KADA
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Maliki Marupu kutoka wilayani Ulanga, mkoani
Morogoro, ametangaza nia kuwania nafasi ya uenyekiti wa CCM taifa,
inayoshikiliwa na Rais Jakaya Kikwete.
Marupu
ambaye amejitambulisha kuwa ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM Taifa, alisema kuwa
amefikia hatua hiyo ili kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho tawala.
Wiki
iliyopita, gazeti hili liliripoti taarifa za kuwapo kundi linalompinga Rais
Kikwete kutaka kutenganisha kofia ili asiendelee kuwa Mwenyekiti wa CCM taifa,
na kumpa nafasi ya kubaki kwenye kiti cha urais.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Marupu alisema kama fomu za
kuwania nafasi hiyo zitatolewa, ataandika historia mpya ndani ya chama hicho.
Hata
hivyo, chini ya utaratibu wa sasa wa CCM, nafasi ya mwenyekiti taifa
haigombewi, bali jina la mgombea ambaye kwa kawaida huwa ni Rais wa Muungano
huteuliwa na Kamati Kuu (CC), kuthibitishwa na Halmashauri Kuu (NEC) na
hatimaye kupigiwa kura na wajumbe wa mkutano mkuu.
Huku
akinukuu Katiba ya CCM, alisema ibara ya 14 kifungu kidogo cha 3, kinampa
nafasi mwanachama yeyote ndani ya chama hicho kuwania nafasi katika ngazi
yoyote.
“Unajua
lazima tuwe wazi. Kinachoogopwa hapa ni kama ikitokea mwenyekiti akawa sio
rais, iwapo patatokea kutoelewana kati yao, basi mwenyekiti wa chama ana uwezo
wa kushawishi wanachama wakamvua madaraka rais,” alisema.
Marupu
alisema, utaratibu unaotumika wa kumpata mwenyekiti, umekuwa ukidumaza
demokrasia ndani ya chama hicho.
Kada
huyo alisema, wapo watakaomuona msaliti ndani ya chama, lakini amelazimika
kuwania kiti hicho kuleta mabadiliko yanayoenda na wakati.
“Wajumbe
wakinipitisha, mchuano wangu na Kikwete utakuwa kama ule uliowahi kutokea
nchini Afrika Kusini kati ya aliyekuwa rais, Thabo Mbeki na rais wa sasa Jacob
Zuma aliyeibuka mshindi,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment