WAAMUA KUKATA RUFAA,
SITTA ATAKA WAJIPANGE UPYA
WAKATI
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikitangaza kusudio lake la kukata rufaa dhidi ya
hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, iliyotengua ubunge wa aliyekuwa Mbunge
wa Igunga, Dk. Dalali Kafumu, wadau mbalimbali wameipongeza hukumu hiyo wakiita
ni darasa tosha kwa demokrasia ya mfumo wa vyama vingi.
Miongoni
mwa waliosifu hukumu hiyo ni pamoja na Spika mstaafu, ambaye pia ni Waziri wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akisema kuwa maamuzi hayo inafaa
yaheshimiwe. Akizungumza
jana mjini Tabora, Sitta alisema kuwa mahakama ina mamlaka yake kisheria, hivyo
wana CCM hawana budi kuyaheshimu maamuzi hayo kwani imefanya kazi yake
inavyotakiwa.
“Kama
kuna mtu anaona hukumu hiyo haikutenda haki, anaweza kwenda mahakamani kukata
rufaa, lakini mimi nashauri ni vema tujipange upya tuingie ulingoni.
“Hapa
mimi sina maoni juu ya jambo hilo, bali cha msingi ni vema tukakaa na
kutafakari yaliyotokea huko Igunga, ili basi tukiona inafaa kukata rufaa sawa,
na kama tuingie ulingoni, yote ni sawa,” alisisitiza Sitta.
Katika
hukumu yake juzi, Jaji Mary Nsimbo Shangali, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo,
iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa CHADEMA, Joseph Kashindye,
alisema kuwa alipokea malalamiko 15 ambayo yaliridhiwa na pande zote mbili,
lakini yakaongezwa madai mengine mawili na kufikia 17.
Mbali
na Dk. Kafumu, washitakiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na
Msimamizi wa uchaguzi jimboni humo, Protace Magayane na kwamba mahakama hiyo
ilithibitisha madai saba ya kutengua matokeo hayo.
Hata
hivyo, wakati Sitta akiwa na mtazamo huo, CCM kupitia kwa Katibu wake wa
Halmashauri Kuu (NEC) Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ilieleza
kutoridhishwa na hukumu hiyo, hivyo kuamua kukata rufaa.
Pamoja
na CCM kuchukua hatua hiyo, wadau mbalimbali wa masuala ya kisiasa na
wanaharakati walisema kuwa, hukumu hiyo ni darasa tosha la demokrasia
linaloonesha jinsi sheria za uchaguzi zinavyovunjwa.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashir Ali, alisema hukumu hizo za
uchaguzi ikiwamo hiyo ya Igunga, zina maana sana kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,
Msajili wa Vyama vya Siasa, wanasiasa na wananchi.
“Tatizo
letu huwa hatusomi hukumu hizi kwa undani, kwani tungekwishajua kuwa ni darasa
tosha la demokrasia. Suala la takrima lilikuwa halieleweki kama ni rushwa,
ushindani wetu wa kisiasa si wa kuvumiliana, una matumizi makubwa ya fedha,
mali za serikali na madaraka kwenye kampeni,” alisema.
Ali
alifafanua kuwa hukumu hiyo imetoa mwanga kuwa, kama hakuna chombo huru cha
kusimamia sheria zinazokiukwa ni sawa na bure, akitolea mfano Tume ya Taifa ya
Uchaguzi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa licha ya kuwapo wakati wa
mchakato huo, vilishindwa kuchukua hatua.
“Kuna
mjadala kuhusu uwepo wa sheria ya Tume ya Uchaguzi, maana tangu kuanza kwa
mfumo wa vyama vingi hakuna sheria ya Tume ya Uchaguzi, badala yake chombo hiki
kinatambuliwa na sheria za uchaguzi, jambo linalotoa mwanya kwa mapungufu
yanayojitokeza sasa,” alisema.
Kuhusu
uwajibikaji wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wakati wa uchaguzi huo
mdogo, Ali alisema kuwa mpaka sasa umuhimu wa ofisi hiyo hauonekani maana kama
hoja ni kusajili vyama, kazi hiyo inaweza kufanywa hata mahakamani.
Alibainisha
kuwa, kwa sasa ofisi ya msajili na Tume ya Uchaguzi ni kama idara tu ndani ya
Ofisi ya Waziri Mkuu, hivyo wananchi wanapaswa kutumia hukumu ya Igunga kama
tathmini wakati huu wa mchakato wa katiba mpya kusahihisha makosa ya kuvifanya
vyombo hivyo huru.
Naye
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Mtatiro Julius, alisema
hukumu hiyo itawafungua wananchi kuona umuhimu wa kubadilisha mfumo wa uchaguzi
ili kuepusha taifa kuingia gharama zisizokuwa za lazima pale kiongozi anapokufa
ama kuenguliwa.
