To Chat with me click here

Wednesday, August 22, 2012

LOWASSA: MKAPA ALIKUZA UCHUMI, JK PUNGUZA MATUMIZI

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ameitaka Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kupunguza matumizi na kufanya uamuzi wa kukuza uchumi kama ilivyokuwa wakati wa mtangulizi wake, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.

Lowassa alisema, Mkapa alifanya uamuzi mgumu kiuchumi uliowezesha nchi kupiga hatua zaidi kimaendeleo ikilinganishwa na sasa ambapo taifa limekumbwa na mfumuko mkubwa wa bei.

“Serikali ipunguze matumizi ili kupunguza Inflation (mfumuko wa bei) kwani ni tatizo kubwa,” alisema Lowassa katika kipindi cha dakika 45 kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV juzi usiku na kuongeza:

“Rais Mkapa wakati wake alifanya maamuzi  mengi ya uchumi, lakini pamoja na wakati wake watu kuuita ukapa, bado alifanya maamuzi mazuri na uchumi ukaenda juu.”

Lowassa alimsifu Mkapa akisema, alifanya uamuzi mgumu wenye lengo la kukuza uchumi na kuyasimamia jambo ambalo linapaswa kuwa mfano kwa Serikali zingine.

“Tusikubali hivyo, tufanye maamuzi ya msingi na tuyaeleze hivyo… Rais Mkapa wakati wake alifanya maamuzi ya kiuchumi akayasimamia, sasa tufanye maamuzi ya namna hiyo na kuyasimamia," alisema Lowassa na kuendelea: 

“Mfumuko (wa bei) umefikia asilimia 17.9. Imekuwa hivyo kwa muda mrefu. Wakati wa Rais Mkapa ulishuka zaidi.”

Alisema Serikali ya Rais Kikwete imefanya mambo makubwa, lakini inatakiwa kubana matumizi ili ukuaji wa uchumi umnufaishe mwananchi wa kawaida.

Lowassa  ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, alisema ili ukuaji wa uchumi umnufaishe mwananchi wa kawaida, lazima mambo matano yafanyike. Alitaja mambo hayo kuwa ni pamoja na usalama wa chakula, upatikanaji wa mafuta na kilimo cha mashamba makubwa.

“Lakini la muhimu zaidi ni Serikali kupunguza matumizi. Lazima Serikali ipunguze matumizi ili kupunguza ‘inflation’ (mfumuko wa bei) lazima kupunguza matumizi, lazima sana,” alisisitiza Lowassa.

Kuhusu usalama wa chakula, Lowassa alitaka wakulima waruhusiwe kuuza mazao yao nje ya nchi bila bughudha.

“Kuna maeneo ambayo nadhani hatujayafanyia kazi, moja ni ‘Food Security’ (usalama wa chakula). Tuangalie uwezekano wa kuongeza hizo barabara zitumike kuwasaidia wakulima,” alisema na kuongeza:

“Kwa mfano wanalima mazao yao Rukwa, tusiwalazimishe kuyauza Arusha kwa sababu gharama za kuyatoa mahindi kutoka Rukwa hadi Arusha ni kubwa mno…Anayetaka kuuza Kenya auze, anayetaka kwenda Burundi ayapeleke. Wakulima wapate nafasi ya kuuza mazao yao kwa uhuru kwa haraka na kwa bei nzuri, hilo ni muhimu sana,” alisema Lowassa.

Kuhusu suala la mafuta alisema ,aliishauri Serikali kununua mafuta kwa wingi wakati wa bei ni nzuri.

Aliitaka Serikali kuchukua uamuzi mgumu katika kuimarisha kilimo cha mashamba makubwa na matumizi ya zana za kilimo za kisasa hasa matrekta.

“Trekta ni muhimu sana… Serikali inajitahidi, imeleta matreka mengi ya kutosha… tuongeze mengine, tuondoke kwenye jembe la mkono,..haliwezi kututoa kwenye umaskini,”alisema Lowassa na kuongeza:

“Hata wakati wa Nabii Bwana Yesu, watu walishahama kwenye jembe la mkono… unakumbuka ile habari ya mtu aliyealikwa kwenye sherehe akasema ‘mimi nimenunua jozi ya ngombe nakwenda kulijaribu’ walikuwa wameshahama, sisi mpaka leo tuko na jembe la mkono, haiwezekani.”

Kauli hiyo ya Lowassa imekuja wakati kukiwa na malalamiko kutoka kwa wananchi na wadau wa siasa kuitaka Serikali ipunguze matumizi hasa katika ununuzi wa magari ya kifahari na safari za ndani na nje za viongozi wa Serikali.

