CHAMA
Cha Walimu Tanzania (CWT) kiliitisha mgomo kwa walimu wote nchini kuanzia
Jumatatu tarehe 30 Julai 2012 mpaka kitakapowajulisha vinginevyo. CWT kinaona
mgomo ndio njia sahihi itakayoishinikiza Serikali kutekeleza madai ya walimu na
kuwaboreshea mazingira ya kazi walimu. Mgomo huu leo unafikisha siku ya nne
mfululizo.
HakiElimu inatambua kuwa walimu wamekuwa na mgomo baridi kwa muda mrefu sasa. Utafiti uliofanywa na HakiElimu mwaka jana ulibaini kuwa asilimia 40.6 tu ya walimu katika sampuli ya utafiti ndio walioonesha nia ya kuendelea kuwa walimu, wakisema mazingira magumu na maslahi duni ndio sababu kubwa za kuwavunja moyo.
Uthibitisho
mwingine wa kuwepo kwa mgomo baridi unatokana na kushuka kwa ufaulu wa
wanafunzi katika mitihani ya Taifa. Kwa mfano katika shule za msingi, takribani
nusu ya wanafunzi wamekuwa hawafaulu kwa miaka 3 sasa; huku mwaka 2011 pekee
ukiwa na asilimia 46.5 ya watahiniwa waliofeli mitihani yao ya darasa la saba;
na kwa sekondari wanafunzi takribani asilimia 90 walipata daraja la nne na
sifuri.
Hali hii pia inadhihirishwa zaidi na uwepo wa wanafunzi zaidi ya 5,000 mwaka huu nchini walioandikishwa kujiunga na masomo ya sekondari kutokujua kusoma na kuandika.
Pia
ripoti ya utafiti uliofanywa kwa niaba ya African Economic Research Consortium
na Benki ya Dunia mwaka 2011 inaonesha kwamba walimu wa shule za msingi
Tanzania wanafundisha kwa wastani wa masaa mawili na dakika nne tu kwa siku; kati
ya masaa 5 na dakika 12 yaliyo katika ratiba ya siku moja.
Mambo haya yote yanadhihirisha kuwa mgomo baridi wa walimu umeendelea kuwepo,
na kuwaathiri zaidi wanafunzi. Wanafunzi hawawezi kujifunza bila walimu; na
walimu bila kufundisha kwa moyo, wanafunzi hawawezi kujifunza kwa ukamilifu.
Ni dhahiri kuwa mgomo huu wa walimu umekuwa na madhara makubwa kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla. Wanafunzi wanakosa masomo. Hii itachelewesha kumaliza ‘mihtasari’ (syllabuses) ya kufundishia, na kuwaumiza zaidi wale watakaofanya mitihani yao ya Taifa mwaka huu.
Usalama
wa wanafunzi uko hatarini, hasa wanapoamua kwenda shuleni kwa kuhisi kuwa
huenda walimu wao watafundisha kwa siku hiyo. Ni hatari sana wanafunzi kuwepo
shuleni bila walimu. Wanakosa mwongozo wa walimu, na kuishia kurandaranda
maeneo ya shule, ama mitaani.
Pia mgomo huu unajenga mtazamo hasi wa jamii kuhusu kazi ya ualimu. Wanafunzi na wazazi wao wanaendelea kutengeneza tafsiri kuwa kazi ya ualimu ni duni sana, na baadhi ya kauli za serikali kuhusu mgomo huu haziijengei hadhi kazi hii adhimu. HakiElimu pia inaamini kuwa mgomo huu utaligharimu Taifa kwa namna mbalimbali.
Baadhi
ya wanahabari waliusikiliza uongozi wa HakiElimu
Baada
ya kuyatafakari haya, HakiElimu inapendekeza yafuatayo:
1. Kila mwanafunzi ana haki ya kujifunza na kuelimishwa. Hivyo basi, Serikali na Chama Cha Walimu Tanzania wanapaswa kufikia makubaliano haraka kadri inavyowezekana, kwa kuwa waathirika wakubwa wa mgomo sio wao wenyewe, ni wanafunzi.
