Katika
hatua nyingine Kamati Kuu ya CCM (CC), imeeleza kuridhishwa na utendaji wa mawaziri, Dk. Harrison
Mwakyembe wa Ujenzi, Balozi Khamis Kagasheki wa Maliasili na Utalii na Dk.
Abdallah Kigoda wa Viwanda na Biashara katika kuwachukulia hatua wakuu wa
mashirika ya umma waliojihusisha na ubadhirifu.
Bila
kuwataja kwa majina, Nape alisema kuwa CC ilipokea taarifa ya maendeleo ya
utekelezaji wa maagizo yake juu ya kushughulikia mapungufu yaliyooneshwa kwenye
taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kamati
mbalimbali za Bunge.
“CC
imeipongeza serikali kwa hatua zilizoanza kuchukuliwa dhidi ya mapungufu hayo,
hasa hatua dhidi ya wakuu mbalimbali wa mashirika kadhaa ya umma, kama vile
Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO), Shirika la Viwango (TBS), Mamlaka ya
Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Ndege Tanzania (ATC) na Wizara ya Maliasili
na Utalii,” alisema.
Hata
hivyo, licha ya kutotajwa kwa majina, mawaziri hao watatu wameanza kazi kwa
vitendo ikiwa ni kuwasimamisha kazi baadhi ya vigogo kwenye wizara zao
waliokuwa wakituhumiwa kujihusisha na ufisadi.
Dk.
Mwakyembe ameanza kwa kumsimamisha kazi aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ATC,
Paul Chizi na wakurugenzi wanne kutokana na ukiukwaji wa sheria, kanuni na
taratibu za utumishi wa umma. Na wiki aliyopita amemsimamisha kazi Mkurugenzi
Mkuu TPA, Ephraim Mgawe na viongozi wengine watatu ili kupisha uchunguzi wa
tuhuma mbalimbali za ufisadi zinazowakabili.
Waziri
Kigoda yeye alianza kazi kwa kumsimamisha aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBS,
Charles Ekelege ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi zilizokuwa
zikimkabili.
Agosti
13 mwaka huu, Waziri Kagasheki, alitangaza kuwatimua kazi vigogo watatu wa
wizara yake akiwamo Mkurugenzi wa Wanyamapori, baada ya kubainika kuhusika
katika kashfa ya utoroshaji wanyamapori hai kupitia Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenda nje.
Vile
vile wiki aliyopita, alitangaza kubadili utaratibu za kuwapata wajumbe wa bodi
zilizoko chini ya wizara ambapo kuanzia sasa watapatikana kwa njia ya ushindani
badala ya kuteuliwa moja kwa moja na waziri.
Nape
aliongeza kuwa, itakumbukwa kuwa CC iliagiza pamoja na viongozi wa kisiasa
kuchukuliwa hatua kwa mapungufu yale, ipo haja ya kuwachukulia hatua watendaji
wakuu wa mashirika yaliyohusishwa na ubadhirifu mbalimbali.
“Kamati
Kuu inawapongeza mawaziri husika na watendaji wote wa serikali walioanza
kutekeleza agizo hili kwani mwisho wa siku maisha bora kwa kila Mtanzania
yatawezekana,” alisema.
No comments:
Post a Comment