NAPE
AKERWA NA MABILIONI YANAYOCHANGISHWA NA CHADEMA
VUGUVUGU
la Mabadiliko (M4C) linaloendeshwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) limeanza kukitia kiwewe Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimesema
hakiamini kwamba Watanzania ndio wanaochanga mamilioni katika mikutano na
harambee za CHADEMA.
Vuguvugu
hilo linaifanya CHADEMA kuwa chama kiongozi, kwa kuifanya CCM kufuatilia nyendo
zake na kujaribu kufuta nyao kwa propaganda zinazoonesha hofu inayokipata chama
tawala.
Baada
ya vijana wa CHADEMA kuandaa hafla ya kuchangia chama hicho juzi Dar es Salaam
na kupata zaidi ya Sh 500 milioni (fedha taslimu na ahadi), jana Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, aliibuka na kudai mabilioni ya CHADEMA
hayachangwi na wapenzi wake bali wafadhili kutoka nje ya nchi.
Katika
mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Nape alidai kuwa CHADEMA
kinaandaa harambee kama njia ya kuhalalisha mabilioni waliyopewa na wafadhili
wao kutoka nje ya nchi.
Nape,
ambaye katika siku za karibuni amekuwa akieneza propaganda dhidi ya CHADEMA
alisema: “Umekuwa utamaduni wa CHADEMA kuwahadaa watu kwa kuitisha harambee za
kisanii baada ya kupewa mabilioni na wafadhili wao, ili mradi wahalalishe kuwa
fedha wanazotumia zimetokana na michango ya Watanzania wakati sikweli.”
Alisema
kuwa, CCM wana ushahidi wa kutosha unaoonesha mabilioni waliyopewa CHADEMA juzi
na wafadhili hao kwa lengo la kuendeleza operesheni mbalimbali nchini.
“Cha
kushangaza badala ya kuwaambia wanachama wao na Watanzania ukweli wa haya
mabilioni, wanaanza kuwahadaa kwa kuwachangisha na kugeuza mapato haya mtaji wa
baadhi ya watu binafsi ndani ya chama,” alisema Nnauye.
Alihoji
kuwa kwa nini mabilioni haya yanatolewa kwa CHADEMA sasa ambapo nchi yetu
imeendelea kufanya utafiti na ugunduzi wa rasilimali mbalimbali zikiwemo gesi
na mafuta?
Nape
aliongeza kuwa, iwapo CHADEMA hawatawaeleza ukweli wananchi, CCM itawasidia
kuwaeleza ukweli wa kiasi halisi cha mabilioni hayo, walikozitoa na mikataba
waliyoingia.
Nape
anasema hayo huku akijua kuwa baadhi ya wanachama waandamizi wa CCM, akiwamo
Rais Jakaya Kikwete, wamekuwa wakichangisha mamilioni ya shilingi katika
harambee mbalimbali za kisiasa na kidini, kutoka kwa wananchi maskini na
matajiri wa Kitanzania.
Hata
hivyo, Mkurugenzi wake wa Habari na Uenezi, John Mnyika, alisema kauli ya CCM
ni kiwewe kinachotokana na nguvu ya M4C.
“Propaganda
chafu hizi ni ishara ya kwamba CCM inaumizwa na namna ambavyo Watanzania
wanajitokeza kuunga mkono CHADEMA kwa hali na mali; CCM sasa inatapatapa
kujaribu kudhibiti wimbi la mabadiliko kwa kutumia siasa chafu,” alisema.
Mnyika
alisema CCM wanapaswa kueleza Watanzania iwapo mikakati hiyo michafu ina baraka
za mwenyekiti wao na serikali yake, kwani madai kama hayo yaliyotolewa na
Waziri wa Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, kuwa CHADEMA
itasambaratishwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa mbinu mbalimbali.
Aliongeza
kuwa, CCM imekuwa ikipata fedha za uchaguzi kwa njia za kifisadi, na sasa
wanataka kuichafua CHADEMA inayopata fedha kutoka vyanzo halali kwa njia za
wazi, na kwamba lengo la CCM ni kukatisha tamaa umma wa Watanzania unaochangia
vuguvugu la mabadiliko.
“Ni
ukweli ulio wazi kwamba CHADEMA imekuwa ikifanya harambee kwa uwazi kwa nyakati
mbalimbali katika kumbi na katika mikutano ya hadhara, ikiwemo ya vijijini
ambapo michango hutolewa kwa uwazi… Aidha michango kwa njia ya simu inaweza
kufuatiliwa na kuthibitisha bila shaka yoyote,” alisema.
Mnyika
alisisitiza kuwa, madai ya CCM kuwa CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni ya
shilingi kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi, na akarudia kukitaka chama hicho
kitaje majina ya serikali, taasisi ama kampuni za nje ambazo kinadai kwamba
zimetoa mabilioni ya shilingi katika siku za karibuni au zinatarajia kutoa.
“Badala
ya CCM kuisingizia CHADEMA, ilipaswa ieleze Watanzania orodha ya vigogo wa
serikali na wanachama waandamizi wa chama hicho, ambao wanaelezwa kuwa na
akaunti nchini Uswisi na nchi nyingine, wakituhumiwa kupewa fedha za kifisadi
kutoka kwa makampuni ya utafutaji wa mafuta, gesi asili pamoja na uchimbaji wa
madini.
“Madai haya si mapya
kutolewa na CCM, yaliwahi kutolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT),
Sophia Simba mara baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 akidai kuwa CHADEMA imepokea
fedha kutoka mataifa ya Ulaya kwa ajili ya kufanya maandamano ya kuiondoa CCM
madarakani, lakini akashindwa kuthibitisha,” alisema.
No comments:
Post a Comment