurudi tena
Chuoni kusomea Udaktari na hakuishi tena maisha ya ujana ambayo sisi wengine
wote tumeishi na kuyafurahia. Mwaka 2012 Legese akiwa na umri wa miaka 57
alifariki dunia. Lakini aliaga dunia akiwa Meles Zenawi na sio Legese Zenawi,
jina alilopewa na wazazi wake huko Adwa kaskazini mwa Ethiopia.
Legese alibadili jina
lake kwa hiari yake kufuatia kuuwawa kwa rafiki yake na mpiganaji mwenzake
Meles mwaka 1975. Aliamua kumuishi mpiganaji mwenzake kwa kuchukua jina lake na
kuacha jina alilopewa na wazazi wake. Meles alifanikiwa kupigana dhidi ya
utawala wa kiimla wa Mengistu Haile Mariam na kumtoa madarakani na kuingiza
uongozi wa kimaendeleo chini ya chama cha Kitaifa cha Ethiopian People’s
Revolutionary Democratic Front (EPRDF). Meles Zenawi aliahidi kumpigania rafiki
yake Meles kwa faida ya wananchi wanyonge wa Ethiopia na akatimiza ahadi hiyo
kwa mafanikio makubwa sana.
Mwanzoni Meles
alipigana kwa lengo la kutaka uhuru wa eneo la Tigray kutoka Utawala
wa Mengistu na kundi la wanajeshi chini ya Derg. Meles na wenzake
waliamini kabisa kwamba utawala nchini mwao chini ya Mfalme Haile Selasie na
hata chini ya utawala wa Derg uligubikwa na ukabila na ueneo kwa faida ya
kabila kubwa nchini humo, Amhara.Aliamini kwamba makabila madogo kama kabila
lake la Tigray kutoka kaskazini mwa Ethiopia na hata makabila mengine kama
Wasomali walikuwa wanakandamizwa na kunyonywa ndani ya nchi yao. Aliamini
kwamba utajiri wa nchi ulikuwa unatumika kwa faida ya kundi moja
lililohodhimadaraka ya nchi na kabila lao. Akiwa na umri wa miaka 19 tu na
mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu aliamua kushika silaha na kupambana
na ugandamizaji huu.
Hata hivyo Meles
alibadili kabisa mtazamo wake alipogundua kuwa sio watu wa Tigray tu waliokuwa
wakinyonywa na kugandamizwa na utawala wa Mengistu bali ilikuwa ni WaEthiopia
wote bila kujali makabila yao. Mwaka 1985 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama
cha TPLF akiwa na umri wa miaka 29 tu.Alihakikisha anaikomboa Tigray kama
mkakati wa kuikomboa Ethiopia yote. Alishirikiana na wakombozi wa Jimbo jirani
la Eritrea ili kutetea Uhuru wao na kuwapa uhuru wa kuamua kama wanataka
kubakia sehemu ya Ethiopia au kuwa Taifa huru ambapo waliamua kuwa Taifa huru.
Akiwa kijana wa chini ya umri wa miaka 30 aliunganisha makundi mbalimbali
yaliyokuwa na lengo la kuleta ukombozi na kujenga Ethiopia mpya chini ya
mwavuli ya chama cha EPRDF. EPRDF ilikuwa ni umoja wa makabila yote nchini
Ethiopia na walimchagua Meles kuongoza mapamabano ya ukombozi.
Mwaka 1991 Meles
Zenawi aliongoza EPRDF kuingia Addis Ababa na kushika Dola huku Mengistu
akikimbilia nchini Zimbabwe. Meles akiwa na umri wa miaka 36 tu alichaguliwa
kuwa Rais wa muda wa Ethiopia na mkutano mkuu wa kitaifa ambao kwa mara ya
kwanza ulikutanisha makabila yote nchini Ethiopia. Miaka mitatu baadaye
kufuatia kura ya maoni Jimbo la Eritrea likajitenga kutokaEthiopia na kuunda
Taifa huru. Meles alitimiza ahadi yake ya kuruhusu watu wa Eritrea kuamua kama
wanataka kuwa Taifa linalojitegemea au kuwa sehemu ya Shirikisho la Ethiopia.
Hata mahusiano kati ya Ethiopia na Eritrea yalipokuwa mabaya sana kiasi cha
kupigana vita kugombea kijiji cha Badme, Meles hakuchukua fursa hiyo kuirudisha
Eritrea kuwa mkoa ndani ya Ethiopia au hata kupata njia ya kwenda baharini,
bali aliheshimu matakwa ya waEritrea ya kujitawala.
