Ndg. Paul Chagonja |
Mkurugenzi
wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, amesema jeshi hilo halina bomu
lililotumika kumuua mwandishi huyo.
Akizungumza
katika kituo cha radio cha Magic FM jijini Dar es Salaam, Chagonja, aliwataka
wananchi kuwa watulivu wakati jeshi hilo likifanya uchunguzi wa kifo hicho.
Alisema
timu itakayofanya uchunguzi itaongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said
Mwema pamoja na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba na maofisa
wengine wa jeshi hilo.
“Tunawaomba
wananchi wa Iringa wawe watulivu wakati Jeshi la Polisi likifanya uchunguzi wa
tukio hili,” alisema Chagonja.
Pamoja
na hayo, alivitaka vyama vya siasa kutii sheria zilizowekwa katika kufanya
maandamano, ili kudumisha amani nchini.
Kwa
upande wake, Mchungaji na Mwalimu wa neno la Mungu katika Kanisa la Evangelist
Asembless of God (EAGT) Jimbo la Dodoma Magharaibi, Emanuel Msengi, amekemea
tabia ya Jeshi la Polisi kutumia nguvu na silaha za moto na kusababisha vifo
vya watu wasiokuwa na hatia.
“Sasa
taifa linaanza kupoteza mwelekeo, kwani inaonesha wazi kuwa nguvu ya Mungu
imetoweka katika taifa na roho ya mauaji kwa watu wasiokuwa na hatia
inatawala,” alisema.
Kuhusu
kuunda tume ya kuchunguza mauaji hayo, alisema ni matumizi mabaya ya fedha za
walipakodi, kwani inaonesha wazi kuwa waliohusika ni askari wa Jeshi la Polisi
na hakuna sababu yoyote ya kuunda tume.
Watu
wa kada mbalimbali wamelaani tukio la mauaji ya mwandishi wa habari wa
Televisheni ya Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Akizungumza
katika ofisi za Tanzania Daima, Sifa Majura, alieleza kushangazwa na kitendo
cha kikatili kinachodaiwa kufanywa na jeshi hilo.
Alisema
ni uonevu uliopitiliza, askari polisi kwa makusudi kukatisha uhai wa mwandishi
huyo aliyekuwa akitimiza majukumu yake.
“Uko
wapi utawala bora tunaouhubiri kila mara…hakuna bali kinachofanyika ni
kuudanganya ulimwengu, ili tuendelee kupata fedha za wahisani hao,” alisema.
Alihoji
kuwa ni kitu gani cha dhambi alichotenda mwanahabari huyo hadi jeshi hilo
lifikie hatua ya kutenda unyama wa aina hiyo.
Aliutaka
umma wa Watanzania kuamka na kuacha kukaa kimya, ili kupinga unyama huo ambao
hauvumiliki.
Huku
akiifananisha nchi ya Marekani alisema pamoja na kuwa na maadui wengi lakini
katika mikusanyiko na maandamano ya raia polisi wake hawaendi na risasi za
moto.
“Nashangaa
hapa nchini Jeshi la Polisi ni wapi wanataka kutupeleka…wenzetu kule pamoja na
vurugu lakini hawabebi risasi za moto zaidi ya virungu na mabomu ya machozi,”
alisema.
Naye,
Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Mbeya, William Mwamalanga, alisema Jeshi la
Polisi linapoteza dira kwa kuwa linashindwa kulinda raia na sasa limegeuka kuwa
la kiuaji.
Alisema
hatua hiyo inajenga chuki miongoni mwa jamii, kwani jeshi hilo linaonesha wazi
kuwa linatumiwa na vyama vya siasa.
Alisema
hali iliyoanza kujionesha sasa hivi kuna hatari kubwa kuja kuibuka wakati wa
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Mwamalanga,
aliwataka viongozi wa jeshi hilo kukubali kuwajibika na kujiuzulu kutokana na
kushindwa kazi.
“Katika
muda mfupi tu mauaji yanaibuka kila mahali, nadhani wakati umefika wa viongozi
wakuu wa jeshi hilo kukubali kujiuzulu bila shuruti,” alisema.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa asasi inayojihusisha na masuala ya afya ya Sikika,
Irenei Kiria, amelaani kitendo hicho na kusema ana matumaini waliohusika katika
mauaji hayo watachukuliwa hatua kwa kufikishwa katika vyombo vya dola, ili
sheria ichukue mkondo wake.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP), Ussu Mallya, alisema,
kitendo kilichofanywa ni cha kusikitisha, kuhuzunisha na kushangaza kwa kuwa,
polisi sasa wameacha kufanya kazi yao ya kulinda raia na kufanya mauaji.
“Msingi
wa polisi wa kulinda raia unaanza kuporomoka, ni vitendo vinavyozidi kuendelea
bila kuchukuliwa hatua madhubuti ya kuvikomesha raia wengi watapoteza maisha,”
alisema.
Alisema
anapouawa mwanahabari ambaye amejitolea kuhabarisha wananchi hicho ni kitendo
cha kutisha waandishi wengine na kuwanyamazisha washindwe kufanya kazi zao kwa
uhuru.
Alisema
wanaohusika wafanyiwe uchunguzi kwa kuwa vitendo hivi visipodhibitiwa
vitazidisha vurugu.
No comments:
Post a Comment