KUNDI LAIBUKA KUTAKA AACHIE CHAMA,
ABAKI NA URAIS
WAKATI uchaguzi ndani ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya taifa ukikaribia, kundi linalopigania mabadiliko
kutaka kutenganisha kofia ya urais na uenyekiti limeibuka upya kutaka
mabadiliko hayo. Hoja hiyo imeibuka sasa wakati
zimebaki siku saba kabla ya CCM kuanza kutoa fomu za kuwania uongozi ngazi ya
taifa.
Mtandao wa kundi hili pana
unaunganisha baadhi ya vigogo wa CCM, wakiwamo wenyeviti na makatibu wa mikoa
na wilaya na makada maarufu ambao hujulikana kama majeruhi wa kisiasa
waliotokana na makundi yenye uhasama ndani ya chama hicho tawala.
Kundi la mlengo huo wa
mabadiliko hayo linataka Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa chama
hicho taifa, aachie nafasi ya uenyekiti ili abaki kuwa rais, kumalizia muda
wake. Hata hivyo, kwa mujibu wa
Katiba ya CCM ya sasa, nafasi ya mwenyekiti na makamu wake hazigombewi, bali
hutokana na uteuzi wa Kamati Kuu (CC) ambayo chini ya utaratibu wa sasa, rais
ndiye anayekuwa mwenyekiti wa chama taifa.
Muundo huo wa uongozi
uliasisiwa na Mwalimu Nyerere wakati ule, kwa hofu kwamba kama rais na
mwenyekiti wanakuwa watu tofauti, ikitokea kwamba hawaelewani, nchi
haitatawalika. Sababu kubwa inayotajwa na
kundi linalotaka mabadiliko hayo, ni kutaka kumpunguzia majukumu rais ili abaki
kuiongoza serikali na shughuli za chama zisimamiwe na mtu mwingine, ambaye
atakuwa na nafasi ya kutosha kukisimamia na kukiendesha.
“Baadhi ya wana CCM wanatuelewa
vibaya kwamba tunataka kufanya uasi ndani ya chama, hapana. Huu ni muundo mzuri
unaotumika katika nchi nyingi duniani, na mfano ni Afrika Kusini. Lengo letu
tunataka kumpunguzia rais majukumu na chama kibaki na mtu mwingine,” alisema
mmoja wa vigogo wa mkakati huo.
Uchukuaji wa fomu kuwania
nafasi za uongozi wa CCM taifa, unatarajiwa kuanza Agosti 22 hadi 28. Akizungumzia tishio la kutaka
kumng’oa Rais Kikwete, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema
kundi hilo linajidanganya kwani mkakati huo hauwezekani kwa sasa.
“Ni kweli tunajua kuna presha
hiyo. Lakini ni mambo ya kushangaza, kwa sababu nafasi ya mwenyekiti na makamu
hazigombewi, hao wanaotaka mtu mwingine agombee nafasi hiyo hizo fomu anazipata
wapi na nani atakayempa?” alihoji Nape.
Alisema fomu za ngazi ya taifa
zitakazotolewa kuanzia Agosti 22, zinahusu wajumbe wa halmashauri kuu pekee na
si nafasi ya mwenyekiti wala makamu wake. “Kwa kawaida nafasi ya
mwenyekiti na makamu wake inapendekezwa na Kamati Kuu na kisha majina yao
yanathibitishwa na NEC. Na hata kwenye kuomba kura, anaombewa na wajumbe wa Kamati
Kuu,” alisema Nape.
Kwa mujibu wa Nape, kundi
linalotaka mabadiliko hayo kwanza lijitokeze na kisha lilete hoja hiyo katika
utaratibu unaopaswa, na si kujificha na kutaka kufanya uhaini, jambo ambalo
halikubaliki ndani ya chama.
No comments:
Post a Comment