Ukweli ni kwamba vita
kati ya Eritrea na Ethiopia ilikuwa ni vita isiyo na maana yeyote ile na
itabakia kuwa doa katika historia ya uongozi wa Meles. Kitendo cha Meles
kutoheshimu maamuzi ya Umoja wa Mataifa kwamba Badme ni sehemu ya Eritrea pia
ni doa ambalo wafuasi wa Meles wataendelea kuwa nalo daima dumu na wakosoaji wa
Meles wataendelea kujengea hoja kuonyesha kuwa Kiongozi huyu hakuwa anaheshimu
maamuzi ya Taasisi za kimataifa. Hata hivyo doa hili haliwezi kufuta kabisa
mafanikio makubwa ambayo kamaradi Meles ameyapata katika Ethiopia
iliyokombolewa.
Meles alipochaguliwa
kuwa Kiongozi wa chama cha TPLF mwaka 1985 Ethiopia ilikuwa kwenye ramani ya
dunia kama Taifa lililoshindwa kulisha watu wake. Dunia nzima kulikuwa na
kampeni za kusaidia kuondoa njaa nchini humo ambayo iliua zaidi ya watu milioni
moja. Wakati mauaji ya kimbari nchini Rwanda yaliua watu milioni moja kwa
mapanga na mashoka, njaa iliua watu kama hao hasa katika maeneo ya Tigray na
Wollo kwa sababu ya uzembe wa Serikali ya Mengistu. Mmoja wa wajumbe wa
Kamati Kuu wa chama cha Mengistu kilichokuwa kinatawala wakati ule (Workers
Party of Ethiopia) bwana Dawit Wolde alimtahadharisha Mengistu kuhusu hali
mbaya ya wananchi na kwamba Serikali ilipaswa kuchukua hatua na kujibiwa
‘kulikuwa na mabaa ya njaa miaka yote kabla sisi hatujatawala. Hiyo ni namna
uasili (nature) inafanya kazi yake. Kuingilia uasili ndio maana leo tumefikia
watu milioni 40’( Meredith in The State of Africa). Mengistu alilewa madaraka
kiasi cha kusahau kwamba siku moja kabla ya kumvua madaraka Mfalme Haile
Selasie walimwonyesha filamu (The hidden famine) ya namna yeye alivyokuwa
anastarehe na pombe aghali na kulisha nyama mbwa wake ilhali wananchi wake
walikuwa wanakufa kwa kukosa chakula katika baa la njaa la mwaka
1984 katika Wilaya ya Wollo. Haile Selasie baada ya kuonyeshwa filamu
hiyo alipoteza fahamu kwa mawazo na siku iliyofuata tarehe 12 Septemba 1974 akavuliwa
ufalme na vijana watatu wanajeshi akiwemo Mengistu Haile Mariam. Mengistu
huyo huyo akiwa Rais wa Ethiopia akawa anajenga hoja kwamba njaa ni tukio la
asili ili ‘kubalance’ idadi ya watu nchini mwake! Haya ndio mazingira ambayo
Meles alichaguliwa kwayo kuongoza mapambano ya ukombozi akiwa na umri wa miaka
29 tu.
‘naomba vitabu vya
Uchumi’ ndio ombi pekee Meles alilitoa kwa mwanahabari wa kigeni
aliyekwenda kumfanyia mahojiano mara baada ya kuchukua uongozi wa Taifa lake.
Mwanahabari huyo alimwuliza ni msaada gani anataka kutoka kwa nchi za magharibi
ili awaambie kupitia habari yake anayokwenda kuandika. Meles alijua kwamba ana
ajenda moja kubwa nayo ni kuondoa njaa. Kuondoa Umasikini nchini mwake. Ajenda
hii Meles aliifanyia kazi kwa nguvu zake zote kipindi chote ambacho yeye
alikuwa Rais na Baadaye Waziri Mkuu wa Ethiopia.
Nakumbuka tulikuwa
tunatania mtu yeyote aliyekondeana kwa kusema ‘ana njaa kama Ethiopia’ na hiyo
ndio ilikuwa picha inayokuja machoni mwa watu wengi duniani kuhusu Ethiopia. Meles
hakumaliza shida zote za Ethiopia, lakini alipambana nazo. Alizipunguza.
