To Chat with me click here

Tuesday, September 4, 2012

DK. SLAA AMBANA IGP


WAFANYA KIKAO CHA DHARURA NA KUWEKEANA MASHARTI MAGUMU

Dr. Willbrod Slaa
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, kuunda tume huru ya kushughulikia vifo vinavyotokea katika hali za utata, hasa vinavyohusisha jeshi hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kumaliza kikao chake na IGP Mwema, Dk. Slaa alisema wamemwambia ikiwa Jeshi la Polisi litaendelea kung’ang’ania kujichunguza katika matukio ya kihalifu huku wakiwa ndio watuhumiwa, CHADEMA hakitakuwa tayari kutoa ushirikiano.

“Tulimwambia ni lazima sheria zifuatwe, na haziwezi kufuatwa kama polisi watajichunguza wenyewe; kwa maana katika hatua hii ya awali tayari wamekwisha kuonesha hali ya kutoaminika kwa kusema milipuko ile ilibebwa na waandishi wa habari,” alisema Dk. Slaa.

Aliongeza kuwa katika hatua hiyo ya awali, walikubaliana na IGP Mwema kuunda kamati ya kufuatilia na kupokea malalamiko.

Kwa upande wa CHADEMA, ameteuliwa Tumaini Makene, na kwa upande wa Polisi atakuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Kamishna Robert Manumba. Kamati hiyo imeanza kazi jana.

Alisema makubaliano mengine ni IGP kuruhusu mikutano ya ndani ya CHADEMA kuendelea, na kutoa amri kwa askari wa Mkoa wa Iringa kuruhusu watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo kupelekewa chakula.

Aliongeza kuwa katika makubaliano hayo walimueleza IGP kuhakikisha kila maelezo yake yanayofanyika kati yao na CHADEMA yanakuwa katika maandishi, kwa kile alichoeleza kuwa mara nyingi walipokubaliana, polisi wamekuwa wanageuka.

Kutokana na hilo, CHADEMA imeamua kusitisha ratiba zake kwa siku mbili kupisha shughuli za mazishi. Baada ya hapo, wataendelea na ratiba ya awali ya kujenga chama chao.

Vilio vyatawala Iringa
Nyumbani kwa marehemu Daudi Mwangosi kulitawaliwa na vilio na majonzi. Watu walikaa katika makundi kujadili tukio la kuuawa kwa mwandishi huyo aliyekuwa akifanya kazi katika Kituo cha Televisheni cha Channel Ten.

Wakati watu wakiwa katika hali hiyo, klabu ya waandishi wa habari mkoani hapa imetangaza kususia shughuli zote za Jeshi la Polisi mpaka watakapotoa maelezo ya kueleweka juu ya kuuawa kwa mwandishi huyo ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoani Iringa (IPC).

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Msaidizi wa klabu hiyo, Francis Godwin, alisema wamesikitishwa na matamshi yaliyotolewa na jeshi hilo kuwa bomu lililomuua mwandishi huyo lilitoka kwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

“Tunashindwa kuielewa kauli hii ya Jeshi la Polisi. Iweje bomu wanalodai limerushwa na wafuasi wa CHADEMA liende kumdhuru mwandishi huyo peke yake wakati alikuwa ameshikiliwa na mmoja wa askari wa jeshi hilo baada ya kupigwa virungu, kwa vile tu alitaka kujua sababu za mwandishi mwenzake kukamatwa?” alihoji Godwin.

Ili taarifa hiyo potofu isiendelee kusambaa, aliomba vyombo huru kuingilia kati ili kupata ukweli wa tukio hilo.

Aliongeza katika maazimio yao ya kutoshirikiana na Jeshi la Polisi kuanzia jana, waandishi wa habari wamekubaliana kutokwenda katika ofisi ya kamanda wa polisi mkoani humo kupata habari ya matukio ya kila siku. Aliwaomba waandishi wa mikoa mingine kuwaunga mkono, kwa kuwa msiba huo unawakilisha manyanyaso wanayofanyiwa waandishi nchini kote.

Alisema kwa kuanza waliwataka waandishi wote walio katika Kamati ya Wiki ya Nenda kwa Usalama mkoani hapa kujitoa katika kazi hiyo na kuacha kuripoti matukio yatakayofahamisha shughuli za Jeshi la Polisi, huku akiomba tukio zima la msiba lisiingiliwe na wanasiasa.

Aliongeza kuwa taratibu za kujua mwili wa marehemu utazikwa lini na wapi ni mpaka wawasiliane na ndugu wa marehemu, ingawa taarifa za awali zilisema kuna mpango wa mwili huo kusafirishwa kupelekwa wilayani Tukuyu, Mbeya kwa mazishi.

Wakati huohuo, nyumbani kwa marehemu Daudi Mwangosi umati wa watu uliokusanyika ulilaani tukio hilo na kueleza hali hiyo inasababisha wananachi wazidi kuichukia serikali. Mmoja wa waombolezaji hao, Mwasonga Lusekelo, alisema serikali inapaswa kuacha shughuli za kisiasa kuendelea na kwamba wananchi ndio wenye uamuzi wa kuchuja pumba na mchele.

Alisema kitendo cha kuendelea kuzuia shughuli za kisiasa ni kuzidi kuipa sifa na kuzidisha imani kwa wananchi kuwa serikali ina mambo mazuri ambayo haitaki wananchi wayajue.

Kwa upande wake mke wa marehemu, Itika Mwangosi, hakuweza kuelezea chochote zaidi ya kulia huku akilalamika kuwa mumewe ameshindwa kurudi nyumbani.

“Mwangosiii, Mwangosi uliondoka ukiahidi kurudi mbona sasa hujarudi, limerudi jina lako tu eeeeh Mungu, kwanini wameniondolea mume wangu?” alisikika akilia mke wa marehemu Mwangosi.

Marehemu Mwangosi ameacha mjane na watoto wanne na kati ya hao wavulana ni watatu.

No comments:

Post a Comment