2. Mgomo huu ushughulikiwe na uishe kabisa. Usiishie kuwaona walimu wamerejea kufundisha, huku wakiwa na kinyongo. Hii italeta mazingira ya kuendeleza mgomo baridi; na madhara yake ni makubwa zaidi.
3. HakiElimu inawakumbusha walimu kuwajibika. Wadai haki zao, huku wakitimiza wajibu wao wa kufundisha na kuendeleza elimu yetu. Wafundishe kwa bidii bila kinyongo, kwa kuwa wasipowajibika watakuwa wanawaumiza wanafunzi na jamii kwa ujumla. Mgogoro uliopo ni baina yao na Serikali, na si wanafunzi.
4.
Kusema serikali haina uwezo wa kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya
watumishi wake; haileti unafuu wa maisha kwa watumishi wa umma. Gharama za
maisha zinazidi kupanda, na mfumuko wa bei nao unawaumiza watumishi kila siku.
Hivyo, Serikali itafute vyanzo mbadala vya mapato. Isitoshe, serikali iweke
malengo, mipango na mikakati ya kuboresha elimu na mazingira ya kufundishia kwa
kuwa ndio njia muafaka na ya haraka ya kuiletea nchi maendeleo.
5. HakiElimu inasisitiza kwamba nchi itafanikiwa kuboresha elimu endapo tu itawekeza kwa walimu kwa kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya walimu, kuwashirikisha walimu katika maamuzi kuhusu masuala ya elimu na kuwapa walimu mafunzo kazini. Elimu bora haiwezi kuletwa na walimu walio hoi!
6. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litenge muda kujadili suala hili kwa kina na kuishauri serikali, hasa kuhusu tahadhari za kuchukua ili tatizo kama hili lisitokee tena. Bunge lina wajibu wa kuishauri na kuisimamia Serikali kuhusu sera, utendaji na usimamizi wa elimu nchini.
Inasikitisha
kwamba Bunge linakwepa kujadili tatizo hili kwa maelezo kwamba liko mahakamani.
Tunaamini kwamba mahakama italiangalia suala hili na kutenda haki, lakini
wajibu wa Bunge uko pale pale.
7. Viongozi wa Serikali wasiwabeze walimu; kwa kufanya hivyo wanawakatisha tamaa. Hata kama baadhi ya walimu hawakusoma kwa miaka mingi kama ilivyo kwa fani nyingine, wana umuhimu mkubwa sana. Ndio wanaowaandaa watanzania wa leo na kesho kimtazamo na kimaarifa. Hivyo, kudai kuboreshewa mazingira ya kazi ni haki yao; na Serikali inaweza kutimiza wajibu wake kwa kuwasikiliza na kushauriana nao bila ubabe na kejeli.
8. Serikali ijijengee utaratibu wa kuboresha mazingira ya watumishi wake, na si kusubiri kwenda mahakamani kuzuia watumishi kugoma. Watumishi wa umma watafanya kazi kwa ari endapo tu wameridhika na mazingira ya kazi na maslahi yao; na si kwa kutumia uamuzi wa mahakama peke yake.
HakiElimu
ni shirika la jamii linalowawezesha wananchi kubadilisha elimu, ndani na nje ya
shule; kuathiri utungaji na utekelezaji madhubuti wa sera; kuchochea majadiliano
ya umma na mabadiliko ya kijamii yenye ubunifu; kufanya utafiti, uchambuzi na
uhamasishaji wa sera, na kushirikiana na wabia ili kuendeleza ushiriki,
uwajibikaji, uwazi na haki za jamii. Shirika linataka kuona Tanzania inaongeza
uwazi, haki na demokrasia kwa kuwapa watu wote fursa ya kupata elimu
inayochochea usawa,ubunifu na fikra tunduizi.
Elizabeth
Missokia Mkurugenzi Mtendaji
No comments:
Post a Comment