Amelitoa Taifa lake kutoka Taifa la kupigiwa mfano kwa njaa na umasikini kwenda
Taifa la kupigiwa mfano kwa maendeleo. Katika kipindi cha miaka ishirini ya
utawala wake hatujasikia baa kubwa la njaa kama ilivyozoeleka kila muongo
nchini humo. Mwana historia mmoja nchini humo alionyesha kuwa kila muongo
ulikumbwa na njaa kali nchini Ethiopia, 1958, 1966, 1973 na 1984. Lakini toka
Meles achukue uongozi wa Taifa la Ethiopia hatukusikia njaa miaka ya tisini
wala miaka ya 2000. Ninaamini watakaomrithi Meles watahakikisha kuwa hakuna
njaa tena ya kiwango kile nchini Ethiopia kwa miongo mingine yote ijayo.
Mafanikio haya yanatokana na sera na maamuzi thabiti na ya dhati kutoka kwa kiongozi
‘Sitaki njaa nchini kwangu’. Pia usimamizi thabiti wa maamuzi sahihi
yaliyotolewa.
Meles aliamua
kupambana na umasikini na kujenga Taifa lenye nguvu za kiuchumi. Aliamua mapema
kabisa kukataa ushauri wa IMF na Benki ya Dunia wa kuufungua uchumi wa Ethiopia
haraka sana (liberalisation). Yeye na wenzake waliamua kuufungua uchumi kidogo
kidogo kulingana na ratiba waliyojiwekea wao wenyewe. Kutokana na hali hiyo
sehemu kubwa ya uchumi wa Ethiopia umeshikwa na wao wenyewe wananchi wa
Ethiopia. Amejenga miundombinu kuunganisha uchumi wa nchi na hivyo kufungua
masoko ya ndani licha ya yeye mwenyewe Meles kusisitiza sana mauzo ya
nje. Kutokana na maamuzi yake, hivi sasa Ethiopia itaanza kuuza nje Viatu
vya ngozi vilivyotengenezwa nchini humo vyenye thamani ya dola za kimarekani
bilioni nne. Hii ni sawa na mara mbili ya mauzo ya dhahabu yote ya Tanzania
kwenye soko la dunia. Ethiopia haina mafuta wala madini ya kutosha kama
Tanzania, lakini uchumi wake umekuwa ukikua kwa zaidi ya asilimia kumi kwa
miaka saba mfululizo. Ndio maana Meles ameweza kupunguza umasikini kutoka
asilimia 45 ya watu waliokuwa wakiishi kwenye dimbwi la umasikini mwaka 1991
mpaka asilimia 29 mwaka 2011. Katika kipindi kama hicho (1991 – 2011) Umasikini
Tanzania ulishuka kutoka asilimia 37 ya watu kuishi kwenye dimbwi la Umasikini
mpaka asilimia 35 tu. Tanzania iliamua kufuata sera za kufungua uchumi wa nchi
kwa haraka kama walivyoshauri Taasisi za IMF na Benki ya Dunia.
Wakati Meles anaaga
dunia ameacha mradi mkubwa sana unatekelezwa nchini mwake. Mradi wa
kuzalisha umeme 10,000 MW, Grand Millenium Project. Lengo lake ni kuzalisha
umeme wa kutosha kufanya mabadiliko makubwa ya maisha ya wananchi wa Ethiopia
na pia kuuza nchi jirani (Diplomasia ya Nishati). Benki ya Dunia ilikataa
kufadhili mradi huu, yeye akaamua kila muEthiopia kutoa fedha za kufadhili
mradi huu. Wananchi wa Ethiopia wote kila mmoja akajitolea mshahara wake wote
wa Mwezi mmoja na fedha hii kugeuzwa kuwa dhamana. Pia wananchi wa Ethiopia
wanaoishi nje ya nchi nao waliruhusiwa kununua dhamana hizi na kufadhili
mradi huu kabambe. Mradi unatekelezwa kwa fedha za WaEthiopia wenyewe. Nina
imani kuwa mradi huu utaendelezwa na viongozi wapya wa Ethiopia. Uzuri ni
kwamba Meles alilea kizazi kipya cha uongozi. Aliamua kuchukua vijana wa rika
mbili chini yake na kuwapa majukumu na kuwalea kiuongoni ili waweze kuwa tayari
kurithi mikoba ya viongozi wanaomaliza muda wao. Waziri Mkuu mpya wa
Ethiopia ana umri wa miaka kumi chini ya Meles. Meles alijua umuhimu wa
kuandaa viongozi wa baadaye. Yeye hakuandaliwa. Mazingira ya ugandamizwaji,
unyanyasaji na umasikini yalimwita kuchukua majukumu ya kiuongozi akiwa kijana
mdogo sana wa miaka 19 alipoamua kujiunga na jeshi la ukombozi, miaka 29
alipochaguliwa kuongoza jeshi la ukombozi na miaka 36 alipochaguliwa kuwa Rais
na baadaye Waziri Mkuu wa Taifa lake.
