IKIWA
imebaki siku moja kuanza kwa sensa ya watu na makazi, kuna uwezekano wa
shughuli hiyo ikakwama jijini Dar es Salaam kutokana na kuendelea kuwapo kwa
mivutano ya malipo ya makarani watakaosimamia kazi hiyo.
Kampeni
ya sensa ya watu na makazi ilizinduliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wiki
iliyopita katika viwanja vya Mnazi Mmoja na inatarajia kuanza kufanyika Agosti
26, mwaka huu na kudumu kwa wiki moja.
Kundi
la makarani zaidi ya 30 jana liliandamana hadi katika ofisi za Wilaya ya
Kinondoni likitaka kujua hatma ya malipo yao ya sh 240,000 za kuhudhuria semina
kwa ajili ya mafunzo kwa siku saba.
Akizungumza
kwa niaba ya wenzake, Judith John, alisema kuwa hadi sasa sensa hiyo ina uwezekano
mkubwa wa kutofanikiwa kutokana na kuwepo kwa sintofahamu juu ya malipo yao.
Alisema
baadhi ya makarani walipewa fedha nusu ya sh 140,000 badala ya sh 245,000 huku
wengine wakiwa hawajui hatima ya malipo yao.
“Tunaona
kuwa kuna watu wana lengo la kuharibu hii sensa isifanikiwe, haiwezekani tangu
tuanze mafunzo hadi sasa tunahangaikia tu malipo bila kula kiapo wala kuingia
mkataba kwa kazi hiyo,” alisema.
Alisema
kuwa kwa sasa wamelazimika kurudi katika ofisi za wilaya ili kuendelea kusubiri
kulipwa fedha zao ambapo hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
Hata
hivyo vyanzo vya habari hii vilifanikiwa kukutana na mtumishi mmoja wa wilaya
hiyo (jina linahifadhiwa) ambaye alikiri kuwepo kwa uzembe katika mchakato huo
na kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa kufanikiwa.
Mtumishi
huyo alisema kuwa kulikuwa na uwezekano wa kupata fedha mapema kutoka benki
lakini baadhi ya viongozi wanaonekana kutaka kujinufaisha wao binafsi jambo
ambalo linaweza kuleta matokeo hasi.
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, alifafanua kuhusu mvutano na kusema
kuwa wanaoendelea kukosa malipo ya semina inawezekana si makarani halisi wa
sensa kwani asilimia kubwa walilipwa nusu ya fedha zao.
Sadick
alikiri kuwepo kwa kasoro katika suala hilo lakini akasema kwa sasa
limerekebishwa na utaratibu wa malipo katika vituo vyote jijini humo
unaendelea.
“Niseme kuwa benki haiwezi
kuishiwa fedha, kilichojitokeza ni malipo tu kuchelewa kwani malipo
yanayotakiwa kutolewa ni makubwa na lazima unapohitaji fedha nyingi upeleke
mapema maombi yako,” alisema.
No comments:
Post a Comment