KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ), Dk. Willibrod Slaa,
amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinachukiwa na wananchi kutokana na
kuendelea kujitetea kwa kutumia sababu zilizotumiwa na wapigania uhuru wa
Tanganyika kujikomboa katika mikono ya wakoloni.
Akizungumza katika
mikutano ya hadhara kwenye vijiji mbalimbali vya kata za Ngerengere na
Makambarai, Dk. Slaa alisema serikali ya CCM imeshindwa kutengeneza fursa ya
wananchi kujiletea maendeleo yao licha ya kuwa katika nchi yenye rasilimali
nyingi.
“Mwalimu
Nyerere pamoja na wapigania uhuru wengine wa Tanganyika hawakumkataa mkoloni
kwa sababu ya rangi, dini wala hali zao isipokuwa waliwakataa kwa vile
walishindwa kuwaondolea watu umaskini, ujinga na maradhi ambayo yanaendelea
kutuandama kila wakati,” alisema.
Alisema
kuwa hayati Mwalimu Nyerere alifikia malengo kwa kuonesha njia ya kupita, hivyo
waliomfuatia walikuwa na wajibu wa kuhakikisha njia hiyo inapitika lakini
serikali ya CCM imeamua kuziba njia hiyo.
Huku
akisoma takwimu za maendeleo katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki,
linaloongozwa na Dk. Lucy Nkya (CCM), Dk. Slaa alisema kuwa hakuna sababu ya
kuendelea kukivumilia chama hicho kwa sababu ya kufanana kwa rangi na badala
yake wananchi wanapaswa kuchukua hatua ya kukipumzisha.
“Kila
mmoja hapa amesikia takwimu nilizosoma, tena zinatokana na vitabu vya serikali
yenu hii mliyoichagua na kuiweka madarakani, mlichagua rais wa CCM, mbunge wa
CCM, Diwani wa CCM, mwenyekiti wa kijiji na serikali ya kijiji ya CCM, sasa
nawasomea hapa ufisadi unaofaywa mnaanza kusikitika,” alisema.
Alisema ni aibu miaka 50
baada ya Uhuru kusikia Watanzania wakizungumzia upungufu wa madawati wakati
nchi nyingine zikiwa zinashindana kwenda kuangalia uwezekano wa kufanya utafiti
utakaozisaidia nchi zao.
No comments:
Post a Comment