To Chat with me click here

Tuesday, August 14, 2012

BODI YA MIKOPO YAONGEZEWA BAJETI

Serikali imetangaza neema kwa wanafunzi wa elimu ya juu baada ya kuongeza fedha za mikopo kutoka Sh. 91,722,783,264 za mwaka jana hadi Sh. bilioni 306 mwaka huu, lakini ikishindwa kuzungumzia hatma ya madai ya walimu.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2012/13.

Alisema fedha hizo zitatoka kwenye fungu la matumizi mengineyo, ambalo limetengewa Sh. 329,962,472,935.

Dk. Kawambwa alisema kiasi cha fedha kilichotengwa kitawanufaisha wanafunzi 98,772 wa elimu ya juu kutoka wanafunzi 93,176 wa mwaka 2011/12.

Hata hivyo, alisema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HLSLB) itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuchangia elimu, kusimamia urejeshwaji wa mikopo ya Sh. bilioni 18 pamoja na kuanza mchakato wa ujenzi wa ofisi ya bodi hiyo.

Akizungumzia Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), alisema litaendesha na kusimamia mitihani ya wanafunzi 1,050,000 wanaotarajiwa kuhitimu elimu ya msingi mwaka huu na pia ile ya kidato cha nne, maarifa, kidato cha sita na ualimu.

Dk. Kawambwa alisema idadi ya shule za msingi nchini imeongezeka kutoka 15,816 mwaka 2010 hadi 16,331 mwaka jana wakati uandikishaji wa watoto wanaojiunga na elimu ya awali ukiongezeka kutoka 925,465 hadi 1,034,729 mwaka jana.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu imeendelea kuboresha mazingira ya kufundishia kwa kuongeza idadi ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi kutoka 934 mwaka 2010 hadi 1,097 mwaka 2012," alisema.

Alisema kiwango cha kufaulu katika ngazi ya elimu ya msingi kimeongezeka kutoka asilimia 53.5 mwaka 2010 hadi asilimia 58.3 mwaka jana, huku idadi ya walimu wa shule za msingi ikiongezeka hadi 180,987 mwaka huu kutoka 165,856 mwaka juzi.

Alisema pamoja na mambo mengine, katika mwaka huu wa fedha, wizara yake inatarajia kujenga vyuo vinne vya mafunzo ya ufundi katika mikoa minne na vinne vya wilaya.

Wakati Waziri Kawambwa akieleza hayo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, zimeitaka serikali kurejea kwenye meza ya mazungumzo na walimu ili kumaliza mgogoro wa kimaslahi uliosababisha mgomo wa walimu nchini.

Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Suzan Lyimo, alisema inasikitisha kuona serikali ikitoa takwimu za kupanda kwa kiwango cha kufaulu wakati utafiti unaonyesha kwamba, wanafunzi 5,200 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka jana hawajui kusoma wala kuandika.

Alisema hayo yanatokana na maelekezo yanayotolewa kwa wakuu wa shule za kuwataka wafaulishe wanafunzi ilhali shule hazina walimu wala vitendeakazi vya kutosha.

Lyimo alisema hali ya elimu inaendelea kudorora ikilinganishwa na miaka ya nyuma na kushauri kuwa elimu ya msingi iwe kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne na iwe ya lazima.

Kuhusu mgogoro wa walimu, alisema serikali imetumia nguvu na vitisho kushughulikia madai ya walimu kama njia ya kuwanyamazisha badala ya kuwasikiliza.

Alisema hata kama madai ya walimu hayakuwa yanalipika, serikali ingefanya mazungumzo na kada hiyo ili kuona uwezekano wa kuongeza kiasi fulani kwa uwezo wake badala ya kuyakataa kabisa.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Huduma za Jamii, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Martha Mlata, alisema serikali inapaswa kuzungumza na walimu ili kumaliza kabisa mgogoro huo.

“Kamati inasisitiza kwamba, CWT na serikali waendeleze majadiliano kwa kufuata sheria za kazi. Serikali ihakikishe kwamba, vyombo vya majadiliano vinafanya kazi yake ipasavyo,” alisema.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment