Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapinga kauli za Serikali, Jeshi la Polisi
na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zenye kulipotosha taifa kuhusu mashambulizi na
mauji yanayoelezwa kufanywa na askari Mkoani Morogoro na badala yake kinataka
uchunguzi huru ufanyike haraka kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo
(Inquest Act).
Kauli
zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani zina mwelekeo wa kulilinda Jeshi la
Polisi ambalo askari na maofisa wake ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji, badala
ya kuwezesha ukweli kuthibitika na hatua kuchukuliwa kwa wahusika.
Hivyokutokana
na kujirudiarudia kwa mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola CHADEMA kinatoa
mwito kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye kwa mujibu wa katiba ibara ya 33 ni mkuu
wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu aingilie na kuwezesha
uchunguzi wa kina.
CHADEMA
kinaukumbusha umma kwamba kwa mauaji hayo na mengine katika maeneo mbalimbali
nchini serikali inayoongozwa na CCM kupitia vyombo vya dola inaendelea kukiuka
Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatambua
kwamba uhai ni haki ya msingi kwa raia wote.
CHADEMA
hakikubaliani na hatua zilizochukuliwa na Serikali mpaka sasa kuhusu tukio
husika pamoja na maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani tarehe 28
Agosti 2012 ambayo kwa sehemu kubwa yametokana na taarifa zisizo za kweli
kutoka kwa maofisa wa Jeshi la Polisi ambao ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji
husika.
CHADEMA
haina imani na timu iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi kuchunguza tuhuma za
askari kufyatua risasi na mabomu ya machozi na kusababisha mauaji kwa kuwa
tayari serikali na Jeshi la Polisi wametoa maelezo yenye kutofautiana kwa
kiwango kikubwa na maelezo ya mashuhuda waliokuwepo na ushahidi wa picha za
eneo la tukio.
Wakati
Serikali na Jeshi la Polisi wakitoa maelezo kuwa marehemu alikutwa umbali wa
mita 300 na kupelekwa hospitali na wasamaria wema, mashuhuda wameeleza wazi
kuwa askari walifika jirani na eneo lake na ofisa mmoja akaonyesha ishara na
ndipo risasi za moto na mabomu ya machozi yakafyatuliwa mojawapo kumpata
marehemu na kudondoka.
Mashuhuda
wote waliohojiwa wanaeleza kwamba bunduki ya polisi ndiyo ilielekezwa na
kufyatuliwa kwa marehemu, maelezo pekee yanayotofautiana ni kuwa baadhi
wameeleza kuwa ni bunduki ya risasi za moto na wengine wa wameeleza kuwa ni
bunduki ya kufyatulia mabomu ya machozi.
Mara
baada ya kudondoka gari hilo liliondoka na gari lingine la polisi lilifika
likiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia cha Mkoa ambaye alitoa
amri ya gari lingine kumbeba Ali Hassan Singano (Zona) na kuondoka naye, hivyo
si kweli kwamba matukio hayo yalitokea mbali na eneo bali pembeni ya meza ya
muuza magazeti huyo karibu na barabara ya kwenda Iringa eneo ambalo polisi
ilikuwa ikifanya mashambulizi.
Kauli
zilizotolewa na Serikali kuwa Jeshi la Polisi lilizuia maandamano ya CHADEMA
yaliyopangwa kufanyika Mkoani Morogoro kwa sababu ya sensa ya watu na makazi si
za kweli kwa kuwa sababu pekee zilizotolewa ni ufinyu wa barabara na kuwa
maandamano yalipangwa siku ya kazi. Ushahidi wa suala hili ni barua ya Jeshi la
Polisi lenyewe ya 23 Agosti 2012 yenye Kumb. Na. MOR/A.25/1/VOL. II/202.
CHADEMA
kinaujulisha umma kwamba Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro ndilo lililoacha
kuheshimu utawala wa sheria na makubaliano yaliyofikiwa baada ya mazungumzo
yaliyohusisha kikosi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kikiongozwa na
Kamanda wa Operesheni za Jeshi hilo Simon Siro na hivyo kuwa chanzo cha mauaji
yaliyotokea na madhara mengine kwa wananchi waliokuwepo maeneo yaliyorushiwa
mabomu ya machozi.
Ikumbukwe
kwamba awali CHADEMA kilipanga kufanya maandamano na mikutano katika Jimbo la
Morogoro Mjini tarehe 4 Agosti 2012 na kuwasilisha taarifa kwa Jeshi la Polisi
kwa mujibu wa sheria.