Meles ana makosa yake
kama binaadamu. Amelaumiwa sana na mataifa ya magharibi kuhusu rekodi yake ya
masuala ya haki za binaadamu na kidemokrasia. Lakini pia amelaumiwa na baadhi
ya wanaharakati kwa kuuza ardhi ya wananchi kwa makampuni ya kilimo ya
mashariki ya kati na mashariki ya mbali kama China. Hata hivyo sijawahi kusikia
tuhuma zozote za Meles kuhusu ufisadi na kujilimbikizia mali. Siku zote
aliamini kuwa cheo ni dhamana na hakutumia cheo chake kwa faida yake
tofauti na viongozi wengi sana wa kiafrika. Hapa nchini kwetu tunashuhudia watu
wakitumia nafasi zao za uongozi kulimbikiza mali. Watu wana tamaa iliyokithiri
ya mali. Ufisadi imekuwa ni hulka na sasa ufisadi unahusisha nafasi yeyote ya
uongozi. Hata tuhuma za ufisadi na rushwa zimekuwa za kawaida mno mpaka unakuta
wala rushwa wanatuhumu viongozi wenye maadili ili mradi tu ionekane rushwa ni
ya kila mtu wa kila chama. Imekuwa kama Wezi kuungana kumkimbiza
Polisi. Meles hakutaka Ethiopia ifikie hali hii. Alipambana na rushwa yeye
mwenyewe kwa kujiwekea viwango vya kutokuwa na mawaa ya rushwa au matumizi
mabaya ya Ofisi ya Umma.
Meles Zenawi ameacha
mfumo wa Uchumi ambao haujapata fursa ya kujadiliwa vya kutosha. Mfumo ambao
umeiweka Ethiopia kuwa moja ya mataifa yatakayokuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi
katika bara la Afrika ndani ya muongo mmoja na nusu ujao. Meles alipambana na
umasikini kwa dhati na kwa nguvu inayostahili. Meles ametimiza wajibu wake.
Natamani kuwa
Meles maana ameishi anachoamini kwa kupambana na ufisadi bila yeye kuwa
fisadi ama kutumia vibaya Ofisi yake ya Umma. Nitaishi kuwa Meles maana
adui wetu nambari moja ni Umasikini, umasikini wa vijijini. Meles alitangaza
mwaka 1991 ‘our first enemy is poverty and backwardness’ na akapambana na
adui umasikini kadiri ya uwezo wake. Hakuna namna bora zaidi ya kumuenzi
Meles zaidi ya kutenda yale mema aliyoyatenda na kurekebisha yale aliyoyakosea.
Nilipata fursa ya
kukutana na Meles mara moja. Nilikutana naye nchini Nigeria katika mkutano
kuhusu mashirikiano ya kiuchumi kati ya nchi za Ulaya na nchi za Kiafrika mwaka
2009. Baada ya mkutano ule niliamua kumsoma Meles na misingi anayosimamia. Ni
kama nilimwona Mahathir Mohamad wa Malaysia ndani ya Meles Zenawi kwa
namna ya utendaji wao na uwezo wao wa kujenga hoja. Isipokuwa tu Meles
hakumaliza shahada yake ya udaktari na Mahathir alimaliza yake. Ni dhahiri
kwamba Meles Zenawi alikuwa ni kiongozi mwenye uwezo mkubwa sana kiakili
pengine kuliko viongozi wote wa kizazi cha pili barani Afrika. Uwezo wake wa
Akili uliwatisha viongozi wa mataifa ya Magharibi. Walimwogopa. Wenzake wa
Afrika walimheshimu. Alikuwa sauti ya Afrika kutoka Addis Ababa, Makao makuu ya
Afrika.Upumzike kwa amani Meles.
No comments:
Post a Comment