To Chat with me click here

Thursday, May 2, 2013

TUHUMA: VIGOGO, WAKALIA MABILIONI YA CIS



Mhe. Kimbisa
Dar es Salaam. Baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara na wizara kadhaa za Serikali za Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wameendelea kukalia mabilioni ya shilingi waliyokopa kupitia uliokuwa Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa kutoka nje ya Nchi (Commodity Import Support - CIS).

Taarifa ambazo zimetufikia zinasema kiasi cha fedha ambacho bado hakijarejeshwa na wakopaji hao ni Sh216 bilioni ambazo kama zingepatikana, zingetosha kugharimia madawati milioni 2.7 kwa gharama ya Sh80,000 kila moja yenye uwezo wa kutosheleza wanafunzi milioni 8.1.

CIS ni mpango ulioanzishwa na Serikali miaka ya 1980 na kuendelea hadi mwanzoni mwa miaka 2000, ambao nchi wahisani zikiongozwa na Japan zilikuwa zikiipatia Serikali fedha za kigeni ili kuimarisha sekta za biashara.

Nchi nyingine zilizochangia fedha hizo ni Uingereza, Uholanzi, Saudi Arabia, Norway, Uswisi, Ubelgiji, Sweden na Denmark na madeni yaliyotokana na fedha hizo ni sehemu ya deni la taifa ambalo linagharimiwa na fedha za walipakodi wa sasa.

Hata hivyo, taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa mpango huo ni kama ulihujumiwa na baadhi ya waliochota fedha hizo kwani walizitumia kinyume cha makusudio na sasa ni kama Serikali imeshindwa kuzirejesha licha ya kumwajiri mkusanyaji kwa mwaka mzima.

Fedha hizo zilitakiwa kutumika kununulia malighafi, vyombo vya usafiri wa barabara, vifaa vya kilimo na ujenzi, wakati huo hali ya uchumi hususan ya upatikanaji wa fedha za kigeni ilikuwa mbaya, hivyo mpango huu ulikuwa usaidie kuinusuru hali hiyo.

Mwanzoni mwa 2011, Serikali iliingia mkataba wa mwaka mmoja na kampuni ya udalali ya Msolopa Investiment Limited ambayo kwa mujibu wa taarifa za uhakika, mkataba wake ulimalizika Januari mwaka jana bila kutimiza lengo la kurejesha mabilioni hayo.

Mkataba huo ulifikia ukomo huku Msolopa ikiwa imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh5 bilioni, sawa na asilimia 2.31 tu ya Sh216 bilioni ambazo bado zinadaiwa mikononi mwa wakopaji. Mkurugenzi wa Kampuni ya Msolopa, Ibrahim Msolopa alikataa kuzungumzia suala hilo akisema hana mamlaka...
“Mkataba wangu na Serikali juu ya suala hilo ulishafikia ukomo, nimeshakabidhi kila kitu kinachohusu CIS kwa Serikali kwa hiyo kama mnahitaji taarifa yoyote nendeni serikalini.”

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema halifahamu suala la watu kudaiwa fedha za CIS... “Ninahitaji muda wa kulifuatilia suala hili na kufahamu undani wake.”

Vigogo wanaodaiwa
Uchunguzi umebaini kuwa fedha hizo zimekaliwa na wafanyabiashara na wanasiasa kupitia kampuni zao wakiwamo wabunge wa CCM, Abbas Mtemvu (Temeke) na Henry Shekifu (Lushoto), Wenyeviti wa CCM wa mikoa, Ramadhan Madabida (Dar es Salaam) na Adam Kimbisa (Dodoma).

Kampuni ya Shamshi & Sons ya Shekifu ilikopa Yen za Kijapani 12,778,082.81 (sawa na Sh.207 milioni) kwa kuzingatia viwango vya sasa vya kubadilisha fedha ambavyo ni wastani wa Sh16.20 dhidi ya Yen moja.

Kampuni ya Cargo Plan International, ambayo mmiliki wake ni Kimbisa ilikopa Yen 2,882,961.79 (zaidi ya Sh46.7 milioni), wakati Tanzania Pharmaceutical inayomilikiwa na Madabida ilikopa Yen 7,031,983.29 (takriban Sh114 milioni).
Kampuni ya A.M.General Agency inayomilikiwa na Mtemvu ilikopa Yen 20,000,000 (sawa na Sh324 milioni). Taarifa zinaonyesha kuwa madeni hayo hayajalipwa.

Shekifu
Shekifu alipohojiwa alisema: “Hayo mambo ni ‘sensitive’ (nyeti) kidogo, siwezi kuzungumza na wewe kwa simu. Kwanza sikufahamu, nakushauri unitafute tuonane ana kwa ana, unaweza kufanya hivyo kesho. Niko kwenye Kamati za Bunge.”

Kesho yake alipofuatwa kwenye Ofisi za Bunge Dar es Salaam mazungumzo yake na mwandishi wetu yalikuwa hivi:
Shekifu: Ehe, mwanangu unasemaje?
Mwandishi: Mimi ndiye tulizungumza kwa simu, ukataka nikufuate ili tuzungumzie suala la deni la fedha za CIS.

