To Chat with me click here

Wednesday, August 29, 2012

IGP MWEMA AMWANGUKIA DK. SLAA

POLISI WAUNDA TUME KUCHUNGUZA MAUAJI YALIYOTOKEA MORO

WAKATI serikali imeunda tume kuchunguza mauaji yaliyotokea juzi mjini Morogoro baada ya polisi kuwashambulia wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema amemwomba Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa kusitisha maandamano na mikutano ya hadhara ya Movement For Change (M4C), kwa siku tano kupisha zoezi la sensa.

Dk. Slaa aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, chama chake kimetafakari na kukubali kusitisha mikutano yake ambayo jana ilipaswa kufanyika mjini Iringa.

Alisema jana CHADEMA ilipanga kufanya mkutano wake wa kwanza mjini Iringa katika viwanja vya Mwembetogwa na tayari walishapata kibali cha polisi mkoani humo kufanya maandamano wakiwa ndani ya magari.
“Lakini ilipofika majira ya saa 3 usiku juzi, tulipata simu kutoka kwa mkuu wa polisi kwamba maandamano yetu yamesitishwa na kutengua mambo yote tuliyoafikiana nao.

“Asubuhi ya leo (jana), tulipigiwa simu na RPC na kutueleza kuwa wanataka kuonana na viongozi wa CHADEMA, huku wakiwa na hoja ya kutaka tuahirishe kufanya mikutano kutokana na sensa na hoja nyingine ni kwamba wananchi wa Iringa watakuwa wameathirika na kifo cha kijana aliyeuawa Morogoro,” alisema Dk. Slaa.

Alisema baada ya kutokubaliana na hoja zote za polisi, alipigiwa simu na IGP Mwema akimwomba Dk. Slaa kusitisha mikutano na maandamano kwa siku tano mkoani Iringa na kwamba vyama vyote vya siasa havitaruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara katika kipindi hiki cha sensa.

“IGP nimeongea naye leo kwa dakika 40 akiniomba kwa kuniita…, ‘Dk. Slaa sijawahi kukuomba hata siku moja naomba nikuombe na usinikatalie kwamba ndani ya siku tano kuanzia leo, tumezuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara kutokana na zoezi la sensa na wewe na chama chako tunawaomba msitishe mikutano yenu’,” alisema Dk. Slaa akimnukuu IGP Mwema.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, CHADEMA imekubaliana na ombi la IGP Mwema kusitisha mikutano yao ya hadhara, lakini wataendelea na ratiba ya mikutano ya ndani wakiwa mjini Iringa.

Alilitaka Jeshi la Polisi baada ya kumalizika kwa sensa, wasije na visingizio vingine vya kusimamisha mikutano yao kwani hawatakubali kusikia masharti mengine.
“Sisi CHADEMA tunawapa polisi nafasi ya mwisho na nchi hii inaongozwa na sheria. Nataka dunia nzima ifahamu na kujua kuwa kufanya maandamano ni haki ya kikatiba kwa kila mwananchi,” alisema.

Wakati polisi wakisitisha mikutano na maandamano, mapokezi ya msafara wa CHADEMA uliowasili mkoani Iringa jana, uliwashitua polisi ambao walikuwa na wakati mgumu kuweka doria na askari wenye silaha kila kona.

Katika hatua nyingine, CHADEMA imetangaza kushiriki mazishi ya marehemu Ally Nzona (38), aliyefariki dunia kwa kupigwa risasi kichwani na polisi mkoani Morogoro.
Alisema CHADEMA kitashiriki katika mazishi ya kijana huyo na kugharamia shughuli zote za mazishi bila kujali kama alikuwa mwanachama wa CHADEMA au la.

“Kama familia yake itaamua kusoma dua hapa Morogoro na kumzika hapa, tutashiriki kikamilifu, tumejadiliana na wanafamilia kuna mambo ya msingi tumekubaliana na walichoomba ni kusaidia kusafirisha mwili,” alisema Dk. Slaa.

Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Faustine Shilogile alisema polisi wanaendelea na uchunguzi kwani hadi sasa haijulikani endapo kijana huyo alifariki dunia kwa kupigwa bomu, risasi au ajali.

Kifo cha kijana huyo kilitokea juzi katika eneo la Msamvu, Manispaa ya Morogoro ambapo wafuasi wa CHADEMA walikuwa wakiandamana kuwapokea viongozi wao wa kitaifa kwa ajili ya mkutano wa hadhara.
Wakati huo huo, serikali imeunda tume kuchunguza kifo cha kijana huyo.
Hatua hiyo ilitangazwa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mazingira ya vurugu hizo.

Dk. Nchimbi alisema jopo la tume hiyo ambalo hakulitaja, litafanya uchunguzi kubaini chanzo cha mazingira ya kifo hicho.
“Polisi walikuta mtu mwenye majeraha mwilini ambaye baada ya kufikishwa hospitalini, alifariki dunia. Polisi Makao Makuu wameunda jopo kuchunguza ili kupata ukweli wa kile kilichosababisha kifo cha mtu huyo,” alisema Dk. Nchimbi.

Bila kutaja majina na idadi ya wajumbe waliomo kwenye jopo hilo na muda gani wataifanya kazi hiyo, Dk. Nchimbi alisema baada ya uchunguzi ndipo ukweli juu ya kile kilichosababisha kifo cha mtu huyo utajulikana.
Nzona alidaiwa kupigwa risasi kando ya meza ya magazeti.

Mbali ya kifo cha Nzona aliyeripotiwa kuwa ni mpiga debe katika mabasi ya Msamvu, Frank Mbalimba na Hashim Seif walijeruhiwa wakati polisi walipotumia nguvu kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA.
Dk. Nchimbi alisema polisi walizuia maandamano hayo ili kupisha zoezi la sensa kwani yangeleta usumbufu.

Waziri huyo aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuheshimu sheria za nchi na kuongeza kuwa, kama mtu anahisi ameonewa afuate utaratibu kuwasilisha madai yake na sio kutumia nguvu.

No comments:

Post a Comment