ATAKA
WALIOWEKA FEDHA NJE WATAJWE
MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), ameitaka Mamlaka ya Manunuzi ya
Umma (PPRA), kufanya uchunguzi wa manunuzi ya mafuta ya kuzalisha umeme ambayo
yanagharimu sh bilioni 42 za serikali kila mwezi.
Zitto
ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Fedha,
alisema kuwa sakata la mjadala wa ununuzi wa rada haliwezi kuisha kwa kufurahia
chenji iliyorudishwa kwani bado taifa linahitaji kujua ukweli.
Akiwasilisha
maoni ya kambi hiyo mjini hapa jana, Zitto alisema manunuzi ya mafuta yamejaa
mizengwe ya ufisadi uliokithiri, na kwamba licha ya kutaka Spika kuunda tume ya
kuchunguza ufisadi huo na Kamati ya Bunge kutaka uchunguzi wa kibunge
kufanyika, hakuna hatua zilizochukuliwa.
“PPRA
haipaswi kufumbia macho manunuzi yanayotafuna sh bilioni 1.4 kila siku, na
yanayoongeza manunuzi ya nchi kutoka nje, hivyo kupoteza fedha za kigeni
hovyo,” alisema.
Aliongeza
kuwa, Wizara ya Fedha ambayo ndiyo wizara mama ya PPRA ambayo pia inasimamia uchumi
wa nchi, inapaswa kuleta bungeni taarifa ya uchunguzi utakaofanywa na PPRA
kuhusu manunuzi hayo.
“Takwimu
zinaonyesha kuwa serikali inapaswa kutumia zaidi ya sh 42 bilioni kila mwezi
kuendesha mitambo ya dharura ya umeme. Manunuzi yenyewe ya mafuta yamejaa
mazonge ya ufisadi uliokithiri. Kambi ya upinzani inataka uchunguzi wa kina
kuhusu manunuzi ya mafuta kuzalisha umeme, ambayo yanachoma bilioni 42 za
serikali kila mwezi,” alisema.
Kuhusu
sakata la ununuzi wa rada, Zitto, alisema mjadala huo bado ni mbichi, kwani
unahitajika ukweli kuwa taifa lilipata hasara kiasi gani pamoja na hatua
stahiki kuchukuliwa dhidi ya wote walioingiza hasara kwa taifa.
Alisema
sehemu ya malipo ya deni la taifa ni mkopo wa serikali iliyochukua kununua rada
kutoka Kampuni ya BAE ya Uingereza na kuongeza kuwa, suala hilo limejadiliwa
kwa upande mmoja wa ufisadi wa kupandisha bei na hatimaye kurejeshwa kwa chenji
hiyo.
Zitto,
alisema kuwa hiyo ilikuwa nusu ya ukweli kuhusu suala la rada, kwani serikali
ilikopa dola milioni 40 kutoka Benki ya Barclays ya Uingereza kwa ajili ya
kununua rada hiyo.
“Mkopo
huo ulikuwa na riba ya asilimia 4.9 juu ya kiwango cha riba zinazotolewa na
Benki ya Dunia au IMF. Kambi rasmi ya upinzani inataka kujua kama mkopo huo
umeshalipwa, na jumla tulilipa kiasi gani. Na chenji ya rada ilikuwa na thamani
yoyote kifedha?” alihoji.
Zitto
pia aligusia suala la udhibiti wa fedha haramu, akisema kambi hiyo imepata
taarifa kuwa mmoja wa viongozi wa juu nchini na baadhi ya mawaziri wa serikali
za awamu zilizopita, ni miongoni mwa wamiliki wa fedha hizo zipatazo sh bilioni
314.5.
Alisema
sehemu kubwa ya fedha hizo zililipwa kampuni ya utafutaji mafuta wa gesi katika
Pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.
“Tunaitaka
serikali kutoa taarifa rasmi ya hatua gani imechukua baada ya taarifa hiyo
kutoka Benki ya Taifa ya Uswisi ilipotolewa. Tunataka kuliambia taifa hatua
itakazochukua kurejesha fedha hizi na nyingine zozote ambazo zimefichwa
ughaibuni. Kambi ya upinzani italazimika kuweka wazi taarifa na majina ya watu
wenye umiliki wa fedha katika benki ya Uswisi iwapo serikai haitatoa taarifa
rasmi kuhusu suala hili,” alisema.
Hata
hivyo msimamo huo wa Zitto, ulimwibua Mbunge wa Simanjiro, Christpher ole
Sendeka (CCM), aliyeomba mwongozo na kumtaka Zitto awataje kwa majina viongozi
hao, kwani kuacha hivyo ni kuharibu taswira ya serikali na Bunge.
Mnadhimu
Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lisu, aliingilia kati akisema Sendeka
hakupaswa kumkatisha Zitto wakati akizungumza na kusema kuwa iwapo ana wasiwasi
na kauli hiyo kwa mujibu wa kanuni anapaswa kuthibitisha maelezo anayoyaona
hayana ukweli kabla ya mtoa kauli kuthibitisha.
Aidha,
Zitto alisema kuna taarifa nyingine zinazoonesha jinsi taifa linavyoibiwa
kupitia kesi mbalimbali ambazo serikali imeshitaki au kushitakiwa kwenye
mahakama za kimataifa.
Alitoa
mfano wa kesi hizo ni ya IPTL na Standard Chartered Bank ya Hong Kong ambayo
imechukua muda mrefu bila kuisha na kuliingiza taifa katika hasara kubwa.
Kuhusu
deni la taifa, Zitto alitaka ufanyike ukaguzi maalumu, ili kubaini uhalali wa
deni hilo ambalo hadi Juni mwaka huu lilifikia dola milioni 10,354.6.
Alisema
ukaguzi ukifanyika, utawezesha kujulikana kama miradi ilitekelezwa kama
inavyotakiwa au kuna mazingira yenye utata.
Kuhusu
mishahara hewa, Zitto alisema watumishi hewa 9,949 ni wengi na kwamba inaonesha
ni jinsi gani serikaki haipo makini katika suala hilo.
Aliitaka
serikali kutumia fedha wanazolipwa watumishi hewa kuwalipa walimu na madaktari
kwani ni nyingi.
“Siku
zote sababu za serikali kutotimiza matakwa ya wafanyakazi katika sekta ya afya
na elimu ni kwamba haina fedha. Lakini tunashuhudia sh bilioni 70 kila mwaka
zikielekezwa kuwalipa watumishi hewa,” alisema.
Kwa
upande wa mashirika ya umma, alisema kambi hiyo inataka kupata maelezo kuhusu
sakata la uuzwaji wa hisa za shirika la UDA pamoja na kuhoji serikali imefikia
wapi katika pendekezo la kulifanyia marekebisho Shirika Hodhi la Mashirika ya
Umma (CHC), ili liweze kumiliki, kusimamia na kuziendesha hisa za serikali
katika kampuni binafsi ambao umiliki wa serikali ni chini ya asilimia 50.
Akisoma
maoni ya Kamati ya Fedha na Uchumi, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dustan
Kitandula (CCM), alisema kuna haja serikali ikadhibiti deni la taifa kabla
halijaongezeka zaidi.
Kitandula
ambaye ni mbunge wa Mkinga, alisema kuwa serikali inapaswa kuchukua hatua za
kinidhamu dhidi ya watumishi wake waliohusika katika ubadhirifu wa ulipaji
mishahara hewa.
No comments:
Post a Comment