ASEMA ANA UWEZO,
UADILIFU KUWA AMIRI JESHI MKUU
HARAKATI
za kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015 umeanza kuwatesa
viongozi wa vyama vya siasa ambapo safari hii, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA
(Bara), Zitto Kabwe, amesema kama akiandikiwa kuwa rais hakuna wa kumzuia.
Zitto
ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alijitapa kuwa kama urais upo, utakuja
tu, kwani ana uwezo, uadilifu na uzalendo wa kuwa Amiri Jeshi Mkuu.
Zitto
ameibuka na kuzungumzia sakata la urais ikiwa ni siku moja tu imepita baada ya
wabunge wenzake kulalamika na kukanusha taarifa za kumpigia debe kwa ajili ya
urais mwaka 2015.
Wabunge
hao, Halima Mdee (Kawe) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), waliandika barua
za kulalamikia habari iliyochapishwa na gazeti moja la kila siku (si Tanzania
Daima), wakidai liliwalisha maneno kuwa walimpigia debe Zitto wakiwa mkoani
Kigoma kwamba anapaswa kuwa rais mwaka 2015.
Akichangia
mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya
Mawasilaino, Sayansi na Teknolojia jana mjini hapa, Zitto alitumia muda mfupi
kufafanua sakata hilo lililozagaa kwenye vyombo kadhaa vya habari na kwenye
mitandao ya kijamii.
“Tamasha
letu la wasanii la Kigoma limeleta maneno maneno…lakini napenda kusema kuwa
urais kama upo utakuja tu. Sina mashaka hata kidogo kwamba uwezo, uadilifu na
uzalendo wa kuwa Amiri Jeshi Mkuu ninao,” alisema Zitto na kushangiliwa na
wabunge wenzake.
Mjadala
huo ulichukua sura mpya kwenye mitandao ya kijamii juzi ambapo baadhi ya watu
walionekana kumlaumu Zitto, wakimhusisha na habari hiyo kuwa aliitengeneza
mwenyewe kama sehemu ya kujiandalia mazingira hayo.
Zitto
ambaye amekuwa akiandamwa mara kadhaa na wanasiasa ndani na nje ya chama chake,
baadhi wakimtuhumu kuwa mamluki na wengine wakimwelezea kuwa ni mwanasiasa
mwenye malengo makubwa hapo baadaye, alifafanua zaidi suala hilo kwenye taarifa
yake kwa kusema:
“Katika
gazeti la Mwananchi la tarehe 23 Julai 2012, kulikuwa na habari yenye kusomeka:
‘Wabunge wamsafishia Zitto njia ya urais 2015?. Habari hii imeleta mjadala mara
baada ya kutoka na kusomwa. Mjadala umekuzwa zaidi baada ya wabunge, Halima
Mdee na Joshua Nassari kukanusha maneno waliyonukuliwa kusema. Napenda kusema
masuala yafuatayo:
“Moja,
waheshimiwa wabunge Halima Mdee, Joshua Nassari, Kangi Lugola, Esther Bulaya,
Deo Filikunjombe, Raya Ibrahim, Amina Mwidau na David Kafulila walihudhuria
tamasha la vijana wa Kigoma All Stars kwa kualikwa na Mratibu wa kundi hilo,
Mwasiti Almasi.
“Wabunge
wengine walialikwa lakini hawakutokea wakiwamo Joseph Mbilinyi, David Silinde,
Amos Makala, Vicky Kamata na Peter Serukamba. Wabunge hawa hawakualikwa na mimi
na wala sikufanya mazungumzo nao yoyote ya awali au kuwaambia au kukubaliana
nini cha kuzungumza au hapana. Tamasha lilikuwa la muziki na halikuhusika
kabisa na siasa.
“Waheshimiwa
wote walipewa nafasi ya kusalimia na wote walizungumza. Wabunge waliozungumza
kwa muda mrefu kidogo ni ndugu Halima Mdee, Joshua Nassari, Deo Filikunjombe na
Kangi Lugola.
“Hotuba
za wabunge wote zilirekodiwa kwenye video neno kwa neno na video hizo zitawekwa
wazi kwenye blogu yangu kama sehemu ya documentary ya tamasha lile la
kihistoria.
“Pili,
sikuhusika kwa namna yoyote ile na kuandikwa kwa habari hii iliyozusha mjadala.
Wala sikujua kama habari hii ingeandikwa, maana katika ziara ile sikuita
mwandishi hata mmoja, maana nilitaka liwe tukio la Kigoma tu.
“Kama
mwandishi kaandika mambo ambayo wabunge hawa hawakuyasema basi itaonekana
kwenye video hizo. Wabunge wenyewe wanajua kwenye nafsi zao nini walichosema
Kigoma na kipi kiliwasukuma kusema waliyoyasema. Nisingependa kuhusishwa kwa
njia yoyote ile na matamshi yao, habari iliyowanukuu na hata makanusho yao.
Maana mwisho wa siku ukweli ndio utasimama.
“Suala
la urais lisitupotezee muda kwani kuna mambo mengi sana ya kujadili kuhusu nchi
yetu. Taharuki ambazo watu wanazipata masuala ya urais yanapotajwa zinashangaza
sana.
“Chama
changu bado hakijatangaza rasmi mchakato wa kupata mgombea urais. Hivi sasa
chama hakina mgombea urais mpaka hapo mchakato utakapotangazwa, ambapo
wanachama wataruhusiwa kuomba kupeperusha bendera ya chama. Mwanachama wa chama
chetu atakaye kubalika na jamii na wajumbe wa mkutano wa uteuzi ndiye atakuwa
mgombea wetu. Kwa sasa hayupo na hivyo tusipoteze muda kujadili jambo hili.
“Mzee
Thabiti Kombo alituachia usia tunapokuwa tunazungumza. Alisema ‘weka akiba’ si
akiba ya fedha, bali ya akiba ya maneno. Tuweke akiba ya maneno. Tusimalize
yote.”
Hata
hivyo akizungumza na gazeti hili mjini hapa jana mara baada ya Bunge
kuahirishwa kwa ajili ya mapumziko ya mchana, Zitto alikanusha tuhuma hizo
zinazomhusisha kuandaa habari hiyo akisema ni matusi kwa tasnia ya habari,
hivyo kuvitaka vyombo vya habari kutowaendekeza wanasiasa wanaotukana waandishi
na vyombo vyao.
“Ni
upuuzi kudhani kwamba mimi naweza kuandaa habari kwenye gazeti hilo…nimeshangaa
na wewe unaweza kuniuliza jambo hili…unaliamini?” alihoji Zitto.
Kuhusu
habari hiyo inayolalamikiwa na wabunge wenzake kuwa ilipotoshwa, alisema kwamba
haoni ubaya kwenye habari husika akidai hata hivyo mengi yaliachwa kuliko
kuongezwa chumvi. “Hakuna aliyenukuliwa kwa ambalo hakusema. Tamasha zima
limerekodiwa kwenye video”.
Kwa
muda sasa kumekuwepo na mjadala juu za Zitto kuhusu kauli yake kwamba anautaka
urais, jambo liliotafsiriwa kuwa ni mikakati ya kutaka kukivuruga chama chake
kwa kikigawa kimakundi lakini Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa,
amekuwa akisema kila wakati kuwa ajenda yao kwa wakati huu si kujadili nani
anafaa kugombea urais 2015 badala yake wanajikita kutatua kero za wananchi.
No comments:
Post a Comment