To Chat with me click here

Saturday, August 4, 2012

TUME YA MABADILIKO YA KATIBA YATUPIWA KOMBORA

JUKWAA la Katiba Tanzania na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), limeirushia kombora  Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba inafanya utani katika zoezi zima la kukusanya maoni ya wananchi jambo ambalo litasababisha ipatikane Katiba ya kundi fulani la watu na siyo wananchi.

Kwa nyakati tofauti Jukwaa hilo na LHRC wameeleza kuwa utani huo upo katika machapisho ya kuelimisha umma yanayotolewa na Tume hiyo na upungufu katika ukusanyaji maoni, wenye ulemavu wa kusikia na kuzungumza kutokuwa na mkalimani, vituo vya kukusanyia maoni kuwa vichache, ratiba za tume, vyama vya siasa kuingilia mchakato na wajumbe wa tume kuendelea na shughuli zao za awali.

Kauli hiyo imekuja ikiwa imepita wiki moja tangu tume hiyo kumaliza kukusanya maoni ya wananchi katika mikoa minane, huku ikijipanga kuendelea na zoezi hilo katika mikoa mingine minane, wiki moja kuanzia leo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana,Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba alisema kuwa, mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi inayofanyika asubuhi inawafanya wananchi wengi kukosa nafasi ya kutoa maoni yao kwa kuwa wanakuwa katika shughuli mbalimbali.

“Ufuatiliaji wetu umebaini kuwa  mikutano inayofanyika asubuhi kuanzia saa 3 hadi saa 7 mchana inakuwa na watu wachache ikilinganishwa na mikutano inayofanyika kuanzia saa 8 mchana hadi saa 11 jioni,”alisema Kibamba.

Alisema kuwa , hali hiyo huwakumba hasa wananchi waishio vijijini  kwa kuwa muda huo wanakuwa katika shughuli za kilimo  na ujenzi na kusisitiza kuwa mkutano unatakiwa kufanyika mara moja kwa siku nyakati za jioni ili kila mwananchi ashiriki.

Alisema kuwa tatizo jingine waliloligundua ni tume hiyo kutokuwa na watu maalumu kwaajili ya kukusanya maoni ya watu wenye ulemavu hasa wenye ulemavu wa kuzungumza na kusikia.

“Tulitoa ushauri awali kwamba Tume itafute watalaamu kwa ajili ya kuwa na mawasiliano na watu wenye ulemavu wa kusikia na kuzungumza lakini haikuwa hivyo, matokeo yake wanapohudhuria mikutano wanashindwa kutoa maoni yao” alisema Kibamba.

Alisema hata vituo vya kukusanyia maoni vipo vichache na  vilivyopo vipo mbalimbali  jambo linalowafanya wananchi wanaoishi katika vijiji au kata ambazo tume hiyo haifiki, kushindwa kutoa maoni yao.

“Machapisho yaliyoandaliwa na Tume pia hayana ubora na yapo machache, hata vile vinavyoeleza Katiba kwa lugha nyepesi haviko sawa, ilitakiwa viandaliwe na wataalamu kutoka asasi mbalimbali nchini,” alisema Kibamba.

Alisema kuwa tume hiyo inatoa ratiba za mikutano yake katika kipindi kifupi na kuongeza kuwa mwezi huu tume hiyo inaanza tena zoezi la kukusanya maoni, lakini mpaka sasa haijatoa ratiba zake.

Alisema kuwa suala jingine ambalo linatakiwa kuangaliwa kwa umakini ni kitendo cha vyama vya siasa kuingilia zoezi la utoaji maoni, huku wanachama wake wakisafiri kila kituo ambacho tume hiyo hufika kukusanya maoni.

“Pia kulikuwa na tatizo la baadhi ya wajumbe wa tume kuendelea na shughuli zao za awali  na kuacha majukumu yao ya kukusanya maoni, pia wananchi wamekuwa wakitishiwa na wajumbe kwa kubanwa na kuulizwa maswali magumu wanapokuwa wanatoa maoni yao,”alisema Kibamba.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, DK Hellen Kijo –Bisimba alisema, wamebaini  kuwapo kwa upungufu mkubwa haki za wananchi kutoa maoni yao kwa uhuru.

Alisema muda wanaopewa wananchi wa kutoa maoni yao hautoshi, kwani hautoi nafasi ya kutosha ipasavyo kama inavyotakiwa.

“Muda uliopangwa na tume wa saa tatu kuanzia saa tatu mpaka saa sita mchana au saa nane mpaka saa kumi na moja jioni kwa kila mmoja kupewa dakika tano  za kutoa maoni hazitoshi na tume haipaswi kufanya hivyo,” alisema Bisimba na kuongeza:

“Muda wa asubuhi kutumika kukusanya maoni ni kuwanyima haki watu wengi kushiriki kutoa maoni yao kwani wakati huo wengi wanakuwa makazini.”

Bisimba alifafanua kwamba taarifa za kuwapo kwa Tume ya kukusanya maoni imekuwa finyu na kwamba hali hiyo imepelekea watu wengi kuacha kushiriki kutoa maoni.

“Kutokana na kukosekana kwa taarifa za kuwapo kwa Tume ya kukusanya maoni katika Kata kumekuwa na mwitikio mdogo wa wananchi kujitokeza kutoa maoni yao jambo ambalo linawanyima haki wananchi kutoa maoni yao,” alisema.

No comments:

Post a Comment