Hali ya kisiasa nchini ambayo inajumuisha chaguzi mbalimbali 
zilizofanyika ukiwemo ule wa Arumeru Mashariki ambao Chama cha Mapinduzi
 (CCM) kilipoteza jimbo,  ni miongoni mwa mambo ambayo yanatarajiwa 
kuvitikisa vikao vya Kamati Kuu, (CC) na Halmashauri Kuu ya chama hicho.
Katika uchaguzi huo ambao ulifanyika 
baada ya mbunge wake Jeremia Sumari kufariki dunia, mgombea wa Chama cha
 Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joshua Nassari aliibuka kidedea.
Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na 
Uenezi, Nape Nnauye, jumla ya agenda 14 zitajadiliwa katika kikao hicho 
ambacho kilianza jioni jana.
Alisema hali ya kisiasa nchini ni miongoni mwa agenda ambazo zitakazojadiliwa katika kikao hicho.
Hata hivyo, alisema wanakusudia kuifanya 
agenda ya pekee ya hali ya uchumi ambayo kwa sasa huingizwa katika hali 
ya kisiasa.  “Si mnafahamu kwamba hapa katikati kumefanyika  chaguzi 
nyingi, zikiwemo za ndani ya chama ni miongoni mwa mambo 
tutakayojadili,”alisema Nape.
Alisema uchaguzi katika mashina na baadhi
 ya matawi umeshafanyika na kwamba watapokea taarifa ya maendeleo ya 
chaguzi hizo ili kama kuna jambo la kushauri wafanye hivyo.
Nape alisema agenda nyingine itakuwa 
itokanayo na vikao vilivyopita,  taarifa mbalimbali na uchaguzi wa 
kujaza nafasi za makatibu wa mikoa.
Aliitaja baadhi ya mikoa hiyo kuwa ni Iringa na Dodoma.
Hadi tunakwenda mtamboni kikao cha Kamati
 Kuu kilikuwa kikiendelea baada ya kikao cha kamati ya maadili 
kilichokuwa kianze saa 4.00 asubuhi kuanza  saa 7.30 na kumalizika saa 
11.00 jioni.

 
 
No comments:
Post a Comment