“Hii
naiona kama hatufikirii sawa sawa, maana matumizi ya mabilioni ya fedha kwenye
uchaguzi yalikuwa kwa vyama vyote kule Igunga hasa CCM, CHADEMA na CUF. Lakini
hili linaweza kuepukwa mana kama upuuzi unafanywa na watu wawili, hatuna sababu
ya kulisababishia taifa hasara,” alisema.
Kwa
mujibu wa Mtatiro, inapotokea hali kama hiyo ya mbunge kuenguliwa au kupoteza
maisha, mshindi wa pili kutoka chama kingine ndiye achukue nafasi badala ya
kurudia uchaguzi.
“Igunga
tuliona Dk. Kafumu walipishana kidogo na Kashindye wa CHADEMA, hivyo kwa vile
huyu alikiuka taratibu, basi mshindi wa pili apewe nafasi kuliko kurudia
uchaguzi, kwani kufanya hivyo kunaweza kukipa chama kilichoenguliwa ushindi
tena wa mtu asiyefaa,” alisema Mtatiro.
Mwanasiasa
huyo pia hakusita kuinyoshea kidole Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,
akisema kuwa, John Tendwa (msajili) ameonesha wazi ni wakala wa CCM anayefanya
mbinu za kukisaidia chama hicho kishinde badala ya kusimamia kanuni na sheria.
Mtatiro
aliweka bayana kuwa makosa yaliyoainishwa kwenye hukumu iliyomtia hatiani Dk.
Kafumu na kumnyang’anya ubunge wake, yalilalamikiwa mapema na wapinzani kwa
Msajili wa Vyama wakati wa kampeni, lakini hakuchukua hatua yoyote.
“Msajili
wa vyama hana meno, na huyu amekuwa na kashfa ya kusajili hata vyama visivyo na
sifa ilimradi tu aweze kuvidhoofisha vyama makini vya upinzani. Hata kwenye
uchaguzi ameonesha wazi anataka CCM ishinde,” alisema.
Mtatiro
aliongeza kuwa, umefika wakati nafasi hizo nyeti za vyombo kama Tume ya
Uchaguzi, Msajili na nyinginezo zitangazwe ili watu wenye taaluma zao
washindanishwe na kuchujwa na chombo maalumu badala ya kuteuliwa na rais.
Naye
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya,
alizungumzia hukumu hiyo ya Igunga akisema imetoa tafsiri mpya kwa wananchi
kuelewa demokrasia ya vyama vingi na namna ya kumpata mwakilishi makini bila
rushwa na vitisho.
“Hili
litakuwa fundisho kwa wanasiasa wanaochezea fedha nyingi kwenye uchaguzi
kununua watu, maana watatambua sasa kuwa kufanya hivyo kutawapotezea viti vyao.
Lakini na wagombea wanapaswa kuwa makini na wapiga debe na vyama vyao, kwani
wanaweza kuingizwa mtegoni kama alivyoponzwa Dk. Kafumu,” alisema.
Akisoma
hoja zilizothibitishwa na mahakama hiyo juzi, Jaji Shangali alisema ni pamoja
na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, kutumia nafasi yake ya uwaziri kutoa ahadi
ya ujenzi wa daraja la Mbutu ambalo lilikuwa ni moja ya kero kubwa kwa wananchi
wa Igunga.Waziri Magufuli akiwa katika uchaguzi mdogo huo katika moja ya
kampeni, alitumia nafasi ya uwaziri kuwatisha wapiga kura wa jimbo hilo kuwa
kama hawatamchagua mgombea wa CCM watawekwa ndani.
Jaji
Shangali pia alisema kuwa Mbunge wa Tabora Mjini, Aden Rage, alipita mitaani
akitangazia wananchi kuwa mgombea wa CHADEMA amejitoa.
Katika
hoja nyingine ni kwamba Imamu Swalekh Mohamed wa Mskiti wa Ijumaa Igunga,
aliwatangazia waumini wa Kiislamu kuwa wasiichague CHADEMA kwa kuwa baadhi ya
viongozi wake walimdhalilisha Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.
Nayo
matamshi ya Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, kudai kuwa CHADEMA imeleta
makomandoo kuuvuruga uchaguzi huo ni mojawapo ya hoja ambazo mahakama hiyo
ilizikubali.
Katika
hoja kuu ya mahindi, Jaji Shangali alihoji kama wananchi wa Igunga walikuwa na
njaa sana. Na kwamba, kama jibu ni ndiyo, ni kwanini uchaguzi usifanyike wakati
hawana njaa.
No comments:
Post a Comment