Amshukia Waziri Membe
Katika hatua nyingine, Lowassa aliilaumu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa , akidai kuwa imekuwa nzito kutoa uamuzi, jambo ambalo limesababisha kudorora kwa balozi nyingi za Tanzania nje ya nchi.

“Wimbo ni mmoja, liturjia inayoimbwa ni moja..Canada kuna tatizo la fedha, Marekani kuna tatizo la fedha, Afrika Kusini kuna tatizo la fedha, liturjia ni moja, kwamba tuna tatizo la fedha, tatizo la kibajeti. Lakini Wizara ya Mambo ya nje imekuwa nzito, kupiga simu na kuwasaidia…,” alisema Lowassa na kuongeza:

“Kwa kweli ni matatizo makubwa sana, kwa mfano unafika mahala mishahara inachelewa kwa miezi sita, miezi mitatu, yule mtu yuko kule hana mjomba hana shangazi anafanyaje? alihoji Lowassa.
Alisema athari za ukosefu wa fedha kwenye balozi hizo zimejidhihirisha kwenye maeneo mengi ikiwa ni pamoja na kupunguza morali ya wafanyakazi.

Lowassa alitoa mfano akieleza Serikali imeshindwa kuikarabati nyumba iliyonunuliwa Washington  kwa Dola za Marekani 100 Milioni, akisema kama ingekarabatiwa na kupangishwa, ingeingiza Dola za Marekani 400,000 kwa mwezi.

Alisema hata jengo la ubalozi lililopo Canada limechakaa, lakini imechukua miezi sita kufanya uamuzi wa ukarabati  tangu watumishi walipoomba balozi ahamie hotelini kufanyia kazi zake.

“Kwa hiyo kuna matatizo ya kifedha, lakini kuna maamuzi tu wa kuchelewa pale wizarani. Tumeyazungumza kwenye kamati yetu, bungeni. Spika amekubali kwamba halikupata mjadala mzuri hivyo tutatafuta muda mwingine ikiwezekana tutawaita mabalozi wote,”
Alishauri pia kuboreshwa kwa sheria za nchi ili kuwezesha mashirika ya fedha na ujenzi kujenga majengo ya balozi nje ya nchi.

“Kwa mfano tusitegemee kujenga nyumba kwa fedha za bajeti, tunaweza kutumia mashirika kama NSSF (Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii), jengo lile likishajengwa linapangishwa… Hilo haliruhusiwi kwenye sheria zetu… Kuna haja ya kuziangalia sheria zetu ili zituwezeshe kununua nyumba, kuuza nyumba na kujenga nyumba zetu.

Kuhusu ukimya
Awali Lowassa alibainisha siri yake ya kukaa kimya akisema kuwa ni hekima kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kusisitiza kuwa sasa hali yake ya kiafya imeimarika.

“Ukimya ni hekima kutoka kwa Mwenyezi Mungu nimetumia nafasi hiyo kuwaacha Watanzania wengine waendelee na kazi badala ya kuwakatisha tamaa,”alisema na kuongeza:

“Kinachonishangaza ni ‘speed’ ya kuandika uongo, tatizo ni kutakiana  ubaya kuandika ubaya. Nataka kuwahakikishia Watanzania kuwa afya yangu ni nzuri ninamshukuru Mwenyezi Mungu,” alisema.

Huku akizungumzia mgogoro kati ya Malawi na Tanzania, alionyesha kukerwa na siasa za chuki, akisema kuna baadhi ya waandishi wa habari wanaotumiwa na wanasiasa wanaomchukia kupotosha habari zake kuhusu mgogoro huo.

“Kwa mfano juzi nilizungumza habari ya uamuzi wa kamati yetu kuunga mkono kauli ya Serikali kuhusu suala la Malawi. Lakini kauli ile imepotoshwa, Lowassa ametangaza vita amekuwa amiri jeshi mkuu, ile ni uongo na hakuna ukweli wowote,”alisema na kuongeza:

“Tunajua Watanzania hawapendi vita, lakini tushirikiane, tuzungumze, tuzungumze, tuzungumze, hadi tufikie mahali pazuri. Nilizungumza mfano wa Wakatoliki wanapokuwa wanamchagua Kiongozi wao Mkuu Papa hukaa ndani wakaomba na kusali mpaka moshi utoke. Sasa na sisi mawaziri hawa wa Mambo ya Nje waliokutana wazungumze mpaka amani ipatikane,”

No comments:

Post a Comment