Marehemu Meles Zenawi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete asubuhi ya leo, Jumanne, Agosti 21,
2012, amepokea kwa mshtuko mkubwa, masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo
cha Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mheshimiwa Meles Zenawi, kilichotokea jana usiku
nje ya nchi ambako alikuwa anatibiwa.
Kufuatia taarifa hizo, Mheshimiwa Rais
Kikwete, kwa niaba ya wananchi wa Tanzania, Serikali yake na kwa niaba yake
mwenyewe amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Ethiopia, Mheshimiwa Girma
Wolde-Giorgis.
Katika rambirambi zake kwa Mheshimiwa
Wolde-Georgis, Rais Kikwete amesema: “Tanzania imepokea kwa mshtuko
mkubwa, masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Mheshimiwa Meles
Zenawi kilichotokea jana usiku.”
Amesema Rais Kikwete: “Kwa niaba
ya wananchi wa Tanzania, Serikali yangu na mimi mwenyewe, natuma salamu zangu
za dhati za rambirambi kwako, kwa wananchi wa Ethiopia na kupitia kwako kwa Mheshimiwa
Azeb Mesfin, mjane wa marehemu na familia nzima ya Mheshimiwa Meles Zenawi.
Tupo nanyi katika msiba huu mkubwa.”
“Kwa hakika, Ethiopia imempoteza
kiongozi hodari, mwana mapinduzi na mpenda maendeleo. Kwa hakika, Afrika
imempoteza kiongozi wa kutumainiwa na msemaji hodari sana wa Bara letu. Daima
tutamkumbuka Waziri Mkuu Zenawi kwa msimamo wake thabiti wa kutetea maslahi ya
Afrika na ustawi wa watu wake. Mimi na Tanzania tumempoteza rafiki wa kweli” amesema Rais Kikwete
na kusisitiza, “hakika tutaukosa mchango wake uliojaa busara, hoja zake
za kusisimua na zenye mantiki sana.”
Rais Kikwete amemaliza kwa kuwaeleza
wananchi wa Ethiopia: “Tunaungana nanyi katika wakati huu mgumu wa
majonzi na tunamwomba Mwenyeji Mungu awape nguvu, moyo, subira na baraka zake
ili muweze kuvuka kipindi hiki. Aidha, tunaungana nanyi na familia ya Marehemu
Zenawi kumwomba Mola ampe mapumziko mema Marehemu Meles Zenawi.”
Waziri Mkuu Zenawi ambaye ameaga dunia
akiwa na umri wa miaka 57 amekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia tokea 1995 na kabla
ya hapo alikuwa Rais wa nchi hiyo kati ya 1991 na 1995.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
21
Agosti, 2012
No comments:
Post a Comment