Hata
hivyo, Polisi wakakataa kufanyika kwa maandamano na mikutano kwa kisingizio cha
Sikukuu ya Nanenane, mgomo wa walimu na ratiba kugongana na ile ya mikutano ya
CCM, sababu ambazo zilibainika kwamba hazikuwa na msingi wowote.
Baada ya
mvutano na mazungumzo CHADEMA ilikubali kutii sheria na kuzingatia matakwa ya
Jeshi la Polisi pamoja na kuwa yalitolewa kinyume cha Sheria kwamba maandamano
na mkutano wa CHADEMA vifanyike mara baada ya siku ya kuanza kwa sensa tarehe
26 Agosti 2012 na CHADEMA ilipendekeza tarehe 27 Agosti 2012 ambayo Jeshi la
Polisi liliikubali.
Polisi
walifanya hivyo wakielewa ukubwa wa barabara za Morogoro na pia wakitambua
kwamba ilikuwa ni siku ya kazi, hata hivyo tarehe 23 Agosti 2012 Jeshi la
Polisi liliandika barua ya kueleza kwamba limetoa kibali cha mkutano (suala
ambalo si mamlaka yake kisheria) na pia limekataza maandamano.
CHADEMA
kikaamua kwa mara nyingine tena kurudi katika meza ya mazungumzo na Jeshi la
Polisi Mkoa wa Morogoro, tarehe 24 Agosti 2012 ambapo polisi ilikubali
maandamano ikiwemo ya watembea kwa miguu na kupendekeza njia mbadala na tarehe
26 Agosti 2012 mazungumzo yakaendelea kwa lengo la kukagua barabara.
Hata
hivyo, kufuatia shinikizo la Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro Faustine
Shilogile kinyume na Sheria ya Jeshi la Polisi ambayo imetoa mamlaka kwa Mkuu
wa Polisi Wilaya kuhusu taarifa za mikutano, polisi ikarejea katika msimamo wa
kukataza mapokezi ya watembea kwa miguu na badala yake tarehe 26 Agosti 2012
bila sababu za misingi ya kisheria na zisizozingatia haki za kikatiba
ikapendekeza kwamba yafanyike mapokezi kwa kutumia magari.
Maelezo
ya Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa iwapo vyama vya siasa visiporidhika na
mazingira kama hayo yapo mamlaka ya kukata rufaa yanapotosha kwa kuwa Sheria ya
Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa hazijaweka utaratibu wa rufaa
hivyo njia pekee ya kisheria ni kutumia mahakama.
Jeshi la
Polisi lingeheshimu utawala wa sheria na mazungumzo lingeruhusu CHADEMA ifanye
maandamano na kutoa ulinzi mpaka eneo la mkutano kwa muda mfupi badala yake
jeshi hilo likaamua kutumia nguvu kubwa na kusababisha mauaji, barabara
kufungwa kwa muda mrefu na kuathiri wananchi waliokuwa wakiendelea na kazi zao.
Iwapo
wanachama na wananchi waliokuwa wamekusanyika kuwapokea viongozi na kuelekea
kwenye mkutano wangekuwa wamekiuka sheria Jeshi la Polisi lingeweza kuwakamata
kwa mujibu wa sheria, hata hivyo hakuna kiongozi yoyote wa CHADEMA
aliyefunguliwa jalada mpaka sasa katika kituo chochote cha polisi kwa kudaiwa
kukiuka sheria.
Kinyume
chake Jeshi la Polisi ambalo likiwa kwenye mazungumzo lilikubali kuwa mapokezi
yafanyike kwa msafara wa vyombo vya moto, lakini tarehe 27 Agosti 2012 likaamua
kupiga mabomu ya machozi kwa wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa
wamekusanyika eneo la Msamvu wakiwasubiri viongozi bila hata ya kusubiri kuona
iwapo yangefanyika matembezi ya miguu kuelekea eneo la mkutano au maandamano ya
magari na vyombo vingine vya usafiri.
Kitendo
cha Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa kinyume cha sheria na kusababisha
mauaji na kufunga barabara kwa muda mrefu kiliwafanya wanachama wa CHADEMA na
wananchi kwa ujumla kutawanyika kuelekea eneo la mkutano na wengine kuingia
barabarani kutembea kuelekea eneo la mkutano na hatimaye polisi walipoona
wamesababisha hali hiyo wakaamua kulinda misafara hiyo mpaka eneo la mkutano
hali inayodhihirisha kuwa uamuzi kama huo ungechukuliwa kutoka mwanzo
yasingetokea madhara yoyote.
