Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna
Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP), Michael Kamuhanda, amesema hawatakuwa na
sababu ya kuzuia mikutano ya CHADEMA baada ya shughuli za sensa kumalizika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamuhanda
alisema tangu siku ya kwanza CHADEMA walipoingia mkoani humo hali ya utulivu
ilikuwa ni nzuri na hakukuwa na matatizo yoyote mabaya waliyosababisha.
“Tunajua watafanya mkutano wao Septemba 2, mwaka
huu, wilayani Mufindi, hatuna sababu ya kuzuia hilo labda ijitokeza sababu ya
kiusalama, kwa kuwa hata Dk. Slaa nimezungumza naye na akaniambia wako salama
na amefurahia walivyopokewa kifalme katika mkoa huu,” alisema Kamuhanda.
Akizungumzia sababu ya kuimarisha ulinzi, Kamanda
Kamuhanda alisema hatua hiyo inatokana na hali halisi ya kisiasa kwa sasa na
kwamba polisi wana wajibu wa kuchukua tahadhari kuhakikisha usalama unakuwepo.
Alipoulizwa kama jeshi hilo linatumiwa na viongozi
wa CCM katika kuhakikisha mikutano ya CHADEMA haifanikiwi, Kamuhanda alisema si
kweli kwani hata baadhi ya viongozi wa CCM wakiwamo wabunge wa mkoa huo
hajawahi kukutana nao.
Tangu kuingia kwa viongozi kadhaa wa CHADEMA mkoani
Iringa, jeshi hilo limekuwa katika tahadhari kubwa kwa hofu kuwa wanaweza
kufanya mikutano kabla ya sensa ya watu na makazi kumalizika.
No comments:
Post a Comment