Mhe. Joseph Mbilinyi (Sugu) |
MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi
(CHADEMA), amemuumbua Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip
Mulugo, akidai hatishwi na kauli zake kwani ana elimu ya kuungaunga akiwa
ametumia jina la mtu mwingine.
Kauli ya Mbilinyi maarufu kama Sugu,
inakuja siku chache tangu Mulugo atangaze kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
kitayarejesha majimbo yaliyoko mikononi mwa CHADEMA mkoani Mbeya, likiwemo la
Mbeya Mjini.
Akizungumza jana kwa simu na Tanzania
Daima, Mbilinyi alisema anamshangaa Mulugo kwa kauli hiyo wakati akiwa na hali
mbaya kisiasa jimboni kwake Songwe, kiasi cha walimu kulalamika kukosa hata
chaki shuleni.
“Mimi Mulugo hanitishi hata kidogo
maana mambo yake yote ni ya kuungaunga, kuanzia elimu yake hadi siasa jimboni.
Huyu nimesoma naye Sekondari ya Mbeya Day nikiwa namtangulia, na jina lake
alikuwa akiitwa Amim si hili la Philip Mulugo,” alisema.
Mbilinyi aliongeza kuwa amefanya ziara
jimboni kwa Mulugo na kuelezwa matatizo mengi yanayowakabili wapiga kura wake,
na kwamba alishangazwa na hatua ya kuona walimu wakilalamika kukosa chaki
wakati mbunge wao ni naibu waziri wa elimu.
“Haya mambo hatuyasemi kwa sababu ya kuwachukia
CCM, bali wanatuletea wenyewe malalamiko wakitaka tuwasaidie kusema. Sasa
Mulugo kashindwa kwake anakuja Mbeya Mjini kujitapa kuwa wataning’oa,” alisema.
Aliongeza kuwa, kutokana na ubabaishaji
wa Mulugo, kuanzia sasa ataanza kumuita jina lake halali la Amim ili watu
wafahamu kuwa hata kweli elimu aliunga licha ya kuteuliwa kuwa naibu waziri.
“Kila mtu anakuwa na ndoto,
haikataliwi, hata yeye alipotoka hadi kuwa Naibu Waziri wa Elimu ni ndoto pia,
hakutegemea kutokana na kusoma kwa kuungaunga kwa kutumia jina na cheti cha
mtu, hakuwa na uwezo,” alisema.
Mbilinyi alifafanua kuwa Mulugo
amemchokoza mwenyewe na kumtaka atambue kuwa yeye si wa kuchezea wala chama
chake cha CHADEMA, na kwamba chama hicho chini yake au mtu mwingine kuliacha
Jimbo la Mbeya Mjini ni baada ya miaka 25 ijayo.
Alisema kutokana na kupendwa na watu na
kuwapa changamoto katika halmashauri licha ya kwamba CCM wana madiwani 22 na
CHADEMA 14, anaamini kabisa kwa sasa atajipanga kugombea umeya badala ya
ubunge.
“Yaani Mulugo amechemsha, hakuna namna
ya kumtoa Sugu wala chama chake, na sasa itafika wakati nitakuwa meya, tena
pale ndio wamechemsha kabisa kumweka mwenyekiti asiyekubalika, na sasa
wakifanya mikutano yao hawapati watu.
“Mulugo ndiyo maana hata historia ya nchi
haijui kwa kuwa elimu yake yenyewe ina utata, aanze kuchunguzwa, mtaniambia
kafanya jambo la ajabu sana, mwenzake alifaulu, lakini kutokana na kutokuwa na
uwezo wa kuendelea na shule yeye akanunua jina lake,” alisema.
Mbilinyi alisema kama Mulugo anahitaji
kuendelea na siasa, basi aende Mbeya Mjini ili wamfundishe jinsi ya kuishi na
watu jimboni kwake na kujua kero zao.
Hata hivyo, Mulugo alipotafutwa
kufafanua madai hayo, alikwepa kulisemea sakata la kutumia jina lingine wakati
akisoma sekondari, akisema kuna vitu ni stori, lakini fitina hizo za kisiasa ni
majungu ya mtu na mtu.
Aliongeza kuwa, Mbilinyi aliwahi kwenda
jimboni kwake Songwe na kusema madai hayo pamoja na kumtukana, lakini wananchi
walimzomea wakisema wao ndio wanamfahamu mbunge wao kuanzia elimu ya msingi
mpaka shahada.
“Matusi yale yalisababisha vurugu mpaka
CHADEMA wakapata kura 19 dhidi ya kura 365 za CCM. Nilichokisema kwenye mkutano
wa Mbeya ni jambo la kawaida kwa mwanasiasa yeyote aliye makini, tena mjumbe wa
NEC.
“Nilisema majimbo yote ya CHADEMA Mkoa
wa Mbeya tutayarudisha. Sasa kwani mbona wao kila siku wanasema watachukua
majimbo yote ya Mkoa wa Mbeya?” alisema Mulugo kupitia ujumbe mfupi wa sms.
No comments:
Post a Comment