To Chat with me click here

Wednesday, August 29, 2012

POLISI WAKUBALI MBINU ZAO ZIMEFELI KWA CHADEMA


NACHELEA kusema kama ni mkakati wa makusudi ama ni kutumiwa na watawala pasipo kujielewa, lakini kwa maneno mepesi napenda kuliomba Jeshi letu la Polisi likubali kuwa mbinu zake za kukidhohofisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) zimefeli.
Takwimu za kisiasa nchini tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi Julai 1992, zinaonesha kuwa vyama vyote vikubwa vimesambaratishwa kwa nguvu ya virungu, mabomu ya machozi, maji ya kuwasha, risasi za moto za polisi vilivyoelekezwa ama kwa viongozi wa vyama hivyo au wafuasi wao.
Sihitaji kuandika historia hiyo upya leo, lakini itoshe kusema kuwa bado tunaikumbuka NCCR-Mageuzi ya wakati huo (1995-1998) chini ya Augustine Mrema na baadaye TLP. Makeke ya mwanasiasa huyu na wafuasi wake yalimalizwa na polisi waliowaandama kila kona kuhakikisha hawaandamani kwa amani wala kufanya mikutano ya hadhara na shughuli zao nyingine za kisiasa.
Tulishuhudia kamatakamata za kudhalilisha kwa viongozi wa vyama vya upinzani na kufunguliwa kesi zisizo na mashiko ambazo mwisho wake zilifutwa bila hata nyingine kusikilizwa. Kwa hilo Jeshi la Polisi tulipe heko kwani lilifanikiwa kutimiza ajenda yake. Swali lililobakia hadi leo ni je, walitumwa kumsaidia nani?
Miaka ya 2000-2005 baada ya NCCR-Mageuzi na TLP kunyong’onyeshwa, kiliibuka Chama cha Wananchi (CUF), enzi hizo kikijiita ngangari, lakini nacho kilishughulikiwa ipasavyo na polisi chini ya IGP yule yule, Omar Mahita.

Sidhani kama kuna anayefurahia mauaji yaliyofanywa na polisi Januari 26 na 27 mwaka 2001 kwa wafuasi wa CUF kule visiwani Zanzibar kwa wananchi zaidi ya 33, wengine kubakia vilema hadi leo, huku mamia wakiikimbia nchi na kwenda kuishi maisha ya ukimbizi eneo la Shimoni Mombasa nchini Kenya.


Yako mengi mabaya ya kueleza kuhusu unyama waliotendewa viongozi wa CUF na wafuasi wao Bara na Visiwani, lakini nihitimishe na kituko cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, ambapo IGP Mahita alijitokeza kwenye vyombo vya habari akiwa na visu na kudai ni vya chama hicho.

Mahita aliyekuwa akijiita ngunguri, yaani jina mbadala la ngangari ya CUF, aliitisha mkutano na waandishi wa habari akiwa na visu kadhaa vipya, akaueleza umma kuwa vimeingizwa kwa makontena nchini na chama hicho kwa lengo la kuvitumia kufanya vurugu.


Mpaka naandika makala haya sikuwahi kusikia kama kuna kiongozi wa CUF alifikishwa mahakamani kuhusika na suala hilo la kigaidi wala kumsikia Msajili wa Vyama vya Siasa akitoa kauli au Jeshi la Polisi kuomba radhi kwa uongo huo wa IGP mstaafu Mahita.
Ngwe hiyo imepita, mwaka 2010 CHADEMA ndicho kimeshika usukani wa upinzani nchini, lakini tayari polisi wamekiandama kwa mizengwe ya kila aina ambayo sasa inaelekea kushindikana kabisa japo hawajakubali. Je, nani anawatuma na kuna ulazima wa kutekeleza hayo badala ya kusimamia haki?
Nijuavyo kuhusu Jeshi la Polisi, ni kwamba hiki ni chombo cha dola cha kudumu milele ila chama cha siasa kinaweza kuja na kuondoka. Na hoja yangu inabakia hapa kuwa, hata kama jeshi letu la polisi linatumwa na watawala kuvisambaratisha vyama vya upinzani je, watawala hao na vyama vyao watadumu milele kama polisi?
Nimeeleza jinsi NCCR-Mageuzi, TLP na CUF walivyoshughulikiwa na kusambaratishwa na polisi na sasa nguvu hiyo wameielekeza CHADEMA kuanzia Januari 5, 2011 jijini Arusha, wakazima maandamano ya amani ya chama hicho na kuwaua kwa risasi wananchi watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 30 kisha kuwafungulia viongozi mashtaka.
Tuliona jinsi polisi wetu wenye wajibu wa kulinda amani ya raia na mali zao, walivyowadhalilisha viongozi wa CHADEMA wakiwemo wabunge kwa kuwapiga mitama na kuwatumbukiza kwenye mitaro ya maji machafu, kuwapiga virungu, na kuvunja vioo vya magari yao kana kwamba ni majambazi sugu yamekamatwa.
Kigezo cha kufanya hivyo tuliambiwa ni intelijensia yao iliwaonesha kuwa maandamno hayo yangekuwa na vurugu. Sawa tuwakubalie kuwa walitimiza lengo la aliyewatuma, lakini swali letu kwao ni kwamba damu iliyomwagika itafutikaje viganjani mwao?
Yako matuko mengine mengi kama kule jijini Mwanza, polisi walipowapiga virungu, mabomu na kuwamwagia maji ya kuwasha wafuasi wa CHADEMA, Mkoani Singida hivi karibuni mkutano wa chama hicho ulivamiwa kwa mawe hadi kijana mmoja anayedaiwa kuwa mfuasi wa CCM kuuawa.
Juzi mkoani Morogoro risasi za polisi zimemuua kijana Ally Nzona na kuwajeruhi wengine wawili, Frank Mbalimba na Hashim Seifu katika harakati za kusambaratisha maandamano ya amani ya CHADEMA.

Pengine hii ni taswira iliyokuwa inataka kujengwa kwa umma kuwa mikusanyiko ya CHADEMA ni ya vurugu yenye kusababisha umwagaji damu. Lakini ukweli mara zote umejidhihirisha kwamba wanaopoteza maisha hawauliwi na chama hicho.

Yafaa sasa polisi wakubali mbinu zao zimefeli kwa CHADEMA, watambue kuwa nguvu ya umma haikwepeki, wananchi wanataka mabadiliko ya kisiasa ndiyo maana wanakiunga mkono chama hicho kwa kila jinsi bila kujali kuna risasi, mabomu ya machozi wala maji ya kuwasha.

Jeshi la Polisi kwa miaka kadhaa baada ya kuingia madarakani IGP Said Mwema, lilibadilika sana kiutendaji na kuendesha mambo yake kisomi, lakini kwa miaka ya karibuni limeanza kurudia ubabe wake wa enzi zile za Mahita bila kutambua hao wanaowadhalilisha na kuwapiga mabomu au risasi ndio viongozi wao wa kesho. Tafakari!

edkamukara@yahoo.com 0714 717 115 au 0788 452 350

No comments:

Post a Comment