To Chat with me click here

Friday, August 17, 2012

PINDA: MWANAHALISI WAENDE MAHAKAMANI


WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amewataka wamiliki wa gazeti la wiki la Mwanahalisi lililofungiwa na serikali hivi karibu, waende mahakamani ikiwa hawakuridhika na uamuzi huo.

Pinda alisema kuwa serikali kwa sasa itaendelea kuitumia Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 kuyafungia magazeti hadi pale itakapofanyiwa marekebisho. Waziri Mkuu alitoa msimamo huo bungeni jana katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinznai Bungeni, Freeman Mbowe.

Mbowe alihoji ni kwa nini serikali imelifungia gazeti hilo kwa kutumia sheria inayolalamikiwa kuvikandamiza vyombo vya habari badala ya kulipeleka mahakamani ili wahusika nao wapate haki ya kujitetea. 

Hata hivyo waziri mkuu alisema serikali imefuata sheria na taratibu za nchi  kulifungia gazeti hilo.

“Kwa msingi wa sheria hiyo, kama kuna mtu anaona hajatendewa haki ni juu yake yeye sasa kutafuta namna ya kwenda mbele  kukata rufaa kwa kuzingatia taratibu zilizopo. Mimi nadhani ushauri mzuri ungekuwa ni huo,” alisema Pinda.
Katika swali la nyongeza, Mbowe, alizidi kusisitiza akihoji kama waziri mkuu haoni kwa kutumia sheria hiyo ni kuwanyima haki wahusika na ni kinyume cha utawala bora.

Pinda katika hilo, alisema haamini hivyo kwa kuwa sheria hiyo imetungwa na Bunge na kwa kuwa bado inatumika ni sheria halali. “Sisi tutaendelea kuitumia  sheria hiyo mpaka hapo itakapokuwa imerekebishwa,” alisema.

Julai 30 mwaka huu, serikali ililifungia gazeti la Mwanahalisi kwa muda usiojulikana kwa kutumia sheria hiyo ikidai kuwa lilichapisha habari ya uchochezi.

Wakati huo huo, waziri mkuu alisema kuwa wakuu wa wilaya na mikoa  ingawa ni watumishi wa serikali, lakini wanaruhusiwa kuimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika maeneo yao kwa kuwa ni jukumu lao la msingi. Alisema katika kufanya hivyo, dhamira ya msingi ni kuhakikisha chama kilichowaweka madarakani kinaendelea kushinda.

“Najua ndugu yangu Wenje kitakuwa kinakuuma sana, kwa sababu tumesema hivyo. Nataka nirejee kusisitiza kuwa wakuu wa wilaya na mikoa, na mimi waziri mkuu, ni kweli watumishi wa serikali tunalipwa mshahara kutokana na serikali kukusanya kodi, lakini hiyo haituondolei jukumu la msingi la kuhakikisha  ilani inatekelezwa  katika maeneo yetu, maana huo ndio msingi sana.

“Na katika kufanya hivyo, dhamira ya msingi ni kuhakikisha chama kilichoniweka madarakani kinaendelea kushinda, ndiyo maana yake…na ndiyo maana ninyi mnapotoka kule, kazi mnayofanya ni kutaka kutuondoa,” alisema na kuongeza kuwa kazi hizo mbili lazima zifanyike kuhakikisha mambo yanakwenda sawasawa.

Pinda alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA), aliyehoji kuwa, kwa maelekezo hayo ya serikali, wapinzani nao wakiamua kufanya kazi za chama kwa maelekezo yao nchi itaweza kusonga mbele.

“Tunavyofahamu DC ni mtumishi wa serikali na analipwa mshahara kwa kodi za wananchi wa vyama vyote, kama kweli maelekezo ya serikali ni hayo na sisi tukiamua kufanya kazi za chama chetu, huoni kwamba nchi haitasonga mbele kila mtu akiamua kufanya kazi ya chama chake?” alihoji Wenje.

Katika swali lake la msingi, Wenje alisema katika mkutano wa hadhara  wa CCM uliofanyika mjini Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, alisikika akisema kuwa ametumwa na Rais Jakaya Kikwete kwenda kuimairisha chama hicho, hivyo akataka kujua kama hiyo ndiyo sera na maelekezo ya serikali kwa ma-DC hao kwenye majimbo ya upinzani.

Pinda alijibu akisema kuwa inawezekana DC huyo alitoa kauli hiyo, lakini yeye hakusikia, na kuongeza kwamba kiongozi wa serikali anawekwa katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ya kisheria ambayo yameainishwa katika sheria na kanuni mbalimbali.

“Hiyo ndio kazi yake ya msingi, ikiwa ni pamoja na kulinda amani, kusimamia maendeleo na kuhakikisha kwamba wananchi wanaishi kwa amani na utulivu. Kama alieleza hayo, mimi tafsiri yangu ni kweli alilolisema hajakosea sana  kwa maana moja, chama hiki ndicho kilishinda na kinayo ilani yake ya uchaguzi, mkuu wa wilaya katika eneo lake ni lazima asimamie  utekelezwaji wake,” alisema.

Naye Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Kessy Mohamed (CCM), alihoji serikali imejipanga vipi kudhibiti matumizi ya fedha chafu ambazo zimeanza kuingia katika baadhi ya vyama vya siasa.

Waziri Mkuu alijibu swali hilo akisema ingawa taarifa hizo ni za kwenye mtandao hawatazipuuza, watazifanyia kazi na ikibainika hatua stahiki zitachukuliwa.

Kuhusu swali la Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM), aliyehoji ni hatua gani zinachukuliwa kwa watu wakiwamo baadhi ya wabunge wanaotumia nyaraka za siri za serikali ambazo wamezipata bila kufuata sheria. Pinda alisema nyaraka hizo zikipatikana kwa kufuata taratibu hakuna tatizo, bali shida ni pale zinapopatikana kinyume cha utaratibu.

No comments:

Post a Comment