OPARESHENI maalumu ya ‘Vua gamba vaa
Gwanda’ inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imeitikisa
Wilaya ya Tarime mkoani Mara, baada ya zaidi ya wanachama 3,500 wakiwemo
viongozi wa CCM kujiunga na CHADEMA wilayani hapa.
Mbali na idadi hiyo ya watu kujiunga na
CHADEMA, pia wananchi wengi wamegombania kadi za chama hicho kama njugu, ikiwa
ni lengo la kutaka kujiunga na harakati za vuguvugu la kutaka kuleta mabadiliko
ya kisiasa hapa nchini kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2014, na
hatimaye uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Wanachama hao
wakiwemo viongozi wa CCM wamejiunga na CHADEMA wakati wa mkutano wa hadhara wa
chama hicho, uliofanyika mjini Sirari kisha kuhutubiwa na mwenyekiti wa Baraza
la Vijana taifa wa chama hicho (BAVICHA), John Heche.
Miongoni mwa viongozi
wa CCM waliorudisha kadi kisha kukabidhiwa kadi za CHADEMA mkutanoni hapo, ni
pamoja na mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Sirari, Masha Vincent ambapo mke
wake pia Veronika Masha alirudisha kadi ya CCM kisha kujiunga na CHADEMA.
Akizungumza kwa niaba
ya wanachama wengine wapya waliojiunga na chama hicho kikuu cha upinzani nchini
mara baada ya kukabidhiwa kadi za Chadema, Masha alisema wamechukuwa uamuzi huo
baada ya kuchoshwa na kile alichodai majungu, fitina na uhasama unaofanywa na
baadhi ya viongozi wa CCM wilayani hapa.
Alisema, enzi za CCM
zinaonekana kuelekea kuisha, hivyo kujiunga kwao na CHADEMA ni kuongeza
vuguvugu la mabadiliko, na kuwaomba vijana kufanya maamuzi ya dhati katika
kuleta mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.
“Mimi nimeamua
kuondoka rasmi CCM. Maana yupo kiongozi mmoja hapa Sirari alikuwa anatusakama
baada ya kumpinga mambo yake. Sasa tupo kwenye chama makini na chenye mtazamo
mpana katika maendeleo ya nchi hii”, alisema Masha kisha kushangiliwa na umati
mkubwa wa watu.
Awali, mwenyekiti wa
Bavicha taifa, John Heche aliwaomba Watanzania kutumia kura zao vizuri uchaguzi
wa serikali za mitaa wa mwaka 2014 pamoja na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na
Madiwani utakaofanyika nchini mwaka 2015 kwa kuipigia kura CHADEMA ili ishike
dola na kuleta mabadiliko ya kweli katika maendeleo ya wananchi.
Alisema, CHADEMA
imedhamiria kuleta ukombozi mpya kwa wananchi wa taifa hili, na kwamba iwapo
Watanzania wataiwezesha kuingia madarakani mwaka 2015, itahakikisha serikali
yake inatumia vizuri rasilimali za nchi kwa faida ya Watanzania wenyewe na si
wawekezaji.
Aidha, akiwa katika mkutano wa hadhara kule Muriba Tarime jana, Heche alilaani vikali mauji ya vijana yanayodaiwa kufanywa na baadhi ya askari polisi katika mgodi wa dhahabu wa Nyamongo uliopo wilayani hapa, na kusema upo uwezekano wa kuishtaki serikali ya Tanzania katika mahakama ya Kimataifa ya makosa ya uhalifu (ICC), kuhusiana na mauaji hayo.
Alisema, CHADEMA
haiwezi kuendelea kuona Watanzania wanauawa kama wanyama katika wilaya hiyo,
hivyo ikibidi ipo siku serikali italazimika kwenda kujibu mashtaka kwenye
mahakama hiyo ya ICC kuhusiana na unyama inaowafanyia wananchi wake kwa
kuruhusu jeshi lake la polisi kutumia mtutu kuwaua raia mgodini hapo.
“Hatuwezi kukubali
vijana wetu, Watanzania wenzetu, wakurya wenzetu waendelee kuuawa kwa kupigwa
risasi na polisi katika mgodi wa Nyamongo. Ipo siku serikali ikibidi
itashtakiwa ICC kutokana na mauaji ya wananchi wetu”, alisema mwenyekiti huyo
wa Bavicha taifa, Heche.
Alisema, mgodi wa
Nyamongo kama ungelitumiwa vizuri na Serikali ya CCM ingelisaidia kupeleka
maendeleo ya elimu, barabara, maji safi na salama ya kunywa, hospitali pamoja
na mawasiliano, lakini kwa sasa madini hayo yanatumika kuwanufaisha raia wa nje
ya nchi.
Hata hivyo,
aliituhumu Serikali ya CCM kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete kwamba utawala huo
umekuwa ombaomba namba moja kwa misaada huko Ulaya, na kusema wakati mwingine
Rais Kikwete huwa anapishana na ndege za wazungu zikiwa zimebeba madini, huku
kiongozi huyo naye akitoka Ulaya kuomba vyandarua, jambo ambalo litaenda
kudhibitiwa na CHADEMA itakapoingia Ikulu 2015.
No comments:
Post a Comment