Shekifu: Unajua nyie waandishi wa habari ni watu hatari sana na suala hili ni nyeti siwezi kulizungumzia kijuu juu tu. Nahitaji muda wa kutosha, unieleze unachofahamu kuhusiana na suala hilo kwa sababu unaposema nadaiwa CIS, nini maana ya CIS?
Mwandishi: CIS ni mifuko iliyoanzishwa na nchi mbalimbali za nje kuwezesha biashara za kimataifa baina yake na wafanyabiashara wa Tanzania; Japani ni moja kati ya nchi hizo na mfuko wake ndiyo unaokudai Yen 12,778,082.81 zilizokopwa kupitia Kampuni ya Shamshi & Sons.

Shekifu: Sikiliza mwanangu, nimekwambia muda huu siwezi kuzungumza chochote, nyie waandishi ni hatari. Hivi unafahamu hata mimi ni mwandishi wa habari ‘by professional’ (kitaaluma),  nimesoma Nyegezi inaelekea haujasoma historia yangu eh? Kasome kwanza historia yangu, mimi ni mwandishi wa habari.
Mwandishi: Kwa maana hiyo unakanusha kudaiwa na CIS?
 
Shekifu: Siwezi kukubali wala kukataa, nahitaji muda wa kutosha ili nizungumzie suala hili. Nakushauri unitafute wakati mwingine, unaweza kunitafuta hata keshokutwa (Ijumaa Kuu).
Mwandishi: Lakini mheshimiwa jana ulinishauri nikufuate hapa ili tuzungumze, sasa unaniambia upo kwenye mkutano nikufuate keshokutwa, umesahau itakuwa Ijumaa Kuu?

Shekifu: Ni kweli mimi nilifikiri labda unataka kuniona. Unajua kuna watu wengine huwa wanakuwa na hamu ya kukutana na sisi ana kwa ana, kiubinadamu tu, nikaona nikuruhusu uje tuonane lakini kuhusu mazungumzo; hapana haiwezekani yaani nyie waandishi bwana! Unataka uje useme nilimuhoji Shekifu wakati natakiwa kuwa kwenye kikao cha kitaifa, hapana hapana, nitafute wakati mwingine tafadhali.

Madabida
Alipoulizwa kuhusu madai hayo Madabida alisema:
“Ninachofahamu TPL haidaiwi hata senti moja na CIS, wewe una ushahidi wa kuonyesha kuwa tunadaiwa? Unafahamu deni halisi lilikuwa kiasi gani, lilichukuliwa lini, likalipwa kiasi gani na balance (salio) ni kiasi gani?  Nieleze hizo taarifa kwanza ndipo niwe katika nafasi nzuri ya kuzungumza na wewe hicho unachonieleza.”

Mwandishi: Ninachohitaji ni ufafanuzi tu sasa ukitaka nikueleze hayo inamaanisha wewe ndiye unayenihoji. Hata hivyo, kwa kuwa umeshaeleza kuwa hamdaiwi hata senti moja, nimekuelewa.
Madabida: Hakuna, nina hakika ili unihoji lazima unieleze unachofahamu juu ya suala unalotaka nikueleze, kwa ufupi awali TPL ilikuwa inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Mwaka 1997 tulipoichukua tulikutana na madeni nakumbuka likiwamo hilo la CIS lakini yote yalilipwa na Serikali.

Mwandishi: Ikiwa hivyo ndivyo, mbona deni linasomeka kuwa anayedaiwa Yen 7,031,983.29 ni wewe na siyo Serikali?
Madabida: Inasomeka nadaiwa mimi kama mtu binafsi?
Mwandishi: Ingekuwa unasomeka hivyo ningekueleza hivyo tangu awali, unadaiwa wewe kupitia Kampuni ya TPL, kwa nini isionekane inadaiwa Serikali kupitia kampuni hiyo? Mbona wizara zilizokopa zinaonekana kuwa zilikopa kama wizara?
Madabida: Sasa hayo mimi sifahamu, labda uwaulize hao waliokuambia.

Kimbisa
Mwandishi: Tunafuatilia taarifa za makusanyo ya madeni ya CIS.  Kampuni yako ni moja kati ya zinazoonekana kuwa bado zinadaiwa, tunaomba kusikia kutoka kwako kiasi cha fedha unachotambua kuwa kampuni yako inadaiwa.
Kimbisa: Hata mimi sina uhakika wa suala hilo, lakini kwa kumbukumbu nilizonazo, tulimalizana na hao watu siku nyingi sana.
Mwandishi: Lakini taarifa tulizonazo kampuni yako bado inadaiwa, tulichotaka ni kufahamu unavyolichukulia deni hilo
Kimbisa: Nafikiri ingekuwa vizuri kama ungewasiliana na hao watu, nahisi wanachanganya mambo kwa sababu nakumbuka tulimalizana nao.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo Mtemvu alisema: “Data zenyewe hata sina, hizi habari zimeishaandikwa mara nyingi wewe kama unataka kufahamu chukua magazeti ya zamani usome.”

No comments:

Post a Comment