Kwa
kuzingatia utofauti mkubwa baina ya maelezo yanayotolewa na Serikali na Jeshi
la Polisi kuhusu matukio husika na ukweli halisi ulivyotokea, CHADEMA
kinasisitiza kuwauchunguzi huru ufanyike kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa
Vifo (Inquest Act) Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania.
CHADEMA kwa
mara nyingine kinaitaka Serikali inayoongozwa na CCM kurejea katika kifungu cha
3 cha Sheria ya Uchunguzi wa Vifo, ambacho kinatoa mamlaka ya Waziri mwenye
dhamana na masuala ya Sheria kuanzisha Mahakama ya Kuchunguza Vifo hivyo
(Coroner’s Court) katika maeneo ya serikali za mitaa kwa kushirikiana na Jaji
Kiongozi.
CHADEMA
kinaikumbusha Serikali kuwa, kufuatia kauli ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni na Mawaziri Vivuli husika kueleza bungeni taarifa za mauaji
yaliyofanywa na vyombo vya dola kwa nyakati mbalimbali, Waziri Mkuu na Mawaziri
wengine waliahidi bungeni kwamba sheria hiyo itaanza kutumika kuchunguza vifo
vyenye utata.
Katika
muktadha huo uchunguzi wa kifo cha Ali Zona haupaswi kufanywa na timu ya polisi
bali sheria hiyo sasa ianze kutumika.
Kwa
upande mwingine, CHADEMA imeheshimu taratibu za maziko zilizopangwa na familia
ambapo mwili wa marehemu ulisafirishwa jana tarehe 28 Agosti 2012 kwenda Mkoani
Tanga kwa ajili ya maziko na CHADEMA kuwasilisha rambirambi zake za awali, taarifa
zaidi kuhusu ushiriki kwa CHADEMA kwenye maziko zitaelezwa baada ya majadiliano
yanayoendelea na familia.
CHADEMA
kwa kuheshimu mazungumzo na utawala wa sheria kwa mara nyingine tena tarehe 28
Agosti 2012 CHADEMA kimesitisha Operesheni za Maandamano na Mikutano yake ya
Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwa rai iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi
(IGP) ili kupisha kukamilika kwa zoezi la sensa ambayo imetokana pia na maelezo
ya mamlaka zingine za kiserikali.
CHADEMA
inatambua kwamba wakati maandamano ya CHADEMA yametolewa rai kuwa yasitishwe
kupisha sensa, maandamano ya wagombea wa CCM kurudisha fomu za uchaguzi wa
ndani ya chama chao yameachwa yakiendelea katika barabara kadhaa nchini bila
kusitishwa kwa kisingizio hicho.
Aidha,
wakati CHADEMA ikiheshimu mazungumzo na kusogeza ratiba yake mbele ya tarehe 26
Agosti 2012 mpaka tarehe 27 Agosti 2012 kupisha sensa hatua ambayo ilifanywa
pia na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo ilitangaza ratiba yake kuendelea
baaada ya tarehe hiyo.
Tume hiyo
inaendelea na mikutano yake ya hadhara inayokutanisha wananchi katika kata za
mikoa mbalimbali wakati huo huo zoezi la sensa likiendelea lakini kwa mikutano
ya CHADEMA inaonekana kufanyika kwake ni kuingilia sensa.
CHADEMA
inataka Serikali na Polisi kueleza iwapo matukio haya na mengine hayana
mwelekeo wa ubaguzi na uhujumu wa vuguvuvugu la mabadiliko linaloendelea nchini
kwa kurejea ukweli kuwa maisha ya wachache yanaweza kuwekwa mashakani lakini si
mabadiliko kwa maslahi ya wengi.
CHADEMA
itaeleza hatua za ziada itakazochukua baada ya kupata ripoti ya uchunguzi wa
mwili wa marehemu (post mortem) uliofanyika tarehe 28 Agosti 2012 na uamuzi wa
Serikali kukubali au kukataa mwito wa kutumia Sheria ya Uchunguzi wa Vifo
(Inquest Act) kuwezesha uchunguzi huru.
Imetolewa
tarehe 29 Agosti 2012 na:
John
Mnyika (Mb)
Mkurugenzi
wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment